Uganda Cranes wakiwa mazoezini
Mataifa Afrika

Uganda wapiga kambi nchini Misri, kujiandaa kuivaa Taifa Stars.

Sambaza....

Timu ya Taifa ya Uganda jana jumatatu asubuhi wamefanya mazoezi ya kwanza wakiwa nchini Misri walipoweka kambi kujiandaa na mchezo wa kukalimisha ratiba kwenye kundi L la kufuzu kwenye fainali za mataifa Afrika (AFCON).

Uganda wakiwa chini ya kocha Sebastian Desabre wamefanya mazoezi mepesi ikiwa ni sehemu ya kutanua misuli kabla ya mazoezi magumu ambayo wanatarajia kuendelea nayo leo Jumanne.

Mpaka sasa wachezaji wanaocheza nje ya Uganda wameendelea kuripoti kambini nchini Misri akiwemo Edris Lubega, Joseph Ochaya, Khalid Aucho na mlinda mlango Salim Jamal na nahodha Denis Onyango.

Wachezaji kumi ndio walioanzia safari nchini Uganda kabla ya kuungana na wale wanaocheza nchini Tanzania Murushid Juuko, Emmanuel Okwi na Nico Wakiro Wadada mjini Addis Ababa Ethiopia kuelekea kambini.

Kocha msaidizi wa Uganda hapo jana amesema kwamba wanaamini kabisa watawafunga Tanzania na kuendeleza rekodi nzuri wanapokutana nao.

“Hatupo kwenye shinikizo lolote, wao Tanzania ndio timu ambayo ipo kwenye shikizo kubwa, hatupambani kwa lolote zaidi ya kuongeza alama kwenye akaunti yetu,” amesema.

Mpaka asubuhi hii wachezaji wengine muhimu walikuwa wanatazamiwa kuwasili akiwemo Milton Karisa, Robert Ondongkara, Moses Opondo, Farouk Miya na Shaban Mohammad ambapo wataendelea na mazoezi leo kabla ya kesho kucheza mchezo wa kirafiki na timu mtaani hapo Misri.

Tanzania inayohitaji alama tatu kwenye mchezo huo ili kujitengenezea nafasi ya kufuzu kwenye fainali za mataifa Afrika kwa mara ya kwanza toka 1979 watawakaribisha Uganda kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.