Blog

Inashangaza kupuuzia na kubeza Senzo kwenda Yanga.

Sambaza....

Huenda zikawa ni taarifa mbaya zaidi na ngumu kustahimilika kwa pande zote mbili, lakini ndio soka lilivyo. Imekuwa ni muendelezo wa matukio yanayopasua vichwa na kushtua jamii ya michezo nchini hasa kuanzia Tarehe 8 ya mwezi agosti, baada ya kumshuhudia Mghana, Bernard Morrison akitua Simba, huku kukiwa na madai kuwa mchezaji huyo bado ana kandarasi na Yanga na kesi yake inasikilizwa ndani ya Shirikisho la Soka Nchini (TFF) yaani haijaisha.

Usajili wa Morrison Simba umeonekana kuwaumiza sana mashabiki wa Yanga na wengine kupata Mshtuko na hata wakijikuta hospitali kwa tiba zaidi. Tukio hilo hilo limewafanya mashabiki wengi wa Yanga kuwaona viongozi wao ni Waongo na wasio wajibika bila kujua soka ni mchezo wenye ladha tofauti kama hizo.

Baada ya Yanga kuhuzunika kwa siku nzima huku Simba wakifurahia ujio wa Morrison na kuona kama wamelamba dume, bila kujua hili lililotokea la Senzo Mbatha Mazingisa kumwaga wino Yanga.

Nikwambie Kitu?! Usajili ulio mkubwa kwa Yanga msimu huu ni wa Senzo Mbatha, hata kama wakifanikiwa kumleta Messi wa Barcelona na kumvisha kijani na njano. Hapa namaanisha, hadi sasa Yanga imelamba dume kumnasa Senzo kuliko hata Simba ilivyomnasa Morrison.
Acha nianzie hapa; tujiulize kwani Senzo amefanya nini pale Simba tangu atue Septemba 7, 2019 hadi leo? Kisha tuone kwanini Yanga imemsajili, na anatarajiwa kufanya vitu gani?. Bila shaka haya ndio maswali makuu ya kuyajibu kuliko hata lile swali maarufu la kwanini amejiuzulu Simba…

Baada ya kuachana na Platinum Stars ya Afrika ya Kusini msimu wa mwaka 2012/13 kama Mtendaji Mkuu wa Klabu, Senzo alitimkia Orlando Pirates ya huko huko Afrika Kusini kabla ya kujiunga na Simba ya Tanzania Septemba 7 akichukua nafasi ya Crescentius Magori kama Mtendaji mkuu wa Klabu (CEO) cheo ambacho kipo kwa mujibu wa katiba ya klabu.

Ujio wake Simba ulileta hamasa kubwa kwa klabu, lakini pia wengi walitegemea Simba kuendeshwa kisasa na kitaalamu zaidi (Professionalism), kitu ambacho Senzo amefanikiwa kwa kiwango chake.

Hadi sasa, Simba imepiga hatua kubwa katika mambo mbalimbali chini ya Senzo. Miongoni mwa mambo hayo ni kama ifuatavyo;

