Mlinzi wa Simba Mohamed Hussein akitafuta mbinu za kimthibiti mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele
Mabingwa AfrikaShirikisho Afrika

Yanga ina nafasi, Simba wanahitaji maombi kufuzu!

Sambaza....

Ni bahati iliyoje kwa nchi yetu katika soka la Kimataifa mpaka sasa tuna washiriki wawili katika michuano mikubwa kwa ngazi ya vilabu  Barani Afrika. Simba inashiriki hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika na Yanga wao wapo katika makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ni nadra sana kwa nchi yetu kutoa wawakilishi katika hatua hizo haswa kutokana na viwango vya vilabu vyetu na aina ya uwekezaji wetu tulionao nchini. Lakini sasa Simba ipo kundi C Ligi ya Mabingwa na Yanga wapo kundi D Kombe la Shirikisho wakitafuta kufuzu hatua ya robo fainali.

 

Tayari katika makundi timu zote nne zimeshakutana kwa maana kila timu imeshakutana na wapinzani wao baada ya kushuka dimbani mara tatu kila mmoja.

Ili timu ifuzu kwenda robo fainali angalau inapaswa kukusanya si chini ya alama tisa katika kundi bila kujali sana magoli yakufunga au kufungwa. Simba waliwahi kutumia njia hii katika msimu wa mwaka 2019 mbele ya kina Ahly na As Vita na wakafuzu.

Fiston Kalala Mayelle akishangilia bao lake dhidi ya Real Bamako

Kwa Upande wa Yanga!

Yanga wakiwa Kundi D mpaka sasa wamecheza michezo mitatu na wakipata matokeo yote ya soka, wamefungwa moja, sare moja na ushindi mara moja. Yanga imefungwa na Monastir, wakwafunga Mazembe nyumbani halafu wakapata sare dhidi ya Real Bamako.

Kimahesabu bado Yanga ipo katika njia sahihi yakufuzu katika kundi lao na kwenda robo fainali.  Yanga wamecheza mechi mbili ugenini na moja nyumbani lakini tayari wamekusanya apama nne.

Katika michezo mitatu iliyobaki Yanga wana michezo miwilo nyumbani ambapo katika soka la Afrika ndio sehemu muhimu yakupata ushindi kutokana na aina ya mchezo wenyewe Barani kwetu. Yanga watawakaribisha Real Bamako na US Monastir katika Dimba la Benjamin Mkapa.

Salum Aboubakar (kushoto) akimuacha kiungo wa US Monastir

Ni wazi Yanga wana kila sababu yakukusanya alama sita kwa ama nne kwa kuwafunga Bamako halafu kuwafunga ama kupata sare dhidi ya Monastir. Maana yake Yanga itakua na alama kumi kama watashinda zote ama nane kama watasare mchezo mmoja.

Mchezo dhidi ya Mazembe ambao utakua ugenini ni wazi Yanga watakwenda Congo kutafuta alama moja ama hata wakipoteza watakua na mtaji wa alama walizopata katika dimba la nyumbani na kuwafanya waweze kufuzu.

Na katika kundi hili kwa vyovyote vile TP Mazembe ndio mshindani mkubwa kwa Yanga, Real Bamako hawaonyeshi kuwa bora na ni wazi huenda wakamaliza wamwisho. Kwa upande wa Monastir wenye alama saba ni wazi huenda wakamaliza wakiwa vinara.

Kwa Upande wa Simba!

Tayari Mnyama anaeonekana kuwa na uzoefu wa michuano ya Kimataifa ameshuka dimbani mara tatu na kukusanya alama tatu pekee. Akifungwa mbili dhidi ya Horoya na Raja Casablanca huku yeye akishinda ugenini dhidi ya Vipers.

Simba wamebakiwa na michezo mitatu ambapo miwili watacheza nyumbani dhidi ya Vipers na Horoya na mchezo wa mwisho dhidi ya Raja ugenini nchini Morocco.

Simba wanahita kupata alama sita zote dhidi ya Horoya na Vipers kabla ya kwenda ugenini ambapo wana nafasi ndogo yakupata matokeo mbele ya Raja.  Endapo Simba akishinda michezo miwili ya nyumbani atakua na alama tisa na hivyo kuangalia Horoya watakua na matokeo gani.

Wachezaji wa Simba wakishangilia bao pekee la Henock Inonga dhidi ya Vipers

Hesabu za Simba ziliharibika baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo haswa wa nyumbani dhidi ya Raja, huku Horoya akipata alama moja ugenini dhidi ya Vipers na kumfanya awe na alama nne.

Kwa maana hiyo Simba anapaswa kumfunga Horoya nyumbani lakini pia akimuombea mabaya mpinzani wake huyo katika mchezo wake dhidi ya Raja unaofwata na wamwisho dhidi ya Vipers ambao Horoya atakua nyumbani.

Ama kwa hakika Simba ana wakati mgumu zaidi kufuzu ukilinganisha na Yanga ingawa kila kitu kinawezekana  katika soka.

Mzamiru Yasin (katikati) akiwatambuka wachezaji wa Raja Casablanca.

Hitimisho!

Yanga wana nafasi zaidi yakufuzu kutokana na mgawanyiko wa alama walizovuna baada ya michezo mitatu na kufanya vibaya kwa Mazembe kunawafanya wazidi kujiamini na kutafuta matokeo kwa nguvu. Hakuna mashaka Yanga wakishinda mechi zao bila kujali matokeo ya wapinzani watafuzu na kwenda robo fainali.

Kwa upande wa Simba wanapaswa kushinda nyumbani halafu wamuombee mabaya Horoya ama waende kufanya maajabu kule Morocco katika mchezo wao wamwisho ugenini dhidi ya Raja Casablanca kwani vi vigumu kwa Vipers kumzuia Horoya nyumbani kwake.

Sambaza....