Blog

Kina Samatta wanatupa sababu mia za kupeleka wachezaji nje

Sambaza....

Habari za mechi ya Uganda na Tanzania zimeshaanza kufifia, wengi tumeshaanza kuangalia upande mwingine wa maisha.

Tumeshatazama sehemu nyingine ambayo inaweza kutufanya tusogeze siku, jua lichomoze na lizame tukiwa wenye furaha.

Furaha zetu zinatengenezwa na vitu vingi sana!, hakuna kitu kimoja pekee kinachotengeneza furaha ya watu wote kwa pamoja.

Kila mmoja wetu anakitu ambacho kinampa furaha, kama mimi ambavyo mpira wa miguu nimeufanya kuwa sehemu yangu ya furaha.

Huyu ndiye mpenzi wangu wa pili, ananipa furaha na kuna wakati ananiumiza lakini mwisho wa siku siwezi kumwacha kwa sababu ndipo furaha yangu ilipo.

Furaha yangu nikuona mpira wa Tanzania ukiendelea kwa kiwango kikubwa, furaha yangu ni kuona vilabu vyetu vikifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. Furaha yangu ni kuona timu ya taifa inafanya vizuri na kushiriki katika mashindano makubwa ya kimataifa.

Ni nani asiyependa kuona bendera ya Tanzania siku moja ikiwa inapeperushwa katika michuano ya kombe la dunia?

Michuano ambayo inamsisimko mkubwa na inafuatiliwa kwa ukubwa ?

Michuano ambayo macho ya watu wengi hutazama pamoja kwa muda wa mwezi mmoja?

Hapana shaka hakuna asiyetamani furaha ya namna hii. Furaha ambayo mpaka leo najiuliza inaweza kunikuta hai siku hii itakapofika ili niishuhudia timu yangu ya taifa?

Matamanio haya hujaa moyoni mwangu, na kujikuta najipa matuamini makubwa kuwa ipo siku nitashuhudia timu yangu ya Taifa ikishiriki kombe la dunia.

Matumaini ambayo hupotea ghafla kila nikianza kusikia sarakasi za mpira wetu.

Wakati ambao unamatumaini ya kuishuhudia timu yako ya taifa ikiwa kombe la dunia ndiyo wakati ambao unashuhudia madudu ya waamuzi kwenye ligi zetu.

Ndiyo wakati ambao unashuhudia migogoro isiyo na faida kwenye taasisi mbalimbali zilizopewa dhamana ya kuongoza mpira wetu.

Migogoro ambayo tunatumia muda mwingi kuihubiri kuliko kuhubiri maendeleo ya mpira.

Ndiyo wakati ambao ambao unashuhudia ligi yetu haina mdhamini na ina timu ishirini (20).

Ndiyo wakati ambao unashuhudia ubovu wa viwanja vinavyotumika kwa ajili ya ligi yetu.

Ndiyo wakati ambao nchi haina makocha ambao wanaushindani mkubwa, makocha ambao wangekuwa na msaada wa kuibua, kukuza vipaji vyetu.

Nchi haina vituo vya kuibua, kukuza na kulea vipaji vya watoto wadogo.

Hapa ndipo tumaini huwa dogo sana. Lakini mechi ya Uganda na Taifa stars ilikuja na somo mkubwa sana ambalo sisi tunatakiwa tusilichukulie kikawaida.

Kama tumeshindwa kutengeneza ligi imara, ligi yenye ushindani mkubwa, ligi ambayo tutaifanya bidhaa kubwa.

Bidhaa ambayo itakuwa inagombaniwa na wadhamini kila kukicha, wadhamini ambao wataweka pesa zao kwa ajili ya kuongeza ushindani katika ligi ili tupate timu imara ambazo zitatoa wachezaji imara kwenye timu ya taifa, basi tunatakiwa tupeleke wachezaji nje.

Kama tumeshindwa kujenga viwanja ambavyo ni vizuri, viwanja ambavyo vitakuwa na mazingira bora ya wachezaji wetu kucheza, Mara kumi tupeleke wachezaji wetu nje ya nchi.

Kama tumeshindwa kuishi bila migogoro isiyo na faida , migogoro ambayo haina tija katika maendeleo ya mpira wetu,ni bora tupeleke wachezaji nje.

Kama kweli tumeshindwa kutengeneza waamuzi bora ambao watakuwa wanatafasri vyema sheria za mpira ili tupate washindi halali, njia pekee iliyobaki ni kupeleka wachezaji kwenye ligi za nje.

Hii ndiyo njia pekee tuliyonayo katika mikono yetu, baada ya njia zingine kuonekana tumeshindwa kuzifuata.

Hii ndiyo njia pekee ambayo ina mwanga bora wa kutufikisha angalau kwenye nusu ya mafanikio ambayo tunayaota.

Uliwaona kina Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta, Hassan Kessy, Simon Msuva na Abdi Banda?

Ukomavu ulikuwa ndani ya miguu yao. Walijua namna ya kucheza na mechi za kimataifa.

Utulivu ulikuwa umejaa kwenye vichwa vyao, miguu yao ilikuwa na ukomavu ambao ulikuwa na dira nzuri.

Dira ambayo ilikuwa inatuonesha kuwa kama tukipata wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa hii ndiyo itakuwa njia ya mkato kwa timu yetu ya taifa kufanya vizuri.

Tumeshindwa kupitia njia ndefu, tusiwe na njia moja tu ambayo tunaamini itatufikisha. Kama njia ambazo tumekuwa tukizijaribu zimekuwa na mbigili nyingi tutumie hii ya mkato.

Tuwekeze muda wetu kutengeneza mawakala wengi na tutengeneze uhusiamo mzuri na vilabu vya nje ili tufanye biashara ambayo itakuwa na faida kwenye soka letu.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x