Blog

Mbwana Samatta, Funga, Funga, Funga.

Nicasius N Agwanda (Kotinyotz)

Sambaza....

Dunia inakimbia kwa kasi kuzunguka jua, majira yanabadilika kwa kasi kutokana na hili, na haijakwama kuzunguka kwenye mhimili wake pia na usiku umekua haukeshi ili kupata mchana. Kila kitu kimebadilika kuanzia tenkolojia mpaka tabia. Mfano wa enzi zetu ni kama umepitwa na wakati kwa sababu enzi zimebebwa na mabadiliko haya makubwa, endelea kusoma makala hii iliyoandaliwa na Nicasius N Agwanda (Kotinyotz).

Nikiwa nimeketi na mzee wangu mmoja wa mtaani nikijaribu kumleta kwenye enzi mpya ambazo hazitaki za Instagram, iliibuka picha ya mchezaji wetu kipenzi Mbwana Samatta. Ilikuwa picha ambayo amepiga akiwa pembeni ya ndege ya klabu yake ya KRC Genk.

Mategemeo yangu ilikuwa aelezee safari hii walikuwa wanaelekea mji gani kwa ajili ya mchezo unaofuata lakini maneno yake yalibeba ndoto yake kubwa. Ndoto ambayo imehama majira na imebadili wakati, ndoto ambayo haikuwa sehemu ya wachezaji wa Tanzania kwa kipindi kirefu mpaka leo.

Samatta alikuwa anajipa changamoto mpya ya kuhakikisha kuwa ananunua ndege yake binafsi (private jet) na hata kama asipoweza basi walau kuwa alijaribu kufanya hili. Katika picha kubwa Mbwana Samatta alikuwa wala hazungumzii ndege kama ndege lakini alinifikirisha zaidi kwa namna msimu huu alivyofanya vyema.

Image result for mbwana samatta

Kwenye Medulla ya Mbwana Samatta na kwenye mboni zake anajaribu kutizama misimu miwili nyuma hali ilikuwaje. Kumbukumbu zinaibuka kuwa alikuwa anacheza na wachezaji kama Wilfred Ndidi pamoja Leon Bailey ambao wakati huohuo pengine ngoma za masikio yake zikawa zinarejea utani ambao walikuwa wakimwambia.

Akitizama kwenye akaunti zao za Instagram anaona mabandiko ya kutia hasira kuwa wanacheza dhidi ya Bayern Munich akiwa na Bayer04 Leverkusen kwa upande wa Leon Bailey wakati Ndidi akiwa kaketi katikati ya dimba la Leicester City mahala ambapo aliishi na kujijengea ufalme bwana Ng’olo Kante kabla ya kutua Chelsea, na sasa yeye ndo bosi wa eneo la kiungo.

Inawezekana kabisa kwenye ujumbe mfupi wa maneno akiwa anazungumza nao wanamtusi na kumwambia kwanini unaringia Benz ya hapo Ubelgiji wakati sisi tayari tunamiliki ndege binafsi pamoja na magari anayomiliki Jay Z na tumenunua nyumba walizowahi kuishi akina Ng’olo na Michael Ballack?

Akitizama kwa undani zaidi anaona kuwa hawa ni wachezaji ambao walimwacha katika nyumba ambayo wazazi wake wamezalisha vipaji kama Kevin De Bruyne na kuviweka katika kilele cha mafanikio kwa tafsiri nyingine ni kuwa anaishi kwenye nyumba yenye Uzima wa Milele kwenye soka kwa wenye juhudi.

Ndani ya akili zake nikawaza pengine Samatta ametizama kiwango chake cha msimu huu na kufunga mabao zaidi ya nane kwenye michezo sawa na mabao yake, kisha akatizama namna washabiki wanavyoimba nyimbo yenye jina lake akagundua kuwa ufalme alioupata TP Mazembe umefika KRC Genk na muda umewadia kwenda kujenga kwingine kwenye changamoto zaidi?

Nikakuna kichwa na kuwaza kwa umri wake wa miaka 25 kuelekea 26 si ndio umri sahihi kabisa kwa mshambuliaji kutua La Liga, Bundesliga na Premier League? Bahati nzuri ana miguu isiyotofautiana kwa kiwango kikubwa na Kelechi Ihenacho ambaye anapata mshahara wa kununua ndege binafsi anayoiota Samatta.

Jambo pekee ambalo linatakiwa kumweka Samatta katika imani aliyonayo ni kiwango alichokionyesha kiendelee kupaa, afunge kwenye ligi lakini afanye makubwa zaidi kwenye Europa League ambayo inafuatiliwa na kila mtu. Ukifunga Ulaya unatambulika kuliko kwenye ligi yako ya kawaida, hii huwa naiita Cristiano Ronaldo Theory, na imefanya kazi msimu huu dhidi ya Messi ambaye alifunga alivyojisikia kwenye La Liga na dhidi ya Salah ambaye alijipatia ufalme Liverpool.

Funga funga funga magoli ndio kitu pekee ambacho Samatta anatakiwa kukiwaza kwa sasa, akikosa kufunga ajifungie chumbani alie kwa uchungu. Anatakiwa kuishi kwenye mawazo ya Bill Shankly. Aliwahi kusema kwa wachezaji wake kuwa ukiwa kwenye “Penalty Box” kwa wapinzania na huna uhakika ufanye nini na mpira, wewe upasie nyavuni tutakuja kujadili machaguo yaliyokuwepo wewe kufanya baadae.

Mimi Kotinyo naamini Umefika muda ambao Samatta inabidi awe na hasira, hasira dhidi ya nyavu za wapinzani, inabidi awaze kwanini nisitwae kiatu cha mfungaji bora kwenye Europa League, inabidi afikirie kwanini nisiwe Awafu mwenye nguvu na nichane kila mdomo wa Simba utakaokuwa wazi.

Huu ndo uzito wa mawazo ninayojitahidi kuwaza kwenye alichokibandika Mbwana Samatta na ninajaribu kuamini kuwa ndio hasa mtihani aliojipatia ili kukimbizana na ndoto aliyojaribu kutushirikisha. Ndoto ambayo nyuma yake kunatakiwa kuwa na maneno yenye maana ya magoli tu, awe amewaza kwa Kiingereza, Kiswahili ama lugha ya kwao na pengine Kifaransa, magoli ndio yatakayonunua Private Jet.

Nikiwa bado nawaza kwa kina na wakati najaribu kuleta picha za Fareed Musa, Shaban Idd Chilunda na Simon Msuva na ndoto walizonazo nasikia kibao chepesi mgongoni, kumbe Yule mzee anahitaji kujua namna ya kubandika na yeye picha kama wanavyofanya wengine. Nilishasahau kazi iliyoniweka pale na kama ingekuwa yenye mshahara malipo yangu yasingetimia kwa kuwaza ndoto za wengine.

Nikiwa sijamtilia maanani bado mzee wangu huyu, nilijikuta namwambia Ndoto ya Private Jet ni Magoli. Nikaondoka zangu na kumuahidi nitamfundisha siku nyingine, acha nikasimulie wasomaji nilivyoota mchana nikiwa macho wazi. Ndoto ya Private Jet ni magoli. Funga Funga Funga.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x