  1. Kuwabadili mashabiki kuwa rasilimali muhimu na chanzo cha kipato kwa klabu. Mwezi Agosti, Simba iliingia Mkataba na Benki ya Equity kusimamia Mradi wa kadi mpya kwa wanachama na Mashabiki ambazo zilijulikana kwa jina la “Simba Card”. Kadi hizi huwafanya Mashabiki na wanachama kulipia ada ya kila mwaka ya uanachama lakini pia kufanya miamala mbalimbali kwa matumizi ya kila siku. Lakini pia kadi hizi zinachangia ongezeko la mashabiki uwanjani kwani kupitia kadi hii, Shabiki anaweza kununua tiketi ya mechi na kupata punguzo la hadi 10%
    Haya yote yanamaanisha kuwa, Simba imeanza kukusanya ada ya uanachama kwa Mashabiki wake kisasa kabisa, hii ndio “professionalism”. Huenda wazo halikuwa la Senzo, lakini yeye alisimamia wazo na kuleta matokeo makubwa.
  2. Kusimamia ujenzi wa Mo Simba Arena. Miongoni mwa kazi za CEO wa klabu ni kusimamia miradi ya klabu. Ndoto za Simba kuwa na viwanja vyake vya mazoezi na kukwepa gharama kubwa za uendeshaji wa klabu zilianza zamani lakini ujio na uwepo wa Senzo umerahishia vitu vingi kikiwemo na hiki.
    Mwezi Desemba, 2019 Simba ilikamilisha ujenzi wa viwanja vya Mo Simba Arena, vya Nyasi bandia na za kupanda na kuipunguzia gharama kubwa klabu za kukodi viwanja kwa ajili ya mazoezi.
  3. Usajili. Tangu atue ndani ya Simba, Senzo amesimamia ujio wa Kocha mkuu, Sven Vandenbroeck na Msaidizi wake, Suleiman Matola, Kisha akamleta Luis Miquissone dirisha dogo la usajili, akamrudisha Shiza kichuya na kumpandisha Cyprian John Kipenye kutoka Simba B.
    Hadi ligi inamalizika, Simba ndio Bingwa wa ligi, Miquissone ameifungia Simba goli 4 na kutoa pasi 1 ya goli, lakini pia alifunga goli katika mechi ya fainali dhidi ya Namungo, ASFC na kuifanya Simba kutwaa kikombe cha tatu katika msimu mmoja. Lakini pia hata hivyo, hakuna anayebisha juu ya kiwango Mujarabu cha Luis Miquissone.
    Mbali na Miquissone, Kocha Sven amefanya kazi kubwa na anastahili pongezi, takwimu zinaonyesha kuwa Sven amesimamia Simba mechi 28 za ligi na kushinda mechi 17, sare 6 na kufungwa 3 pekee. Kwa upande wa magori, klabu imefunga magoli 59 na kufungwa 18.
    Hii inamaanisha kuwa kati ya alama 88 za Simba msimu huu, Sven amekusanya alama 57 pekee na kupoteza alama 27.
    Takwimu hizi ni dalili tosha kuwa Usajili wa Simba chini ya Senzo umekuwa na matunda makubwa na kuonekana kuwa ni wa kitaalamu zaidi.
  4. Tovuti ya klabu. UKiachana na tovuti hii ya (www.kandanda.co.tz), Simba ndio inayofutia kwa kuwa na tovuti yenye mvuto zaidi. Mei 23, mwaka huu, Klabu ya Simba ilizindua tovuti yake, tovuti ambayo hukusanya matukio muhimu ya klabu na taarifa mbalimbali zinazohusu wachezaji wa Simba na shughuli za kila siku za klabu.
    Kwa Afrika Mashariki na kati, Simba imeonekana kupiga hatua kubwa katika hili, kwani vilabu vingine bado havijagutuka juu ya hili kuwa litaongeza umaarufu wa klabu (Brand) na hata kuvutia wawekezaji.
    Hii ni kazi iliyotukuka ya Senzo kama CEO. Nasema ni kazi yake kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa msimamizi Mkuu wa shughuli na miradi yote klabu lakini pia Senzo ni mtaalamu wa masuala ya habari (media packaging) hivyo bila shaka katika hili alikuwa na ushawishi mkubwa.
  5. Wadhamini na timu ya wanawake. Hakuna klabu itakayoendelea duniani kama itakosa wadhamini aidha kwa kuwapoteza au kushindwa kuwaleta. Kaulimbiu ya Senzo akiwa Simba ni klabu kujitegemea yaani kuwa na uwezo wa kujiendesha bila kulimbikiza madeni.
    Chini yake aliimarisha mahusiano ya klabu na wadhamini waliopo kama SportPesa na kampuni ya A1 Products inayozalisha kinywaji cha Mo energy chini ya kampuni ya Mwekezaji wao Mohammed Enterprise Limited (MeTL) na kuhakikisha kampuni hiyo inaridhishwa na mahusiano na klabu na hata kuongeza Mkataba mpya kwa kila mwaka na kuipa klabu zaidi ya shilingi milioni 250 kwa mwaka.
    Lakini pia mafanikio ya timu ya wanawake ya Simba (Simba Queens) ni matokeo ya juhudi za uwekezaji wa klabu na usimamizi bora wa Senzo.
  6. Uweledi katika timu. Ukiachana na haya niliyoyataja, kubwa kuliko ni uongozi wake hasa katika kutatua masuala mbalimbali kwa kutumia uzoefu wake wa miaka 21 aliyokuwepo katika tasnia ya Soka katika masuala ya uongozi.

