Blog

Nilimsamehe Samatta baada ya Dakika 90

Sambaza....

Kitambaa cha unahodha kilikuwa katika mkono wake wa kulia, kila jicho lilimtazama yeye kama kiongozi, kiongozi ambaye atakuwa mfano kwa wengine waliopo uwanjani. Kiongozi ambaye atakuwa wa kwanza kupigania nchi na wa mwisho kutakata tamaa. Kiongozi ambaye miguu yake haikutakiwa kuwa na neno “kukata tamaa”.

Miguu yake ilitakiwa ipigane sana tena kuzidi yeyote ambaye alikuwa amevaa jezi ya Taifa Stars!, kwanini ? , kwa sababu yeye ndiye alikuwa ni kioo cha timu. Siku zote kiongozi hutazamika kama kioo.

Jana Mbwana Ally Samatta, kila nyuso ilikuwa inamwangalia yeye, kila jicho lilikuwa linamtazama yeye na kila sikio lilikuwa linasubiri maajabu ambayo atayafanya yeye. Maajabu ambayo tunayatamani sana yatokee haraka!, maajabu ambayo tuna kiu nayo!, maajabu ambayo kila Mtanzania anatamani kuyaweka katika kumbukumbu zake ili aweze kusimulia.

Mimi jana nilitoka na cha kusimulia, tena nitasimulia sana mpaka siku ambayo nitaenda kaburini. Najua furaha yangu bado haijakamilika na ukamilifu wa furaha yangu utatimia siku ambayo tutaenda Cameron!.

Lakini hili halinizuii kusimulia kitu ambacho nilikiona jana, kitu hiki kitabaki kwenye kumbukumbu zangu sana!, kwanini nasema hivo?.

Tulifanya vibaya sana kwenye mechi ambayo tulitakiwa kufanya vizuri. Ikizingatia tulitoka kufanya vizuri dhidi ya Uganda kila jicho liliamini litashuhudia matokeo mazuri katika nchi ya Cape Verde.

Lakini ikawa tofauti na mategemeo yetu. Tuliambulia maumivu, maumivu ambayo yalitukatisha tamaa sana. Maumivu ambayo yalifanya chozi letu lijenge nyumba katika mashavu yetu.

Chozi halikuwa na sehemu ya kukaa, kila tulipokuwa tunajaribu kulisihi likae ndani ya macho halikutaka kutii wito letu, halikutamani kukaa tena kwenye macho yetu, nje ya macho yetu ndiyo ilikuwa sehemu sahihi kwa chozi kukaa.

Ilibidi iwe hivo ili kukamilisha neno “huzuni” ilikuwa ngumu kwa neno huzuni kukamilika bila kushuhudia chozi likiteremka taratibu kutoka kwenye mboni za macho yetu mpaka mashavuni.

Na kibaya zaidi hakukuwepo na mtu wa karibu kutusaidia kutupa leso kwa ajili ya kupangusa machozi yetu, ikawa nafasi kubwa kwa kilio chetu kuongezeka. Kilio ambacho kilikuwa na maumivu.

Maumivu ambayo yalisababishwa na kufungwa goli 3-0 dhidi ya Cape Verde nyumbani kwao Cape Verde. Tulitegemea matokeo mazuri zaidi ya haya kwa sababu tunatamani sana kufika pepo.

Tuliona hii ndiyo nafasi pekee kubwa kwetu sisi kufika pepo ilipo lakini matokeo yale yalikuja kama maumivu ya tindikali ndani ya kidonda kibichi, kilio kikubwa kilisikika kwetu!, kilio ambacho kilisababisha wengi wetu tukate tamaa.

Tulikata tamaa haswa!, hatukuwa na imani tena na timu yetu ya taifa kwa sababu tu ya matokeo ya Cape Verde!. Na wengine tulienda mbali mpaka kuhoji uwezo wa kocha Emmanuel Amunike!. Tulimvua nyota zote na tukasahau kuwa kabla ya kufika pepo lazima ufe!.

Hatukutaka kabisa kusikia neno “kifo” katika masikio yetu. Tuliamini tutafika pepo bila kufa. Lakini hii ilikuwa tofauti kabisa na kwa wachezaji wetu wa timu ya taifa.

Waliamini katika kifo ndiyo njia pekee ya kufika peponi, hawakuogopa kifo!, kila ambalo lilikuwa kwao kwa minajili ya kuwadhoofisha lilikuwa na maana kubwa sana kwao katika safari ya kuelekea peponi.

Ndiyo maana hata nyuso zao zilizungumza hili. Zilizungumza neno “kutokata tamaa”. Matokeo yaliyotokea katika ardhi ya Cape Verde hayakuwakatisha tamaa kabisa. Waliamini bado sana nafasi kubwa sana.

Ndiyo maana waliingia uwanjani wakiwa na nguvu za kupigania nchi yao. Lakini katikati ya mapigano kilitokea kitu ambacho kilikuwa na uwezo wa ” kuwabomoa” na “kuwajenga”.

Taifa Stars ilipata penalti. Imepata penalti katika kipindi ambacho inahitaji goli kwa aina yoyote ile ili ipate nguvu ya kupata matokeo mazuri. Bila shaka penalti ile ilikuwa na umuhimu mkubwa sana kwa wakati huo.

Lakini kwa bahati mbaya nahodha, kioo na kiongozi akakosa ile penalti. Kichwa changu nilikiinamisha chini, kama binadamu mwenye kinyongo nilijikuta namlaumu Mbwana Ally Samatta kwa kukosa ile penalti.

Nilijua kuna mawili yatatokea, moja ” timu ingekosa kabisa nguvu ya kupigana kwa sababu ya kukata tamaa baada ya Mbwana Ally Samatta kukosa ile penalti. Pili, nilitegemea morali ya timu ingeongezeka baada ya kukosa ile penalti kwa kuamini kuna nafasi nyingi wanaweza kuzipata.

Ndicho kitu kilichotokea, timu haikukata tamaa. Hata aliyekosa Penalti hakuonekana kuumizwa na kukatishwa tamaa. Alijua kukosa penalti ni sehemu ya mchezo tu. Aliwekeza nguvu zake kuipigania Taifa Stars.

Nguvu ambazo zilikuwa na matunda sana kwa sababu alihusika kwenye magoli yote mawili ambayo Taifa Stars waliyapata. Yani alitoa pasi ya mwisho kwa goli la kwanza lililofungwa na Simon Msuva na akafunga goli la pili.

Hapa ndipo nilipokumbuka kitu kimoja, kitu ambacho kilitokea baada ya yeye kukosa penalti. Kichwa changu nilikiinamisha na kuanza kumlaumu yeye. Nilihisi kama amelikosea sana Taifa lakini baada ya dakika 90 nilimsamehe Mbwana Ally Samatta kwa moyo mweupe kabisa na hapa ninaumia kutokuwepo kwake katika mechi inayofuata dhidi ya Lesotho.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x