Sambaza....

WAKATI uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba SC ukitaraji kufanyika Novemba 3 mwaka huu. Mwenyekiti wa klabu atakayeingia katika bodi ya ukurugenzi na wajumbe. Ukiachana na muitikio mdogo kwa waliojitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti, Simba inaweza kupata mtu wa mpira-Mtemi Ramadhani mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na ‘mtu hasa wa Simba’ Swedi Nkwabi.

Pia wapo wanachama zaidi ya 20 waliojitokeza kuwania nafasi ya ujumbe. Ni vizuri, lakini tangu mwanzo wa mchakato wa mabadiliko ya kiuendeshaji klabu-kutoka mfumo wa kutegemea wanachama hadi kuingia katika soko la hisa niliamini klabu hiyo inafanya haraka kupitisha mabadiliko hayo na bila shaka watakuja kuyajutia.

Mohamed Dewji anataraji kuwa mwekezaji atakayemiliki asilimia 49 ya hisa za klabu. Simpingi Mo lakini nitaendelea kutokubali namna alivyojitahidi kuhakikisha malengo yake yanatimia. Atawekeza Tsh. 20 bilioni lakini kumbuka tajiri huyo amekuwa akiisaidia klabu yake kwa mtindo wa kuikopesha na inasemekana tayari deni hilo limefikia Tsh 6 bilioni katika kipindi cha miezi 30 iliyopita.

Wanachama wa Simba Wakiwa katika moja ya Mkutano
Wanachama wa Simba Wakiwa katika moja ya Mkutano

Nilikuwa nikiamini kuwa mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ulipaswa kuchukua walau miaka miwili hadi mitatu, na kitendo cha kuwahishwa na kupelekwa haraka haraka ilikuwa ni kwasababu ya kuhakikisha watu Fulani wanachukua nafasi na wengine ambao kimsingi ni wengi-waanzilishi wanawekwa kando.

Je, mwenyekiti wa klabu ya soka anahitaji elimu ya digrii ili klabu ifanikiwe? Kwanini wazee kama Mzee Hassan Dalali wananyimwa nafasi za uongozi kwa kigezo cha umri wa miaka 65? Nani aliyeweka kanuni/sheria hizi katika katiba mpya ya Simba? Je, wanachama walikuwa makini kupitia katiba yao mpya kabla ya kuipitisha?

Wakati ule nilisema ‘njaa’ na ‘tamaa’ ya ubingwa wa ligi kuu ilichangia Mo kueleweka lakini baada ya kuwashibisha bila shaka kuna makosa mengi wanachama watajutia kutokana na uharaka walioufanya wakati ule wakipitisha katiba mpya ambayo inaruhusu mwekezaji kuwekeza kwa asilimia 49.

Tayari, klabu inaelekea kuwaondoa wenye Simba yao kwa kigezo cha elimu, si hivyo tu wanaelekea kupata viongozi ambao si watu kabisa wa mpira zaidi ni wafanyabiashara ambao wanatumia kinga ya kiwango cha elimu kuchuma na kula vya Simba. Katiba mpya ni sawa na kupitisha ‘uporwaji’ wa klabu kutoka kwa waanzilishi.

Ndiyo, MO anaweza kuijengea Simba uwanja, hostel na gym lakini hatafanikiwa kirahisi kwa sababu mambo mengi yalifanywa kwa ‘mhemko’ tu na si nia ya kuendeleza Simba ikiwa mikononi mwa watu wenyewe wa Simba.bila, Mtemi na Mkwabi leo hii Simba ilikuwa inakosa kiongozi, lakini licha ya wawili hao kujitokeza kwa kuamini wanakidhi vigezo vya kuwa wenyekiti, hatujui kama watapitishwa wakati wa mapingamizi na uhakiki.

Sambaza....