Chini ya Senzo ni vigumu sana kusikia wachezaji wamegoma. Bila shaka ulizisikia zile tetesi za kugoma kwa Clatus Chama kusafiri na timu mkoani Kagera, lakini pia bila shaka ulisikia ile skendo ya Paschal Wawa, Jonas Mkude na Erasto Nyoni… Matukio haya yote yalitatuliwa kwa njia ya amani na isiyoleta Mshtuko kwa mashabiki na mtikisiko kwa klabu.

Haya nilikutajia ni machache tu kati ya mengi yaliyo. Ukiyatazama kwa undani mambo hayo, Mashabiki wa Simba walikuwa na haki ya kuhuzunika. Wasiojua huenda wasielewe kwanini Senzo ni muhimu, lakini niwaambie tu kuwa Senzo ndio alikuwa muhimili wa aina ya mfumo wa Simba kiuendeshaji lakini pia ndio injini ya soka la Kisasa.
Acha tuhamie Yanga. Hapa inabidi tujiulize swali lingine la muhimu; alivyosajiliwa Yanga tutarajie vitu gani kutoka kwake? Kwanini Senzo ndiye aliyekosekana kwa muda mrefu ndani ya yanga? Je ni wakati sahihi kwa Yanga kuwa na CEO kama Senzo? Twende taratibu…

Morrison akisaini Simba Sc


Mei 31 mwaka huu, klabu ya yanga kwa kushirikiana na wadhamini wao, kampuni ya GSM waliingia katika mkataba wa miaka minne na kampuni ya La Liga ya kusimamia maendeleo ya mabadiliko ya kimfumo ya klabu. Mkataba huo unagharimu zaidi ya bilioni 2.6 za kitanzania.


Kazi kubwa ya La Liga katika mkataba huo ni kuhakikisha wanasaidia maendeleo ya soka la kisasa na kuiongezea thamani Yanga. La Liga watatoa wataalamu kwa ajili ya kusaidia mabadiliko ya kimfumo na mabadiliko katika klabu hiyo katika mlengo wa kisasa zaidi.
Katika sifa kubwa za Senzo ni kuliabudu soka la kisasa na linaloendeshwa kiweledi. Bila shaka Mabadiliko ya Yanga yana uhusiano mkubwa sana na ujio wa Senzo.
Uwepo wake ndani ya Yanga utasaidia pakubwa sana kutokana na uzoefu wake alkini pia uchu wake wa kubadili soka la Afrika kuwa la kisasa zaidi.
Hivyo ni dhahiri kuwa, jukumu la kwanza la Senzo Yanga ni kusaidia mabadiliko lakini pia Uzoefu wake katika uendeshaji wa soka utayafanya mabadiliko ya Yanga yawe na matokeo chanya zaidi hata ilivyotarajiwa.


Pili, Senzo ataisaidia katika usimamiaji wa shughuli za kila siku. Ndani ya yanga kilikosekana kitu ambacho Simba walikuwa nacho yaani klabu inakuwa na Mtendaji Mkuu ambaye ndiye huratibu vitu vyote kwa kushirikiana na nafasi zingine za kiuongozi. Yeye ndiye mtu wa kwanza kuyatazama mambo na kushawishi maamuzi yake.


Tatu ni upatikanaji wa Kocha na wachezaji bora kwa ajili ya mageuzi ya klabu. Yanga haitabadiliko kwenye mifumo ya kiundeshaji pekee lakini pia hata aina na viwango vya wachezaji na makocha watakaofaa kuitumikia Yanga itabadilika. Senzo anajua wapi kwa kuwapata na jinsi gani anaweza kuwanasa katika soko la kiushindani.


