Blog

Ujio wa Manji ulikuwa Sinema ya Yanga?

Sambaza....

Asubuhi ya Agosti 17 ilikuwa ndiyo siku ambayo tulikuwa tunahesabu masaa kwenda uwanja wa Taifa kushuhudia mechi kati ya Yanga na USM Alger’s.

Na ndiyo siku ambayo wana Yanga wengi walipatwa na mshangao wenye maswali mengi, maswali ambayo mpaka sasa inawezekana hakuna mwenye majibu sahihi.

Ni siku ambayo kurasa za mitandao ya kijamii ya Yanga ilikuwa imepambwa na Tangazo ambalo mpaka sasa halina majibu sahihi.

Tangazo ambalo lilikuwa linaonesha mwenyekiti wa klabu ya Yanga atakuwepo ndani ya uwanja wa Taifa kushuhudia mechi kati ya Yanga na USM Alger’s.

Wengi walimkumbuka sana, na walikuwa na hamu naye sana na shauku kubwa ilibaki kumuona akiwa katika uwanja wa Taifa.

Wengi tulijua ni changa la macho ambalo tulikuwa tunachezewa na viongozi wa Yanga lakini mwisho wa siku tulimshuhudia Yusuph Manji akiwa kwa mchina.

Tena akiwa na siha, na tabasamu lilikuwa limependezesha uso wake , hii yote ilionesha alikuwa ameikumbuka Yanga kwa kifupi wote wawili walikuwa wamekumbukana (Yanga na Yusuph Manji).

Maswahiba wawili ambao herufi za mwanzo za majina yao zinafanana, na ndiyo maswahiba wawili ambao wanapenda sana, ni ngumu kuwaachanisha hawa watu kwa sababu Yanga inampenda Yusuph Manji na Yusuph Manji anaipenda Yanga.

Wanapendana na wanahitajiana sana, siku ile ya mechi ilijidhihirisha. Yanga ilimwihitaji sana Yusuph Manji kushinda ile mechi , ndicho kitu kilichofanyika.

Yanga alishinda tena mbele ya waarabu, timu ngumu katika michuano hii. Kwa mara ya kwanza matumaini yalianza kuwajaa mashabiki wa Yanga.

Waliiona timu mpya, timu yenye hali ya juu na timu iliyokuwa inapigana muda mwingi mwa mchezo. Waliiona Yanga ambayo ilikuwa Yanga imara na tishio ndani ya misimu mitatu iliyopita.

Kwa kifupi Yanga iliyokuwa imepotea kwa kipindi kifupi ilionekana siku ile tena mbele ya Yusuph Manji.

Ulikuwa ujio rasmi wa Yusuph Manji? Hili ndilo lilikuwa swali gumu ambalo mpaka sasa halijapatiwa majibu.

Inawezekana ilikuwa sinema ambayo wengi wetu tulichezewa? , hatuwezi kujua kwenye hilo lakini kikubwa ambacho kinatakiwa kuanishwa kuwa Yusuph Manji amerudi katika majukumu yake ya Uenyekiti wa klabu ya Yanga?

Ni muda mrefu nafasi hii imekuwa na mkanganyiko imekuwa kama haina mtu, na inahitajika kupata mtu ambaye atashika nafasi hiyo ili timu iwe na mwenyekiti.

Kuonekana kwa Yusuph Manji katika uwanja wa Taifa kama mwenyekiti wa Yanga ilikuwa ni kutuaminisha Mwenyekiti amerudi kwenye majukumu yake ya kawaida.

Lakini kutoona majukumu anayotimiza kama mwenyekiti linabaki ni swali ambalo halina majibu kwa wengi.

Na swali hili linahitaji jibu lenye uwazi kuliko kuficha kitu ambacho kina manufaa kwa klabu ya Yanga.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x