Simon Msuva
Blog

Simoni Msuva uko kimya sana rafiki yangu.

Sambaza....

Hello. Kheri ya mwaka mpya rafiki yangu. Nimekukumbuka sana , nimekumbuka vingi ambavyo tulikuwa tunazungumza.

Nimekumbuka ile kauli ambayo ulikuwa unapenda kuniambia kila nilipokuwa najisahau kufanya kitu cha kutimiza ndoto yangu.

Ulipenda kuniambia nisilale kwa sababu giza bado halijaingia. Na ulipenda kunisisitiza kuwa hata kama giza likiingia natakiwa kuukana usingizi.

Kuuruhusu usingizi ufunike macho ni dhambi kubwa sana. Usingizi usahaurisha kila kitu ambacho binadamu huwa anakitamani.

Siku zote mwenye ndoto ambayo haijakamilika huwa hapati usingizi. Utaanzaje kulala wakati akili yako inawaza vingi ambavyo hujavitimiza?

Ni ngumu sana, ndoto huumiza kichwa, na ndoto huwezi kuiita ndoto kama hujaamua kuifanyia kazi ipasavyo.

Haya ni baadhi ya maneno yenye hekima na busara kubwa ambayo ulikuwa unayatumia ipasavyo kuniambia mimi.

Siku zote ulikuwa unaumizwa sana na wewe kuendelea kuwa kariakoo. Sawa, inawezekana Kariakoo ni sehemu ambayo vijana wengi hutamani kufika.

Na hii ni kwa sababu tu kuna miamba miwili ya soka hapa nchini. Miamba ambayo ni maarufu na yenye ushawishi mkubwa.

Miamba inayopendwa sana, miamba ambayo imegawanya nchi yetu mara mbili. Upande wa kwanza ni Yanga na upande wa pili ni Simba.

Ndiyo maana wengi hutamani sana kufika hapo, na wengi wanapofanikiwa kufika hapo hupitiliza kulala moja kwa moja.

Tena kibaya zaidi hulala usingizi wa pono. Huwezi kuwaamsha hata kwa kelele gani ambazo utaamua kuzipiga.

Kuna uchwai pale, kuna pepo ambalo wengi huwa linawasahaulisha vijana wengi kila wakidanikiwa kukanyaga pale.

Pepo ambalo huwafanya wajione hapo ndipo walipofika. Na kuna wakati mwingine huwa hawaoni kama kuna klabu kubwa nyingine duniani kama Simba na Yanga.

Huwezi kuwaambia chochote kuhusu Manchester United, Arsenal, RealMadrid mbele ya Simba na Yanga. Kwao wao Simba na Yanga ni kubwa kuzidi mpira.

Hayo yote ni kwa sababu ya pepo la kujisahau. Pepo la kusahau ndoto zao. Wengi huwa na ndoto na za kucheza mpira wa kulipwa ulaya lakini wanapofika Kariakoo , wakiona mataa ya Kariakoo hudhani pale ndipo ulaya.

Hakuna anayekumbuka kuwa Kariakoo ni njia nzuri ya kwenda ulaya, ingawa ina vishawishi na vikwazo vingi.

Ni njia ambayo ni muhimu kuitumia ili kufikia lengo. Ubaya kila wakifika pale huwa wanabadili lengo, kitu ambacho ni dhambi kwa sababu kwenye maisha ni bora ubadili njia ya kufikia lengo lako kuliko kubadili lengo lako.

Pepo kusahaulisha huwa linafanya kazi kubwa sana. Lakini kwa bahati mbaya pepo hili halikufanikiwa kwa rafiki yangu Simon Msuva.

[poll id=”4″]

Alitumia muda mwingi sana kupigana nalo. Hakutaka kabisa ashindwe, hakutaka kubadili lengo lake la kwenda kucheza soka la kulipwa ulaya.

Tena kila alipokuwa anamuona Mbwana Samatta alizidisha nguvu ya maombi ta kushinda na pepo hilo. Alifunga sana.

Kila alipokuwa anafunga magoli ndipo alipokuwa analimaliza nguvu lile pepo. Mwisho wa siku rafiki yangu Simon Msuva aliondoka.

Kaskazini mwa Afrika yakawa makazi yake mapya. Makazi ambayo alipanga kuyatumia kama njia ya yeye kufikia alipopalenga.

Msimu wake tu wa kwanza akawa anafunga tu. Ndipo hapo moyo wangu ukawa unajawa na tabasamu kwa sababu rafiki yangu Simon Msuva anaendelea kuikimbilia ndoto yake.

Na kitu kizuri dunia ya sasa inawahitaji sana aina ya wachezaji kama yeye. Wachezaji ambao wanafunga magoli wakitokea pembeni.

Dunia imehama kutoka kwenye kuwategemea washambuliaji wa kati mpaka kuwategemea wachezaji wanaotokea pembeni.

Ndiko dunia ilipo, na ndipo rafiki yangu Simon Msuva alipo. Lakini hofu yangu ni ukimya wake. Kakaa kimya sana, hanitumia hata salamu siku hizi.

Sijui amenisahau?, sijui lile pepo alilolishinda Kariakoo limepanda ndege mpaka Afrika ya Kaskazini?

Popote alipo mwambie nimekumbuka sana na yeye ajaribu kunikumbuka kwa kunipa salamu. Salamu pekee ninayoitaka kutoka kwake ni kufunga tu magoli.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x