Blog

Huu siyo muda sahihi wa kumuondoa Zahera

Sambaza kwa marafiki....

Matokeo ya jana yalikuwa magumu sana kwa mashabiki wa Yanga. Matokeo ambayo hawakuyategemea , matokeo ambayo yalikuja na ncha kali ya maumivu katikati ya kilindi cha mioyo yao. Hakutegemea hiki na wanaona kabisa hawakustahili haya matokeo.

Matumaini makubwa yalianzia kwenye midomo ya viongozi wao wakiongozwa na Antonio Nugaz. Hawa ndiyo Waliowapa matumaini ya uongo mashabiki wa Yanga. Hawa ndiyo waliodiriki kusema kuwa wanauwezo wa kuifunga Pyramid FC goli 3-0.

Waliingia uwanjani wakiwa na matumaini hayo. Waliwaamini viongozi wao kupitiliza na wakaweka picha kichwani mwao kuwa Yanga inauwezo mkubwa sana wa kuifunga Pyramid FC, timu ambayo katika mechi kumi na mbili (12) zilizopita imecheza mechi nne (4 ) za ugenini na kufungwa mechi moja tu na kushinda mechi tatu kati ya nne za ugenini.

Hawakutazama hili, hawakuwa na wazo kabisa kuwa Pyramid FC ni timu ambayo ilikuwa na wachezaji waliounganika vyema tofauti na timu yao ya Yanga na wao wakakubali kabisa kuwa Yanga ilikuwa na uwezo wa kuifunga Pyramid FC goli 3-0 pale CCM KIRUMBA.

Tangu awali nilichambua kuwa Yanga hawana uwezo kabisa wa kuifunga Pyramid FC hizo goli kwa sababu Pyramid FC ni timu bora kwa sasa kuzidi ilivyo timu ya wananchi Yanga. Yanga mpaka sasa hivi timu yao haijaunganika vizuri.

Yanga imekuwa timu ambayo inacheza vizuri sana kwenye nusu yao ya uwanja. Kwenye nusu yao ya uwanja imekuwa ikimiliki mpira ikiwa inajiamini sana lakini ikivuka mstari wa katikati kwenda kwenye nusu ya timu pinzani imekuwa ikicheza vibaya.

Wachezaji hubutua tu mpira kwenda mbele na hawawazi namna sahihi ya kutengeneza nafasi kuliko kubutua mipira. Viungo wao wamekuwa hawana uwezo wa kutengeneza nafasi kwa washambuliaji wao .

Hakuna muunganiko kati ya safu ya kiungo cha Yanga na safu ya ushambuliaji ya Yanga . Muunganiko huu unahitaji muda kutafutwa. Hapa ndipo hoja yangu ya kusema bado mapema kwa Mwinyi Zahera kufukuzwa Yanga inapoanzia.

Mwinyi Zahera amesajili wachezaji wapya wengi sana. Katikati kikosi chake cha sasa wachezaji wa zamani hawazidi wanne ambao huanza kikosi cha kwanza cha Mwinyi Zahera , wengine wote ni wachezaji wapya yani wachezaji sita wote ni wapya.

Kuwaunganisha wachezaji wapya kwa kipindi hiki na kuwafanya wacheze vizuri inahitaji muda sana. Ni ngumu kwa sasa hawa wachezaji wapya kuungana vyema na kuwaza kucheza vizuri katika hali ya ushindani ambao mashabiki wa Yanga wanataka.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.