Manara na Mo Dewji(Mwekezaji)
Blog

MO-DEWJI, hakuna mapinduzi yaliyofanyika bila kumwaga DAMU

Sambaza kwa marafiki....

Najua ni mfanyabiashara, tena mfanyabiashara mkubwa Afrika. Tajiri namba moja mwenye umri mdogo Afrika.

Hii inatosha kabisa kunipa picha kuwa anaamini katika hatua. Anaamini katika nyakati, nina imani kubwa kwenye hilo.

Nina imani kubwa kuwa Mohammed Dewji ana picha kubwa sana ya klabu ya Simba. Picha ambayo inawezekana wengine hatuna uwezo wa kuiona.

Ila yeye pekee ndiye mwenye uwezo mkubwa wa kuitazama kila uchwao. Maono ya klabu ya Simba ameyabeba yeye.

Yeye ndiye mwenye hisa kubwa ndani ya Simba. Yeye ndiye aliyeweka pesa nyingi sana kwenye klabu ya Simba kuliko mtu yeyote.

Pesa ambazo anategemea kuzirudisha na kupata faida kama ambavyo wafanyabiashara wengi wanavyokuwa wanawaza.

Hakuna Mfanyabiashara ambaye huwaza hasara katika akili yake. Akili za wafanyabiashara wengi huwaza faida tu.

Kila pesa yake inapotoka katika mfuko wake kitu cha kwanza kuwaza ni jinsi gani ambavyo pesa hiyo inaweza kurudi katika mfuko wake ikiwa na faida.

Ndipo hapo ninaporudi katika maneno yangu ya awali kuwa Wafanyabiashara wengi waliokomaa huamini katika hatua na nyakati.

Huamini kuwa mafanikio huja kwa hatua ndogo ndogo za kwenda mbele zinazokusanyika ili kuunda kitu kikubwa chenye mafanikio.

Wengi wao huwaza namna ambavyo wanaweza kupiga hatua za kwenda kwenye mafanikio. Ndiyo maana huwa wana vitu viwli ambavyo wengi wetu huwa hatuna.

MALENGO na MIPANGO. Hivi ni vitu viwili ambavyo ni tofauti sana kwenye biashara ya aina yoyote, na ni muhimu sana kufikia mafanikio.

Kufikia ndoto au maono ambayo mwanadamu huyapanga lazima awe na MALENGO na MIPANGO. Maneno mawili mazito.

Na ni maneno mawili ambayo unaweza ukachanganya kwa kuona kuwa ni kitu kimoja kumbe kuna utofauti mkubwa sana kwenye maneno haya.

Kocha wa Simba Sc, Aussems

Kwanini nasema hivi ?, Malengo ni yale ambayo mwanadamu hupanga kuyapata. Mfano, klabu ya Simba inaweza ikawa na malengo mbalimbali.

Kwa mfano inaweza ikawa na malengo ya kujenga uwanja, kufika robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika na kuchukua ubingwa wa ligi ya Tanzania.

Hayo ni malengo, malengo haya hutimia kipindi ambacho kuna kuwa na kitu kimoja kinachoitwa MIPANGO. Mipango ni sawa na barabara ambalo mtu hulichonga kufikia malengo husika.

MIPANGO ni njia za kufanikisha MALENGO yako. Kuna kitu kimoja hapa ambacho wengi huwa tunakisahau sana.

MALENGO siku zote huwa hayabadiliki. Yanabaki vile vile mpaka siku ambayo yatakapotimizwa. Wakati MIPANGO hubadilika siku zote.

Mfano , Simba inaweza ikawa na lengo la kujenga uwanja wa mpira wa miguu, na ili kufikia lengo hili ikawa imepanga kutumia fedha zote zinazopatikana getini siku ya mechi.

Lakini kwa bahati mbaya mapato ya mlangoni yakawa hafifu, hivo ili kutimiza lengo Simba inaweza ikaamua kutafuta mpango mwingine wa kujenga uwanja, tofauti na ule wa awali wa kutegemea viingilio.

Hapa kitu pekee ambacho kimebadilika ni MIPANGO lakiñi lengo limebaki pale pale ili liweze kufikiwa au kutimizwa.

Najua Lengo kubwa la Mohammed Dewji ni kuifanya Simba kuwa moja ya timu imara kwenye michuàno ya vilabu hapa Afrika.

Hili ni lengo mama, na ni lengo ambalo haliwezi kutimizwa ndani ya mwaka mmoja tu. Inahitajika kuamini hatua ili kufikia lengo hili.

Ndiyo maana huko juu nimeongea kitu kimoja kuhusu kuamini hatua (KU-TRUST PROCESS) ni kitu ambacho naamini Mohammed Dewji anakijua na anakiamini sana. Anaamini katika mipango ili kufikia hakua kubwa ya mafanikio. Ndiyo maana hata matokeo haya wanayoyapata kwenye ligi ya mabingwa.

Mapinduzi siku zote huja baada ya damu kumwagika. Matokeo mabovu wanayoyapata Simba kwa sasa ni hatua ya wao kufikia mapinduzi ya kweli ya mpira, naamini kuna funzo kubwa wanapata kupitia haya mashindano.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.