Tahariri

Jinsi Kibegi cha Simba Kilivyoleta Maajabu.

Sambaza....

Wahenga husema “Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki”. Rafiki kweli hawezi kukuacha au kukunenea mabaya wakati wa dhiki, rafiki wa kweli ataambatana nawe hata wakati wa mateso kwa uaminifu. Habari ya kibegi kilichokua kimebeba jezi mpya ya simba kimenikumbisha usemi huu.

Katika tamasha la kibishara kati ya Smba na NMB wiki iliyopita, Simba kupitia mtengenezaji wake wa jezi “sandaland” walitangaza ujio wa jezi mpya za msimu wa mashindano 2023/24. Na walitambulisha kibegi ambacho jezi mpya zilikuwemo humo na kutangaza kuwa utambulisho utafanyika juu ya kilele cha mlima Kilimanjaro.

Shauku ya mashabiki wa Simba na hata wasio wa Simba ilikua kubwa kujua nini kipo ndani ukizingatia watani zao Yanga walishatambulisha jezi zao huku wakiwa wamelitawala soko la jezi nchini.

Kibegi cha Simba kikiwa safarini katika mlima Kilimanjaro..

Tarehe 20 mwezi huu safari kuanza kuupanda mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi Afrika, moja ya vilele saba virefu duniani. Safari ya kibegi kuelekea kilele cha Uhuru haikua rahisi kwani marafiki saba (wapanda milima) walikubali kufa kwa dhiki na mateso ili kuupanda mlima ili kuitimiza nia ya rafiki yao (Simba) kuzindua na kutambulisha jezi katika kilele cha mlima Kilimanjaro, mashujaa hao walikubali mateso, njaa na hata uchovu lakini hawakuwa tayari kuisaliti nia, hawakuwa tayari kurubuniwa na kuivujisha jezi.

Timu ya habari ya Simba hongera kwao, hawakuwa nyuma walihakikisha wanaufahamisha umma kila hatua na kila tukio kuelekea kileleni. Maudhui ya picha na video yaliwekwa katika mitandao ya kijamii ya klabu ili kuufahamisha umma.

Tarehe 21 jioni kibegi kilifanikiwa kufika juu ya kilele cha Uhuru mita elfu tano na zaidi toka usawa wa bahari na utambulisho wa jezi kufanyika.

Jezi mpya za Simba zilizozinduliwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro.

Huu sio utambulisho wa kawaida, mwingine atauliza Simba wamefaidikaje na utambulisho wa jezi mlimani? Kulikua na ulazima gani Simba kutambulisha jezi juu ya mlima Kilimanjaro? Kwahiyo Simba walishindwa kuaandaa hafla na kutambulisha jezi zao badala yake waende mlimani?

Kila shabiki na mpenzi wa soka anaweza kuhoji, wengine wanaweza pata majibu lakini wengine wanaweza jikuta katika migogoro juu ya maswali haya magumu lakini nikutoe shaka KANDANDA.CO.TZ iko hapa kukutoa shaka zote. Simba imefaidika pakubwa juu ya safari hii kibegi kuelekea kilele cha mlima kilimanjaro;

Kuongezeka kwa wafuasi na wafuatiliaji katika mitandao ya kijamii.
Ndani ya siku mbili hizi yaani juzi na jana Simba imekua namba moja katika mtandao wa Twitter ikiwa ndio ukurasa uliofuatiliwa na kutembelewa zaidi kuliko ukurasa mwingine wowote ule nchini.

Kibegi cha Simba kilifanikiwa kuwa top tranding katika mtandano wa Twitter.

Lakini pia Simba imepata wafuasi wapya, timu ya habari na mawasiliano ya Simba ilihakikisha maudhui yanayowekwa yanakidhi na kuikata kiu ya mashabiki, lakini pia kuwafahamisha na kuwajuza kila hatua ya safari ya kuelekea kileleni, picha zenye ubora ziliwekwa katika kurasa zao za kijamii na ikawafanya mashabiki wa simba ndani na nje ya nchi kuwa macho na kurasa za klabu, pengine sio mashabiki wa simba pekee lakini hata mashabiki wa timu pinzani walikuwa macho katika kurasa za kijamii za Simba.

▪Kuutangaza Utalii wa nchi.
Ukiachana na Royal Tour aliyoifanya rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan basi safari ya kibegi cha Simba kuelekea kilele cha mlima Kilimanjaro ndio hamasa kubwa ya utalii kuwahi kufanyika nchini.

Suala la kupanda mlima ni la kizalendo, Simba iko katika kampeni ya kuutangaza utalii wa nchi kwani katika mashindano ya kimataifa huvalia jezi zenye chapa kifuani yenye picha ya mlima Kilimanjaro sawia na maneno yasomekayo “VISIT TANZANIA” wakiwa na maana TEMBELEA TANZANIA.

Kikosi cha Simba Sc kikiwa kimevaa jezi zenye nembo ya Visit Tanzania kifuani.

Simba wameamua kuwa mfano kwa kuchukua hatua, lakini picha na mandhari za mlima Kilimanjaro zilizowekwa katika kurasa zao za kijamii zimewafikia watu wengi ulimwenguni hivyo wameuona uzuri wa mlima na vivutio vingine hivyo tutarajie mafuriko ya wapanda mlima huko mbeleni.

Kuwavutia wadhamini na wawekezaji kuwekeza Simba.
Imeonekana wazi kuwa Simba wanaweza kumpa mdhamini na muwekezaji nafasi kubwa kuonekana kutokana na utajili mkubwa wa wafuasi, lakini pia namna wanavyompa mshirika thamani, tutarajie wingi wa wawekezaji kwenda kuwekeza Simba wakiamini watapata nafasi kubwa ya kuonekana kwa walaji.

NB: UKITAKA KURUKA AGANA NA NYONGA.

Sambaza....