Sambaza....

Klabu ya Simba imewasili jana Uswatini ikitokea Afrika ya kusini, huku wakigawana vikosi viwili kwa kuwa ndege iliyokuwa iwafikishe Uswatini haikuwa na uwezo wa kubeba kikosi chote, badala yake kikosi cha kwanza kiliwasili saa saba mchana  na kingine kikiwasili saa tisa.

Akielezea juu ya hali ya hewa na wachezaji kwa ujumla,Mtendaji mkuu wa Simba, Crescentius Magori  amesema kuwa, timu iko vizuri wachezaji wana morari kubwa

“Hali ya hewa ni nzuri, uwanja ni mzuri ni wa nyasi za kawaida na kama ujuavyo timu yetu ikikutana na viwanja vya aina hii, basi mpira huwa ni mzuri”.

Kama zilivyo taratibu za shirikisho la soka Afrika (CAF) timu mwenyeji hufanya taratibu zote za kuipokea timu pinzani kuhakikisha wanapata hoteli, usafiri na uwanja wa kufanyia mazoezi, hii ni kama walivyofanya Simba kwa Mbabane Swallows katika mchezo wao wa kwanza lakini hali imekuwa tofauti kwa wenyeji wao Mbabane Swallows.

Magori amesema kuwa, Simba haikupokelewa na wenyeji wao, na hata hoteli wameandaa wao wenyewe kwa kuwa walituma timu ya maandalizi mapema ili kuweka mazingira sawa kwa timu yao kufikia na kukwepa figisufigisu vya wenyeji wao.

“ Hadi leo tunajipikia wenyewe, timu haikupokelewa na wenyeji, na hata ratiba ya uwanja ni ngumu, kwani leo asubuhi tunafanya mazoezi ya mwisho kwakuwa jioni kutakuwa na wenzetu  na hata tarehe 5 kutakuwa na mechi pia, hivyo ratiba ya matumizi ya uwanja inabana”

Simba itaingia dimbani kesho kupepetana na Mbabane ikiwa na mtaji wa magoli 4-1 na  ili iweze kufuzu kwenda hatua inayofuata ni lazima isiruhusu magoli zaidi ya mawili, na kama Mbabane watashinda goli 3-0 watafuzu kwa faida ya goli la ugenini.

Magori aliendelea kwa kusema  kuwa wachezaji wa Simba wanajitambua na wanaelewa umuhimu wa mechi hiyo

“Wachezaji wanajua hasa Simba inataka nini kwenye mchezo kama huu, wanajua kama wakifuzu hatua hii wataenda hatua inayofuata kabla ya kuifikia hatua ya makundi”

“Wachezaji wanasema watapambana ili wapate matokeo kwa maana wasifungwe magoli matatu, lakini hatutegemei kufungwa tunataka tupate ushindi hapa kwenye uwanja wa ugenini kwakuwa uwanja ni mzuri na tunaweza kucheza mpira wa uhakika”

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa hapa Dar es Salaam, Mbabane ilionekana kufanikiwa hadi dakika ya 82 kwani Simba ilikuwa mbele kwa goli 2-1, matokeo hayo yaliwafanya waanze kujilinda wakijua fika kuwa kama matokeo yataisha kwa 2-1 mechi ya marudiano ingekuwa rahisi kwao.

Hii ni sawa na misimu kadhaa ilipita, ambapo Mbabane Swallows waliwatoa Azam Fc katika mashindano ya shirikisho Afrika, Azam ilishinda goli 1-0 nyumbani lakini ugenini walipigwa  goli 3-0, hii inaonyesha kuwa Mbabane wanaweza kupindua meza kama tu Simba watakosa utulivu na  nidhamu ya mchezo katika dakika tisini za ugenini.

Sambaza....