Sambaza....

NILIMUONA mshambulizi raia wa Zambia, Obrey Chirwa jukwaani wakati mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu Tanzania Bara Yanga SC ikiendeleza ´dozi´ ya vichapo kwa Alliance School Academy Jumamosi iliyopita.

Chirwa- mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita alikuwa amekaa kando ya viongo wa Yanga na alionekana mwenye furaha muda wote. Taarifa za awali zinadai mshambulizi huyo aliyefunga magoli 24 ya ligi kuu Bara katika misimu miwili iliyopita anarejea Tanzania na Yanga itamsaini wakati wa dirisha dogo la usajili mwezi ujao.

NI USAJILI SAHIHI…

Kama kweli Yanga wanahitaji kurejesha ubingwa walioupoteza msimu uliopita wanapaswa kuboresha kikosi chao katika usajili mdogo na kati ya nafasi wanazopaswa kuzifanyia nyongeza ni nafasi ya mashambulizi na ile ya ulinzi.

Kumuongeza Chirwa itakuwa Jambo zuri kwani licha ya safu hiyo kufunga magoli 14 katika michezo saba waliyokwishacheza bado washambuliaji Herieter Makambo, Amis Tambwe, Matheo Anthony na Yusuph Mhilu wameshindwa kuwa wabunifu.

Chirwa ataongeza magoli- hakuna shaka kuhusu hilo, lakini zaidi ataongeza utulivu na fursa ya Yanga kutengeneza magoli zaidi. Chirwa ni mshambulizi mwenye mbinu za kutafuta penalti, ana uwezo mkubwa wa kukaa na mpira na pia ni mpambanaji mwenye uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga kwa wenzake.

 

Kumrejesha Mzambia huyo ni Sawa na kuongeza ´bunduki´ muhimu vitani hasa ukizingatia wapinzani wao katika mbio za ubingwa Azam FC na Simba SC wana safu za mashambulizi zinazowapa wigo mpana wa uchaguzi makocha wao.

Raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma, Tafadwa Kutinyu, Mghana, Enock Atta, Mbaraka Yusuph, Daniel Lyanga na kinda Yahya Zaydi wanampata machaguo mengi ya washambuliaji wa kati kocha wao Hans van der Pluijm katika timu ya Azam FC.

Wakati Mnyarwanda, Meddie Kagere, Mganda, Emmanuel Okwi, Marcel Kaheza, Adam Salamba, John Bocco na Mohamed Rashid wakimpa fursa pana ya uchaguzi wa washambuliaji kocha Patrick Aussems katika kikosi cha Simba.

Yanga licha ya kufunga wastani wa magoli mawili katika kila mchezo- safu yao ya mashambulizi itakuwa bora zaidi kama watamuongeza Chirwa.

Vilevile, ijapokuwa beki yao imeruhusu magoli manne hadi sasa hawapaswi kudharau kuhusu mianya kati beki ya kati na ile ya kulia. Vicent Andrew, Abdallah Haji hawatoshi kusaidiana na nahodha Kelvin Yondan katika beki ya kati na kocha Zahera Mwinyi anapaswa kusaidiwa kuongeza beki wa kati mwenye uzoefu mkubwa, pia beki wa kulia ambaye atamsaidia kinda Paul Godfrey.

Kumrejesha Chirwa ili kuungana na Tambwe, Makambo, Mhilu na Matheo katika mashambulizi ni sawa, lakini Yanga wanatakiwa pia kuitazama ngome yao vile inavyopepesuka wakati wanaposhambuliwa na kuifanyia nyongeza ili iwe imara.

Sambaza....