Mabingwa Afrika

Simba yaingia katika rekodi 8 zilizowekwa klabu bingwa Afrika…

Sambaza....

Ligi ya mabingwa Afrika, imefika katika hatua ya  robo fainali. Hatua hii ni hatua ya mtoano, huku timu  8 zikitinga hatua hii.

 Timu zilizotinga ni Wydad Casablanca ya Morocco, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Esperance De Tunis ya Tunisia, Horoya  ya Guinea, TP Mazembe hya DRC Congo, CS Constantine ya Algeria, Al Ahly ya  Misri na Simba SC ya Tanzania.

Ligi ya msimu huu wa 2018/ 2019 ina tofauti kubwa na ligi ya Mabingwa Afrika 2017/2018.  Kandanda inakuletea takwimu na rekodi zilizowekwa hadi kufikia hatua hii ya mtoano ukilinganisha na  ligi ya msimu uliopita.

Rekodi nane zimewekwa, kuanzia kwa timu zenyewe washiriki, shirikisho la soka Afrika na aina ya matokeo kwa timu zote ukilinganisha na msimu uliopita.

  1. Timu shiriki

Ikiwa ni mashindano ya 55 kwa shirikisho la Afrika kuyasimamia nan i mashindano ya 23 tangu kubuniwa na kuitwa  ligi ya mabingwa Afrika. Msimu huu timu zilizoshiriki zilikuwa  timu 57 kutoka katika mashirikisho 46. Hii ni tofauti na mashindano ya 54 msimu wa 2017/2018 ambapo timu shiriki zilikuwa  59 kutoka mashirikisho 47 pekee.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa, msimu uliopita ulihusisha timu nyingi zaidi ukilinganisha na msimu huu. Kumekuwa na tofauti ya timu 2 na shirikisho moja.

                         2.Bingwa mtetezi kutinga robo fainali

Esperance De Tunis ya Tunisia ndio bingwa mtetezi wa mashindano haya. Naye amefanikiwa kuongoza kundi  B akiambatana na  Horoya  ya Guinea kufuzu hatua ya mtoano akijikusanyia alama  14 huku anayemfuata akiambulia alama 10 pekee.

Msimu wa 2017/18 bingwa mtetezi alitolewa katika hatua ya robo fainali,  licha ya kufuzu kwa  alama 12,  Wydad Casablanca aliga mashindano.  Je Esperance de Tunis kufuata nyayo za Wydad Casablanca?

  • 3. Idadi ya magoli yaliyofungwa.

Ligi hii imehesabu magoli  306 yakiingia kambani katika mechi  130 zilizochezwa.  Hii ni sawa na wastani wa magoli 2. 35 kwa kila mechi. Tofauti na msimu uliopita kwani magoli 351 yalifungwa katika mechi  146 zilizochezwa, sawa na wastani wa goli 2.4 kwa kila mechi

Hii ina maana kuwa msimu huu kumekuwa na ukame kidogo wa magoli kulinganisha na msimu uliopita. Lakini ligi bado, huenda magoli yakawa ni mengi zaidi hadi kuisha kwa ligi Juni 1.


                                                    4. Mfungaji Bora

Hadi sasa mfungaji bora wa ligi ya mabingwa ni Moataz Al- Mehdi wa Al-Nasr ya Libya.  Kwa sasa ana magoli 7 akifuatiwa na Meddie Kagere mwenye magoli 6, Clatus Chama akiwa na magoli 5 wote kutoka Msimbazi.

Lakini hadi kufikia hatua hii, timu ya mfungaji bora ( Al-Nasr ) ilikwisha towelewa katika raundi ya kwanza. Yaani Moataz amecheza michezo minne pekee, miwili ya raundi ya awali na miwili ya raundi ya kwanza.

Hii ni tofauti na msimu wa 2017/2018, kwani mfungaji bora alikuwa sehemu ya timu zilizofuzu kwenda hatua ya mtoano na hadi kubeba ubingwa. Anice Badri ndiye aliyekuwa mfungaji bora akipachika jumla ya mabao 8 katika timu yake ya Esperance De Tunis ya Tunisia.

5, Esperance De Tunis ndio timu pekee kushinda mechi  4.

Kati ya timu 8 zilizofuzu, hakuna timu hata  moja iliyopata ushindi katika michezo minne isipokuwa Esperance De Tunis  ya Tunisia. Esperance katika kundi B imejikusanyia jumlaya alama 14 ikishinda michezo yote mitatu ya nyumbani na mmoja wa ugenini dhidi ya FC Platinum na kupata sare mechi mbili dhidi ya Horoya na Orlando Pirates ugenini.

Timu zingine zote, zimeonekana kuwa vizuri nyumbani, huku zikipata ushindi nyumbani pekee, na zile zenye alama 10, zimepata sare moja ugenini.Mfano watimu hizi ni Al –Ahly, CS Constantine, Wydad Casablanca, Mamelodi Sundowns na Horoya.

6.Timu 5 kati ya 8 zilizotinga robo fainali zilitinga pia msimu uliopita.

Ukilinganisha na msimu huu, timu zilizotinga robo fainali msimu uliopita nyingi zimefuzu tena msimu huu.

Timu ambazo ni maingizo mapya ni tatu pekee ambazo ni Simba SC, CS Constantine na Mamelodi Sundowns, lakini zingine zote zina uzoefu wa msimu uliopita.

Timu tatu ambazo zilikuwepo msimu uliopita na msimu huu hazipo katika hatua hii ni Es- Setif, Etoile Du Sahel na 1 de Agosto.

  • 7.Simba ndio timu iliyofuzu kwa alama chache zaidi.

Katika makundi yote manne (A, B, C na D) timu iliyofuzu kwa alama kubwa zaidi ni Esperance De Tunis ikiwa na alama 14, ikifuatiwa na TP Mazembe yenye alama 11, kisha timu tano zote zikiwa na alama 10 kwa kila moja, timu hizo ni Wydad Casablanca, Mamelodi Sundowns, Horoya, CS Constantine na Al- Ahly.

Simba ndio timu pekee yenye alama 9. Imefanikiwa kufuzu  kwa alama chache zaidi ukilinganisha na alama za timu zote katika makundi manne. Kwa maana hiyo kundi D, ndilo kundi lenye wastani mbovu zaidi wa alama za kufuzu, kwani jumla wana alama 19 pekee ukilinganisha na makundi mengine yenye alama zaidi ya 20.

  • 8. Simba ndio timu pekee yenye tofauti ndogo zaidi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa kuangalia wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, Simba ndiyo inayoshika mkia katika jumla ya timu zote. Simba imefuzu hatua ya robo fainali ikiwa na tofauti ya mabao -7  yaani ikiwa na deni la goli 7.

Horoya ndio inayofuata ikiwa na deni la goli 1 (-1), CS Constantine na Wydad Casablanca zote zina tofauti ya goli 2, Mamelodi Sundown ikifuata ikiwa na tofauti ya goli 4, Esperance de Tunis goli 7,Al –Ahly goli 8 na TP Mazembe ndio timu inayoongoza kwa tofauti kubwa ya mabao, ina goli 9.

Je unadhani kupitia rekodi hizi, timu ipi ni tishio zaidi? Kwa rekodi hizi, timu ipi itakuwa ni  ahueni kwa Simba zikikutana hatua ya mtoano?

Je ni Esperance De Tunis, TP Mazembe au Wydad Casablanca?

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x