Blog

Asante Magufuli kwa viwanja, tuchimbie na msingi

Sambaza....


Hili ni ombi langu, ombi ambalo sijawahi kukuomba hata siku moja kwa sababu tu siyo kila kitu tunatakiwa kukuomba wewe.

Hata ambavyo viko ndani ya uwezo wetu ni dhambi kubwa sana kunyanyua midomo yetu na kukuomba wewe.

Utatufikiriaje ?, hatujakomaa? , hatuwezi kusimama wenyewe kwa miguu yetu miwili ?. Ni aibu kubwa sana kwetu sisi na kwako.

Majirani watafikiria ni aina gani ya malezi ambayo ulituachia?. Hujui kutulea? . Hukutufundisha umuhimu wa sisi kujitegemea katika maisha yetu ?

Yani mpaka familia zetu wenyewe wewe ndiye ambaye uwe unahusika kuzilea?. Hii ni aibu kubwa sana. Aibu ambayo ilikuwa inanifanya nisite kukuomba hiki.

Nilikuwa naogopa kwa sababu hiki kilikuwa ndani ya uwezo wetu. Sema tu hatujawahi kuamua kabisa kukifanya hiki kitu.

Tuliowaamini kutuongoza hawajawahi kabisa kuamua kukifanya hiki ambacho ndicho kitu cha msingi kuzidi vitu vyote.

Kitu ambacho uti wa mgongo wa maendeleo ya mpira wetu wa miguu hapa Tanzania. Kitu ambacho ndicho kisima cha kutoa maji safi na salama katika mpira wetu.

Wakati uko kwenye hafla na timu yetu ya Taifa ya Tanzania kipi kilikuwa kinakuja kwako Mheshimiwa Raisi John Pombe Magufuli ?

Ulikuwa unawaza nini kuhusu wale wanajeshi ambao walisababisha uwape wito wa kuja Ikulu kwa ajili ya kula chakula cha pamoja na kuwapongeza ?

Ulikuwa unafikiria nini wakati unawatazama hao wanaume kwenye luninga mpaka ukafikia hatua ya kufurahia kama ulivyoonekana kwenye video yako ?

Ulifikiria ni wapi hao wanajeshi wako waliokupa furaha walikotoka?. Ni mfumo upi ambao umewafikisha mpaka hapo walipo ?

Mkuu, hapa ndipo panaponiuma na ndiyo sababu ya Mimi kukuomba hiki kitu. Kitu ambacho kiko ndani ya uwezo wetu lakini tuliowakabidhi madaraka wanatufanya tuone haliwezekani.

Tumepiga kelele sana. Tumeongea sana lakini hakuna kitu ambacho tumefanikiwa kukipata. Wewe ndiye baba yetu.

Baba ambaye hufurahia kila watoto zako tunapofanya vizuri. Na ni furaha ya wengi kuona tunaendelea kufanya vizuri.

Ndiyo maana kwa furaha kubwa uliamua kuwapa milioni 5 na viwanja kwa kila mchezaji aliyefanikisha sisi kwenda Misri.

Tunashurukuru kwa upendo huo. Lakini kuna kitu ungetufikiria. Kiwanja pekee hakitoshi kabisa. Hakitoshi mkuu.

Umetoa viwanja kwa watu ambao hatujui misingi ya maendeleo ya mpira wa miguu. Simaanishi kuwa ukawachimbie misingi wachezaji uliowapa viwanja kule Dodoma.

La hasha!, maana yangu ni hii hapa. Maendeleo ya mpira wa miguu yana msingi wake. Na msingi wake huanzia chini. Chini ambako ndiko kuna vipaji. Vipaji ambavyo vinatakiwa kuibuliwa, kulelewa na kukuzwa katika misingi imara.

Tunatakiwa tuwe na kituo kikubwa sana cha kuibua, kukuza na kulea vipaji tangu vikiwa na umri mdogo. Hapa ndipo tunapotakiwa kuwa.

Hapa ndipo palipo na msingi mkubwa wa furaha yetu. Hapa ndipo palipo na bomba linalotoa vijana wenye vipaji kwa ajili ya mafanikio ya timu yetu.

Furaha ambayo uliipata Ikulu, na furaha ambayo tuliipata sisi Watanzania wote siku ambayo tunaifunga Uganda ilikuwa furaha kubwa sana.

Hofu yangu ni moja tu. Hii furaha itajirudia lini tena ? . Tutasubiri tena baada ya miaka 39 kama tulivyosubiri awali ili kupata hii furaha ?

Kati ya makosa ambayo tuliyafanya mwaka 1980 baada ya kufuzu ni sisi kutokuwa na mwendelezo wa mafanikio baada ya hapo.

Yani ilikuwa kama tumebahatisha kufuzu, ndiyo maana ilituchukua tena miaka 39 ya sisi kufuzu tena. Tumefuzu tena kwa Mara ya pili, tumefikiria tena baada ya kufuzu?

Tumefikiria kujenga Taifa Stars imara ya kutuwezesha kufuzu tena ?. Hili swali ndilo ambalo limenifanya likuombe hiki kama Baba wetu.

Tufikirie kutujengea msingi imara wa mpira wetu ili hii furaha Iwe endelevu. Yani tusisubiri tena baada ya miaka 39 ili tuipate hii furaha, tusiwe watu kama ambao tunabahatisha kwenye mafanikio yetu.⊂

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x