Sambaza....

Masikini mtu kwao ugeni si kitu chema. Hakika ukiwa mgeni lazima uwe mpweke, upweke ambao hukufanya ushindwe kufanya mambo kwa uhuru hata yakiwa ni kawaida kufanyika.

Wenyeji wao hufurahia kuwapokea wageni kwani upo usemi unenao kuwa “Mgeni njoo mwenyeji apone”, usemi huu wa Kiafrika unamaanisha kuwa wageni huja na neema wageni huja na baraka hivyo mgeni akija basi mwenyeji atafaidika.

Katika soka la Bara la Afrika ni tofauti na Mabara mengine ya soka, Afrika ukiwa ugenini ni haswaa uko ugenini sababu mwenyeji huwa na nguvu kuliko mgeni. Soka la Afrika linasadikika kuwa gumu sana hususani kwa mechi za ugenini kwani kila kitu kinakuwa cha mwenyeji kuanzia uwanja mpaka mashabiki.

Wakati wa nyuma timu shiriki katika mashindano ya CAF kutoka Tanzania zilikuwa mchekea sana zinapokwenda ugenini kwani hazikuwa na muamko wa kuzitaka badala yake walitegemea sana kuzicheza vema mechi zao za nyumbani swala ambalo lilichagiza sana timu zetu kufanya vibaya kimataifa hususani michezo ya ugenini.

Lakini sasa mambo yamebadilika, soka la sasa limebadilika sana hususani kutokana na maendeleo ya sayansi na Teknolojia, urushwaji wa matangazo mubashara katika vituo vya habari na televisheni kumepunguza ufanyikaji wa vitendo viovu kwa wageni ambapo vilikuwa vinafanyika lakini havikuwa vikionekana.

Mashabiki wa Yanga wakiwa safarini kuelekea nchini Rwanda.

Ilikuwa ni ngumu sana kwa timu za Tanzania kupata mashabiki wawapo ugenini labda kwa wale Watanzania wachache waishio nje, lakini sasa mashabiki wameamua kusafiri na timu zao na kuwapa motisha tena wakiwa mbali na nyumbani.

Wawakilishi wa Tanzania katika msimu huu wa mashindano ya klabu bingwa Afrika ambao ni Simba na Yanga wamekuja na kampeni ya kusafiri na mashabiki wao hata katika mechi zao za ugenini.

Yanga wao watacheza na El Merrik ya Sudani pale Kigali Rwanda ambapo timu imeshawasili tayari nchini Rwanda huku mashabiki nao wakiwa tayari wameshafika tayari kutoa motisha katika mchezo huo utakaopigwa tarehe 15 mwezi huu.

Kikosi kizima cha Yanga, viongozi na benchi la ufundi walivyowasili nchini Rwanda.

Simba wao watamenyana na mabingwa wa Zambia wa msimu uliopita Power Dynamos, kikosi kimeshawasili Zambia toka jana, na mashabiki wao wameshafika tayari kwa kutoa hamasa kuelekea mchezo huo wa kesho ambao utachezwa katika uwanja wa Levi Mwanawasa.

Mashabiki ambao Simba wameondoka nao ni idadi kubwa kiasi cha kujaza mabasi zaidi ya matatu huku Yanga wakiondoka na idadi kubwa zaidi ya mashabiki ambao wamejaza zaidi ya mabasi sita madogo.

Uwepo wa mashabiki uwanjani utazifanya timu za Simba na Yanga kujihisi kama wapo nyumbani kwani motisha ambayo walikuwa wakiikosa katika nyakati za nyuma sasa wanazipata wakiwa ugenini mbali sana na nyumbani. Uwepo wa mashabiki wao utawanufaisha kama vile:

Mashabiki wa Mnyama Simba.

Kuchochea morali ya kupambana kwa timu.
Kelele za mashabiki jukwaani kutawafanya wachezaji kujiona wako na deni kwa mashabiki wao ambao wamesafiri mwendo mrefu kuja kuwapa motisha hivyo hilo litawafanya wachezaji kuongeza bidii za kuushinda mchezo kwa ajili ya mashabiki wao.

Uwepo wa mashabiki uwanjani kutawafanya wachezaji kuuona uzito wa jezi na kuihisi thamani ya nembo hivyo kuongeza morali ya kupambana.

Mshambuliaji wa Simba Kibu Denis akimuacha mlinzi wa Wydad Casablanca katika mchezo wa ugenini wa Ligi ya Mabingwa Afrika

Kupunguza presha kutoka kwa mashabiki wa timu mwenyeji.
Mbwa mkali kwao. Uwepo wa mashabiki kutawafanya wachezaji kutojihisi wanyonge kwa kusikia kelele za mashabiki wa timu wenyeji pekee badala yake Sauti na kelele kutoka kwa mashabiki wao nazo zitasikika hivyo kutawapunguzia wachezaji presha za nje ya uwanja.

Uwepo wa mashabiki wa timu zetu kutawanyima uhuru mkubwa mashabiki wenyeji kufanya fitina nyingi na kuwatoa wachezaji wageni mchezoni.

Simba na Yanga watamalizia nyumbani Dar es salaam michezo yao ya marudiano mwishoni mwa mwezi huu.

NB: KAMA HUWEZI KUMSHINDA UNGANA NAE.

Sambaza....