Sambaza....

Koti langu litakuwa nadhifu, sitoruhusu hali ya uchafu wa aina yoyote katika mwili wangu. Nitaonekana mzee- kijana. Mzee anayejipenda haswaa!.
Mzee ambaye muda mwingi nitakuwa natumia kuangalia mifugo ambayo nitakuwa nashirikiana na mke wangu kuitunza.
Mke ambaye amejaa upendo, mwenye kunijali, kuniheshimu na kunipenda kama ambavyo aliwahi kuapa mbele ya madhabahu takatifu ya mwenyezi Mungu.
Kwetu sisi Mungu ndiye ambaye tunamwamini kama kiongozi sahihi na tegemeo kubwa sana katika maisha yetu, mimi na mke wangu hatutaacha kumtumikia yeye katika siku zote za maisha yetu.
Tukiwa vijana tunamtumikia ipasavyo, tunamwabudu na kumsifu kwa miujiza mingi ambayo amekuwa akitutendea. Kila jua linapochomoza hutenda muujiza wa kutupa uhai bila gharama ya aina yoyote, hata jua linapozama kukaribisha giza hutuandalia ulinzi madhubuti kwetu sisi.
Messi
Hatulipii gharama zote hizo!, ni kwa ajili ya upendo wake. Haijalishi tunamkosea mara ngapi lakini rehema yake ni kubwa na neema zake zimetukuka.
Ndiyo maana akatupa watoto, watoto ambao watatupa wajukuu. Wajukuu ambao nitakaa nao mwaka 2050 kipindi ambacho nitakuwa mzee.
Nikiwa natumia muda mwingi sana kukaa nyumbani kuangalia mifugo ya familia pamoja na kukaa kwenye bustani huku nikiwa nimevaa nguo nadhifu , pembeni yangu meza yangu ikiwa imebeba jagi la maji.
Miguu yangu sitosita kuichoresha nne, huku macho yangu nikiyapa burudani ya maandishi kutoka katika moja ya gazeti la michezo kwa wakati huo.
Ndipo hapo mjukuu wangu atatumia nafasi ya kuongea na mimi nikiwa nimetulia peke yangu. Atatamani sana vingi kuvijua vya zamani kipindi ambacho mimi nilikuwa kijana.
Atatamani kujua hali ya maisha ya zamani na ya sasa. Atadadisi sana jinsi ambavyo tulivyokuwa tunaishi!, hali ya uchumi ilikuwaje na ikiwezekana anaweza kuuliza kwanini sikufanikiwa kuwa tajiri namba moja duniani!.
Nitajifanya kukohoa lakini ukweli utabaki pale pale kuwa swali hilo ni gumu na linahitaji uongo wa kumwiimarisha yeye ili aweze kupigana ili aweze kufika sehemu ambayo nilishindwa mimi.
Sitokuwa na nafasi ya kupiga nne tena, miguu yangu nitaiteremsha na gazeti langu nitalikunja na kuliweka juu ya meza  kujiandaa kujibu swali hilo.
Wakati najiandaa kujibu swali hilo , kwa wingi wa mambo waliyonayo watoto, mjukuu wangu atatamani kushika gazeti lile la michezo na kutaka kuanza kusoma, ndipo hapo anapokutana na mchezaji hatari duniani kwa kipindi hicho cha 2050.
Bila kujizuia ataanza kumwaga sifa nyingi sana, ataniaminisha kuwa anakipaji cha pekee na hakuna mchezaji kama yeye duniani,ndipo hapo na mimi nitaingia kwenye mazungumzo yake kwa kumwambia kuna mchezaji ambaye aliwahi kutokea katika sayari ya peke yake.
Sayari ambayo binadamu wengine huwa hawatokei!, huyu ni mchezaji wa aina nyingine na watofauti sana na wachezaji ambao waliwahi kutokea duniani.
Najua dunia inawakumbuka wengi sana , na kuwaheshimu wengi sana na kuwatazama kama vipaji halisi na bora kuwahi kutokea katika uso wa ardhi ya dunia hii lakini ukweli unabaki pale pale kuwa mchezaji huyu ni watofaufi na wakipekee na yuko katika dunia yake mwenyewe ambayo aliiumba na kuimirikisha mwenyewe.
La Masia ilikuwa sehemu yake ya kwanza kumtambulisha. Mwanzoni hawakuona kipaji kikubwa ndani ya miguu yake na umbo lake lilivyokuwa wengi walidhani ana matatizo ya kiafya.
Wakamdharau, lakini hawakumpuuzia. Waliendelea kuwa naye. Alikulia pale, akalelewa pale na mpaka akapandishwa kwenye timu ya wakubwa ya Barcelona.
Sehemu ambayo ameweka utukufu wake uliotukuka. Utukufu ambào hauna doa hata kidogo. Hata alipoanza kupewa nafasi na kochwa wa Barcelona kipindi hicho (Frank Rjikaard) alionesha mwanga kuwa anaweza kuwa mchezaji wa daraja la juu kama Diego Maradona.
Na watu walizidi kumfananisha na Diego Maradona , kuanzia miguu aliokuwa anatumia, ukimbiaji, ukokotaji wa mpira mpaka umbo.
Wengi wakawa wanaiona taswira ya Diego Maradona kwake, lakini muda ulitupa majibu tofauti na ambavyo tulikuwa tunafikiria awali.
Akiwa na jezi ya Barcelona amefanya mengi makubwa ambayo Diego Maradona hakuwahi kufanya akiwa na vilabu vyake.
Ameweka rekodi nyingi sana, rekodi ambazo zinaweka ugumu wa maisha kwa kizazi cha mpira kinachokuja kuja kuzivunja.
Rekodi ambazo zimemfanya kuwa mchezaji aliyechukua Ballon D’or mara tano katika maisha yake ya kucheza mpira.
Maisha ambayo mpaka sasa hajaruhusu kuporomoka kwa kiwango chake kwa muda wa miaka 10. Amepigania kipaji chake sana.
Amefanya vingi sana kwa kutumia mguu wake wa kushoto , mguu wenye sumaku kila ukinasa mpira, atatamani muda mwingi apewe yeye tu mpira ili ufurahie kumtazama.
Huyu ndiye Lionel Messi , Mchezaji wa kipekee kuwahi kutokea katika dunia hii. Kuna wengi watatajwa, utamsikia Juma akimtaja Pele, kesho John atamtaja Maradona na kesho kutwa Maduhu atamtaja Cristiano Ronaldo lakini ukweli ni kwamba Lionel Messi alitokea kwenye dunia ya kipekee ambayo binadamu mwingine hakuwahi kuumbwa na hapa duniani aliishi kwenye dunia ya kipekee na ya kwake peke yake.

Sambaza....