Nne, Senzo atakuwa ni daraja la klabu na Mwekezaji. Kama ilivyokuwa kwa Simba, Senzo wa Yanga ataimarisha mahusiano ya kimikataba yaliyopo kati ya Yanga na makampuni mbalimbli kama wadhamini ikiwemo kampuni ya GSM inayoifadhiri Yanga hadi sasa.
Senzo pia anajua jinsi ya kuwaleta wadhamini zaidi kwenye mifumo ya klabu na kuitengezea pesa klabu. Hii inamaanisha kuwa, kuna uwezekano Mkubwa kwa Yanga kuimarika kiuchumio baada ya ujio wa Senzo.


Tano, Senzo anaenda kusimamia bidhaa na mali za klabu na kukuza jina la klabu ndani nan je ya mipaka ya Tanzania. Kama alivyofanya kwa klabu zingine, pia naweza kufanya kwa Yanga kwa kukuza ‘brand’ ya timu na kupatisha thamani yake iliyopotea kwa misimu mitatu sasa. Hii itawafanya wachezaji kujisikia fahari kuichezea Yanga na kujituma zaidi ili kuipa mafanikio.


Sita, Kuibadilisha kauli ya “Yanga ya Wananchi” kuwa katika vitendo. Bila shaka nadhani hiki ndicho kitu cha awali zaidi kwa Senzo kukifanya akiwa na Yanga yaani kuwabadili mashabiki wa Yanga kuwa chanzo kikuu cha kipato kwa klabu kwa kubuni mifumo mizuri ya kulipia kadi za uanachama na ushabiki lakini pia kuichangia klabu kwa njia ya hisani.
Saba, Yanga inaenda kuundwa upya hasa mifumo ya kiutawala ndnai ya klabu na hata marekebisho ya katiba ili kuweka cheo cha CEO lakini pia mpangilio wa vyeo na majukumu yanayoendana na soka la kisasa na mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa klabu kama walivyoingia katika makubaliano na La Liga.

Viongozi wa Yanga na GSM katika hafla ya utiaji saini ya uhusiano na Laligaga


Nane, Kusimamia miradi mbalimbali ya klabu ikiwemo viwanja. Usishangae Msimu ujao kuwaona Yanga wanafanyia mazoezi katika viwanja vyao, kwa sababu tayari wameshampata mtu sahihi wa kusimamia kiweledi miradi yao na kuleta matokeo makubwa.


Senzo ni chachu ya maendeleo ya soka kwa Yanga na nchini kwa ujumla, japo najua Usajili wa Senzo una maana gani lakini nasema ujio wake ni dalili tosha kuwa GSM wamejitoa kuhakikisha klabu inapiga hatua kubwa na za haraka iwezekanavyo.
Wamejitosa kwa sababu uwepo wake hauhitaji njaa njaa bali unahiutaji timu iwe na fedha, kisha Bwana Mipango (Senzo) aweke na kisimamia matumizi mazuri ya fedha hizo.


Ujio wa Senzo pia unamaanisha, Yanga imeamua kupambana na kurudisha hadhi yake na kuingia katika mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa klabu tena kwa weledi Mkubwa.


Senzo karibu Yanga, tuondolee migogoro miongoni mwa viongozi na baina ya viongozi na wachezaji ambayo imedumu kwa muda mrefu. Senzo saidia masuala ya kimikataba baina ya klabu na Wachezaji maana hili nalo ni tatizo sugu.

Hakika Yanga Mpya ilimuhitaji Senzo, na Senzo aliihitaji Yanga ya mabadiliko. Hatimaye wanamabadiliko wamekutana, acha wafanye mabadiliko ya kweli katika soka la nchi hii. Sisi wadau tunashukuru kwa kinachoendelea maana inakuza soka letu kibiashara na hata kiuendeshaji. Kila la heri Senzo katika kazi yako mpya.

Sambaza....