Sambaza....

Nilikuwa nafuatilia kwa ukaribu sana malumbano kati ya kaka yangu Shaffi Dauda na baadhi ya wana Simba waliokuwa wanaongozwa na Hadji Manara.

Chanzo cha malumbano kilianza pale ambapo Shaffi Dauda aliposema Simba katika kundi lao walikuwa “UNDER DOG”.

Kauli ambayo wana Simba wengi wakiongozwa na Hadji Manara ilionekana kama tusi. Waliona kama wamedharirishwa sana.

Yani kwa kifupi walivulishwa nguo mbele ya kadamnasi. Iliwauma sana, na mwisho wa siku hawakukubaliana na kauli hiyo kuwa wao ni ” UNDER DOG”.

Kujiamini kulianzia kwa mashabiki, walianza kujiamini sana kuwa wao ni daraja sawa na kina As Vita na Al Alhly. Hakuna chochote ambacho ungewaambia wakakuelewa kuhusu ukubwa wa hizi timu.

Unajua kipi kilizaliwa baada ya hapo?, timu nayo ilijiamini sana tena kupitiliza. Timu ilicheza kuwahakikishia watu kuwa wao siyo “UNDER DOG”.

Kiburi zaidi kilikuja baada ya wao kuwafunga Saura katika uwanja wa Taifa. Tena goli 3-0 kwa bila. Habari kubwa ilikuwa siyo kuifunga goli 3-0.

Habari kubwa ilikuwa Simba wamemfunga nani ?, Naam!, walikuwa wamemfunga Mwarabu.

Makusu akishangilia moja ya bao kwenye mechi (Sio ya Simba)

Tena goli 3-0 , tena kwa kuutawala mchezo kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya mwisho. Hapo ndipo kiburi kilipozidi kwa Simba.

Ungewaambia nini kuhusu ugumu wa mashindano haya wakati wao walianza kuyaona ni mashindano mepesi baada ya kuwafunga Waarabu?.

Watu ambao wanaonekana wana Hatimiliki ya michuano hii?, watu ambao kila msimu huwafanya vizuri?, hapana shaka Simba walijiona wamefika hili daraja.

Kocha mkuu wa Klabu ya Simba
Kocha mkuu wa Klabu ya Simba

Walijiona wanaweza sasa kuogopeka na timu nyingi kubwa barani Afrika. Wakajiamini sana kuanzia hapo. Neno ” UNDER DOG” likawa limefutika katika vichwa vyao.

Wakaamini wao wanaweza wakafanya vyema tena katika uwanja wowote ule. Ile hali ya kumheshimu mpinzani ikawa imetoweka kuanzia kwa mashabiki mpaka kwenye timu.

Mashabiki waliamini wana timu bora sana, na timu ya Simba ikaamini inaweza ikaonesha ubora wake katika uwanja wowote.

Ndiyo maana hata jana hawakuwaheshimu As Vita. Walisahau kabisa kuwa As Vita ni moja ya timu bora sana barani Afrika.

As Vita ambayo msimu jana walifika fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika. Hawakuwapa heshima yao Stahiki kabisa As Vita.

Ndiyo maana wakaenda kufunguka, kitu ambacho kilimalizika kwa Simba kufungwa magoli mengi sana.

Hapo chanzo kikuu ni kimoja tu , ni wao kukataa kuwa ni “UNDER DOGS”. Ninaamini kabisa kama Simba wangekubali kuwa wao ni ” UNDER DOGS” wangepata matokeo chanya.

Kwanini nasema hivo?, nasema hivo kwa sababu kina faida kubwa ya kuitwa “UNDER DOGS” kuliko hasara.

Kivipi?, Unapoingia uwanjani huku ukijua kuwa wewe ni “UNDER DOGS” lazima uwe na heshima kwa mpinzani.

Lazima ile hali ya kujiamini sana itoweke kwako. Unakuwa unacheza kwa tahadhari huku ukiwa unajiamini kwa kawaida.

Ipi faida ya kucheza kwa tahadhari huku unajiamini kawaida?, wachezaji hufanya maamuzi sahihi na yenye uhakika ndani ya uwanja.

Kila mpira wanaopata hufikiria namna ya kufanya maamuzi sahihi yenye manufaa kwa timu kwa ujumla ndani ya uwanja.

Mchezo unaofuata Simba itakutana na Al Ahly

Pia, hata timu inapojizuia, hujizuia vizuri kwa kuepuka makosa mengi binafsi. Makosa mengi binafsi ndani ya timu hupungua kwa sababu umakini huwa mwingi ndani ya timu.

Hali hii husababisha madhara gani kwa mpinzani?, unapokubali kuwa wewe ni “UNDER DOG” na mpinzani kuonekana kama ni mkubwa kwako basi mpinzani wako hujiamini sana.

Anapojiamini sana hujikuta anafanya maamuzi ambayo hayana utulivu ndani yake, na wakati mwingine hulazimika kufanya makosa ya kimaamuzi au kinidhamu.

Na kadri muda unavyozidi kwenda yeye “HU-PANIC” , anapokuwa amepanic ndipo hapo unaweza kumfunga vizuri kwa sababu anakuwa kwenye wakati ambao hawezi kufanya maamuzi sahihi na wewe unakuwa kwenye wakati ambayo unaweza kufanya kitu sahihi.

Sambaza....