Kotei (Kushoto) akimthibiti Muleka wa TP Mazembe
Mabingwa Afrika

Waamuzi wa mchezo na TP Mazembe wabadilishwa, Simba walalamika.

Sambaza kwa marafiki....

Shirikisho la kandanda barani Afrika (CAF) limefanya mabadiliko ya waamuzi na maofisa wa mchezo utakaozikutanisha timu za soka za TP Mazembe na Simba SC katika mchezo wa marudiano utakaofanyika April 13 mjini Lubumbashi nchini DR Congo.

Barua ya CAF kwenda kwa vilabu vyote imesema kwamba mabadiliko hayo ni kutokana na sababu za kiufundi.

CAF imeonesha kuwa mwamuzi wa kati katika mchezo huo atakuwa Janny Sikazwe kutoka Zambia badala ya Bamlak Tessema Weyesa kutoka Ethiopia ambaye angepaswa kusaidiwa na Temesgin Samuel Atango kutoka Ethiopia  pamoja na Gilbert Cheruiyot kutoka Kenya.

Sikazwe atasaidiwa na Berhe Michael kutoka Eritrea na Romeo Kasengele kutoka Zambia huku mwamuzi wa akiba akiwa Audrick Nkole kutoka Zambia pia.

Wakati hayo yakijiri Klabu ya Simba imetuma barua ya malalamiko kwa CAF kufuatia mabadiliko hayo ya Ghafla kwa waamuzi wakisema kitendo hicho kinaleta giza kwenye macho yao hasa ukizingatia kuwa umbali kutoka Lubumbashi na Zambia kuwa mkaribu mno.

Barua hiyo iliyosainiwa na afisa mtendaji mkuu wa klabu ya Simba Crescentius John Magori, imewataka CAF kumrudisha mwamuzi wa mwanzo ili kuondoa wasiwasi ambao umeanza kujengeka kuelekea mchezo huo.

“Kwa weledi mkubwa tunaiomba ofisi yako kuingilia kati na kwa wakati suala hili ili kuhakikisha kwamba waamuzi wa hapo awali walioteuliwa kuchezesha mchezo huu wanarudishwa ili kuonesha kuunga mkono mchezo wa kiungwana, mabadiliko haya ya ghafla yanaleta minong’ono ukizingatia kuwa waamuzi wapya ni majirani kabisa na nchi ya DR Congo,” barua ya Simba imesema.

Mchezo kati ya Simba na TP Mazembe utapigwa katika uwanja wa Stade TP Mazembe uliopo mjini Lubumbashi ambapo kwa matokeo ya mchezo wa kwanza ya 0-0 itawalazimu Simba kutafuta ushindi ama sare ya mabao ili kujikatia tiketi ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.