Sambaza....

Jana nilikuwa mimekaa kwenye banda umiza nikiwa natazama mechi kati ya Tanzania Prisons na Yanga. Hapana shaka hii ni mechi ambayo ilikuwa na hisia kubwa sana kuzidi mechi zote ambazo zimechezwa msimu huu kwenye ligi kuu.

Ilikuwa mechi ambayo ilionesha namna gani ambavyo mashabiki wa Yanga wana mapenzi makubwa na timu yao.

Kuanzia kwenye banda umiza ambalo nilikuwa nimekaa lilikuwa limepambwa na mahaba ya mashabiki wa Yanga.

Mahaba ambayo yalijidhirisha kila Yanga ilipokuwa inapata goli, walishangilia kwa hisia sana na kuna wakati nilijiuliza leo hii Yanga inacheza dhidi ya Simba?

Jibu la swali langu lilikuwa na uhalisia ule ule wa mechi ya jana kuwa Tanzania Prisons ndiye aliyekuwa anacheza na Yanga.

Hata nilipokuwa natazama ndani ya uwanja, jinsi mashabiki wa Yanga walivyopokea ule ushindi nilikuwa bado siamini kama mechi ile ilikuwa dhidi ya Tanzania Prisons.

Nilijua ni mechi dhidi ya mtani wao wa jadi na hii ni kwa sababu hali ya hewa ndani ya uwanja ilikuwa yenye kutia moyo sana kwa wachezaji na benchi zima la ufundi.

Mashabiki walikuwa pamoja na wachezaji wao, waliwaonesha mapenzi ya hali ya juu. Waliupokea ule ushindi kwa furaha kubwa sana.

Kila nyuso ya shabiki wa Yanga ilitawaliwa na tabasamu nene. Tabasamu hili lilinifanya nikumbuke ule utaratibu wa kuchangia.

Swali ambalo lilikuja haraka haraka ni moja nalo ni kuwa huo mchango uliishia wapi ?, ulishindikana na kwanini ilishindikana ?

Unajua kwanini nilifikiria kuhusu huo utaratibu wa kuchagia ?, niliunganisha lile tabasamu la shabiki wa Yanga na tukio hili la kuchangia timu.

Huu ndiyo ulikuwa wakati wa viongozi wa Yanga kulichukua tabasamu la kila shabiki wa Yanga na kuligeuza mtaji kwao.

Ndicho kipindi ambacho mashabiki wengi wa Yanga wanafuraha sana kulingana na matokeo ya timu yao.

Na ndicho kipindi ambacho shabiki angependa kuendelea kuona timu yake ikiendelea kufanya vizuri.

Kipindi hiki viongozi wa Yanga walitakiwa kuwapa mashabiki wa Yanga jukumu la kuwalipa wachezaji.

Ndicho kipindi ambacho viongozi wa Yanga wangekuja na kampeni mahususi ambayo ingemfanya shabiki ajivunie kuwalipa mshahara wachezaji.

Wachezaji ambao kila wakikanyaga uwanjani wanawapa furaha. Kama kuna sehemu walikwama katika zoezi la mwanzo wasikate tamaa.

Wafikirie namna sahihi ya kujiuliza ni wapi walipojikwaa, viongozi wa Yanga hawatakiwi kuendelea kulala walipoangukia huku wakilaumu hali ambayo iliwasababisha wasifanikiwe kwa kiasi kikubwa kwenye kampeni hiyo.

Wanatakiwa wafikirie upya na waendelee walipoishia. Mengi yanasemwa kuhusiana na hali ya uchumi wa Yanga.

Wanatakiwa kutoka nje na kuja na kampeni ambayo shabiki ndiye atakayeibeba kwa kiasi kikubwa. Mfano, kwa sababu Yanga ni timu ya wananchi.

Kila mtu kwa muda mrefu amekuwa akijua Yanga ni timu ya “WANANCHI” basi viongozi wa Yanga wangeanzia hapa.

Waanzishe kampeni maalumu, kampeni ambayo itawakumbusha wana Yanga kuwa hii ni timu yao, siyo timu ya viongozi au Yusuph Manji.

Hivo jukumu la kuielea na kuitunza lipo mikononi mwao. Hivo basi wanatakiwa wachukue jukumu hili wao kama wao.

Kampeni hii iende na kauli mbiu ambayo itawafanya wana Yanga waone fahari kuhusika na kuwalipa wachezaji. Liwe jambo la kujivunia kwao.

Wakiona hii ni ngumu, basi waingie makubaliano ya kibiashara na kampuni yoyote. Mfano wakiingia makubaliano ya kiabishara na moja ya kampuni la kinywaji hasa hasa kwa muda huu sikukuu itakuwa na faida kubwa kwao.

Mfano, wakaingia makubaliano ya kibiashara na kampuni moja la vinywaji mfano kampuni la soda. Ambapo wataendesha shindano kubwa kupitia Yanga.

Mfano, nyuma ya visibo kuwe na herufi ambazo shabiki wanatakiwa azikusanye. Mfano, kizibo kinaweza kikawa na Herufi A kingine kikawa na herufi J.

Shabiki anatakiwa akusanye herufi za visibo ili kukamilisha jina la mchezani mfano Ajib na kunakuwepo na zawadi maalumu kwa mtu ambaye anakamilisha jina husika.

Kampuni hili la biashara litapata nafasi ya kutangazwa na timu ya Yanga, na kutoa nafasi kubwa kwa vinywaji vyake kununuliwa na asilimia fulani inaenda kwa Yanga.

Ndiyo maana jana wakati natazama mechi niliamini huu ndiyo wakati sahihi kwa viongozi wa Yanga kuwafanya mashabiki wao kushiriki moja kwa moja au kwa njia ya kibiashara ili wapate nafasi ya kupata kipato cha ziada kitakachoisaidia timu.

Sambaza....