Henock Inonga Bacca
Mabingwa Afrika

Simba Kwenda Zambia na Mashabiki Wake, Hatma ya Inonga Hii Hapa!

Sambaza....

Wekundu wa Msimbazi Simba baada ya kumfahamu mpinzani wao katika Ligi ya mabingwa Afrika rasmi wamesema watakwenda na mashabiki wao nchini Zambia.

Simba watakutana na Power Dynamos ya Zambia katika mchezo wa hatua yakwanza ligi ya mabingwa Afrika ambapo wakifanikiwa kupata ushindi watafuzu hatua ya makundi.

 

Akizungumza mbele ya Waandishi wa habari msemaji wa klabu ya Simba Ahmed Ally alisema “Kuelekea mechi yetu dhidi ya Power Dynamos tunategemea kupeleka mashabiki kama ilivyo kawaida yetu tunapokuwa na mechi kwenye nchi za jirani tunatumia basi kupeleka mashabiki,” alisema na kuongeza;

“Bahati nzuri Zambia tumeshawahi kwenda huko. Utaratibu ambao umeandaliwa na Simba ni tutatoa basi hadi Ndola, Zambia na litarejea nchini baada ya mechi,” Ahmed Ally.

“Basi litaondoka nchini kwenda Zambia tarehe 13, Septemba saa 1 usiku na tutafika Ndola, Zambia tarehe 15, Septemba. Tarehe 17, Septemba baada ya mechi basi litaanza safari kurudi Tanzania. Kwa yeyote ambaye anataka kuungana nasi afike ofisini. Kwa kila mtu gharama ni Tsh. 200,000 na anatakiwa kuwa na pasi ya kusafiria na kadi ya manjano. Mwisho wa kupokea nauli ni tarehe 10, Septemba.”

Willy Esomba Onana akishangilia bao katika mchezo wa Simba Day dhidi ya Power Dynamos.

Ahmed pia amesema wapo katika mipango yakutafuta timu zakucheza nazo michezo ya kirafiki na pia amezungumzia hali ya wachezaji majeruhi Aubin Kramo na Henock Inonga.

“Katika kipindi chote cha kambi tunatarajia kucheza michezo miwili ya kirafiki. Tunasubiri uthibitisho wa timu ambazo tutacheza nazo, moja ya nje na nyingine ya ndani. Lengo letu kama Simba ni tupate mechi ngumu, mechi ya kiushindani.”

“Taarifa njema ni kwamba Aubin Kramo na Henock Inonga wamepona na wamerejea mazoezini na wenzao,” Ahmed Ally alimalizia.

Sambaza....