Sambaza....

Kuna aina ya wachezaji wawili uwanjani. Aina ya kwanza ni mchezaji bora na aina ya pili ni mchezaji muhimu. Hawa wote hukaa kwenye timu moja.

Hujenga timu moja na huitajika kwa pamoja ili kukamilisha neno timu. Mchezaji bora mara nyingi huyu ndiye ambaye hutazamwa kwa jicho pana sana.

Kila mtu humtazama kutokana na kipaji chake kikubwa kuzidi wengine , kwa kifupi tunaweza kumwiita kama “Gifted Player”.

Ana kitu cha ziada ambacho mchezaji mwingine hana au hawezi kukifanya. Hawa ndiyo huwa wanaibeba timu kipindi ambacho timu imezingirwa na giza.

Hawa hutokea sehemu ambayo huwezi kutarajia huku miguu yao ikiwa na taa kwa ajili ya kuleta nuru kwenye giza la timu.

Hawa wako wachache sana na huzaliwa kwa nadra sana na siyo kazi nyepesi sana kuwapata kwani inahitajika kazi kubwa sana kuwapata.

Na wakati mwingine hutokea kwa kizazi kimoja na kizazi kingine. Kuna wakati kizazi cha miaka ya 1970 kilimshuhudia Pelle.

Kizazi cha 1980 kikaja kumshuhudia Diego Maradona. Alipotoka tu kwenye uso wa dunia ya mpira kilikuja kizazi sukari, kizazi kitamu , kizazi cha dhahabu.

Dunia ilishuhudia rundo la wachezaji wengi bora kama kina Ronaldo De Lima, Ronaldinho, Zidane na wengine.

Muda uliwasukuma nje ya ulingo wa mpira wa miguu na muda huo huo ukawaleta kina Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Wachezaji bora kabisa wa muongo mmoja uliopita. Wachezaji ambao tunaweza kuwaita ” Gifted Players” kutokana na uwezo wa ndani ya uwanja.

Uwezo wa kufanya maamuzi wakati mgumu kwa manufaa ya timu. Uwezo mkubwa wa kuusoma mchezo ndani ya uwanja.

Kwa kifupi hawa hujitofautisha kabisa na wengine. Hawa tunaweza kuwaita kama jiwe kuu. Lakini pembeni yao huwa kuna mawe madogo madogo.

Mawe ambayo husababisha jiwe hili kuu liweze kusimama ipasavyo, ndipo hapo tunapokuja kuwapata wachezaji muhimu ndani ya kikosi.

Hawa kuna wakati unaweza kuwadharau sana ndani ya kikosi na kuona labda wanauwezo wa kawaida lakini umuhimu wao hutokona na kocha.

Kocha ambavyo huamua kuitengeneza timu yake. Kwa mfano, Chelsea ya Antonio Conte kulikuwa na wachezaji bora kama Eden Hazard na Ng’olo Kante.

Hawa ndiyo walikuwa wachezaji bora kwenye kikosi cha Muitalia huyo, lakini kwa mfumo wake wa 3-4-3, wachezaji kama Marcus Alonso na Victor Moses walibaki Kuwait wachezaji muhimu.

Sarri, Kocha wa Chelsea

Leo hii Chelsea ya Mauricio Sarri hamtazami tena Victor Moses katika umuhimu mkubwa kwa sababu tu mfumo wa Mauricio Sarri haumwangalii Victor Moses tena.

Mauricio Sarri hatumii tena Wingback kama ambavyo Antonio Conte alivyokuwa anamtumia vizuri Victor Moses.

Timu yake ameitengeneza kwa kuwekeza umuhimu wa mfumo wake kwenye miguu ya Jorginho, huyu anabaki kuwa mchezaji muhimu kwenye mfumo wa Sarri.

Hata Simba ya msimu jana Asante Kwasi alikuwa mchezaji muhimu ndani ya kikosi kwa sababu moja tu, walimu ambao waliifundisha waliwekeza umuhimu wa mfumo wao kwa Asante Kwasi.

Wote Pierre Lenchantre na Masoud Djuma walimchezesha Asante Kwasi kama Wingback, na alionekana mchezaji muhimu dhidi ya Mohammed Hussein.

Lakini pamoja na Asante Kwasi kubaki kuwa mchezaji muhimu , Emmanuel Okwi alibaki kuwa mchezaji bora ndani ya kikosi cha Simba.

Hata kikosi cha sasa cha Patrick Assumes, Emmanuel Okwi , Chama wanabaki kama wachezaji bora ndani ya kikosi cha Simba.

Ila kuna wachezaji muhimu sana kwenye mfumo wa sasa wa Simba. Ukiachana na beki Paschal Wawa, mchezaji mwingine muhimu ndani ya mfumo wa Simba ni John Bocco. Huyu ndiye mshambuliaji ambaye amecheza dakika nyingi kuliko washambuliaji wote wa Simba msimu huu. Unajua kwanini?

John Bocco hutumika kama beki wa kwanza kwa kuanzia kukabia juu hasa hasa kwenye mechi za ugenini.

Pili, John Bocco anauwezo wa kufikia eneo kubwa la uwanja kuliko mshambuliaji yoyote ndani ya kikosi cha kwanza.

Kwa kifupi John Bocco ni mzuri wakati timu ikiwa haina mpira kuliko Emmanuel Okwi na Meddie Kagere. Na ikizingatia timu iko ugenini dhidi ya timu ngumu, John Bocco alitakiwa kuwepo kuisaidia timu kukaba.

Hivo Simba wanaenda kwenye mchezo wa Leo bila beki wao wa kwanza. Tatu, John Bocco anapokuwa anakimbia hutengeneza uwazi.

Uwazi ambao hutumia na washambuliaji wa Simba. Pia anapokuwa ameshuka chini katikati au pembeni, hushuka na beki mmoja wa kati.

Akishuka na beki mmoja wa kati, nyuma hubaki na uwazi , uwazi ambao hutumiwa na kina Okwi na Kagere. Hivo, John Bocco kutokuwepo kwake kunapunguza idadi ya uwazi kwa mbele.

Sambaza....