Blog

Wakati Samatta anaenda England, Kichuya anarudi Mchangani

Sambaza....

Maisha ndiyo yalivyo , hayakupi unachokitamani ila yanakupa unachopigania . Hapa ndipo lilipo daraja kubwa linalowatenganisha wachezaji wengi wa Tanzania na Mbwana Samatta.

Mbwana Samatta amekuwa akitumika kama kioo cha wengi , kila mchezaji anatamani sana kufika alipo Mbwana Samatta. Kila mchezaji anaonekana ana wivu na mafanikio ya Mbwana Samatta.

Ni kama ilivyo kwenye muziki wetu wasanii wengi kutamani kufika alipo Diamond Platnumz ndivo ilivyo kwenye mpira wetu wanasoka wengi kutamani kufika alipo Mbwana Samatta.

Kwenye maisha kutamani pekee hakutoshi , moyo wako kuwa na tamaa ya kufika sehemu fulani hakutoshi kabisa. Kuna kitu cha ziada ambacho kinatakiwa ili kufikia matamanio yako.

Kupigania matamanio yako kwa juhudi kubwa ndiyo kitu pekee ambacho mwanadamu anatakiwa kuwa nacho wakati anapigania ndoto zake.

Kutamani pekee kuwa unatamani kufika sehemu fulani hakutoshi. Mdomo hauwezi kukufikisha sehemu ambayo unaitamani. Miguu ndiyo silaha tosha ya kukufikisha hiyo sehemu unayoitamani.

Miguu yenye juhudi , miguu yenye tamaa ya kupiga hatua za uhakika za kwenda mbele , hata kama ni hatua fupi lakini ziwe hatua za uhakika zinazoonekana kuwa ni za mbele.

Mbwana Samatta akiongoza kupasha misuli kabla ya mpambano

Kurudi nyuma kuna haribu vitu vingi sana ambavyo ni vya msingi. Taifa letu lilitamani kumuona Shaban Chilunda akifika sehemu ambayo ni kubwa. Matamanio ambayo yalitokana na sisi kuona kipaji chake.

Tuliona kipaji chake ni kikubwa hakifai kuwa hapa , hata yeye moyo wake uliona hafai kuchezea hapa , muda wake ulikuwa umefika kwenda sehemu ambayo Mbwana Samatta yupo.

Hispania pakawa sehemu yake ya kwenda lakini ghafla tukamuona kwenye ligi yetu. Hivi ndivo ilivyokuwa kwa Shiza Ramadhan Kichuya. Kipaji kikubwa , kipaji kilichobeba guu la kushoto lenye hatari.

 

Guu ambalo linaweza kukanyaga nyasi zozote zile na likafanya maajabu. Guu hili lilienda Misri , tukaona ni mwanzo mzuri wa hili guu kusogea kwenda mbele , lakini cha kushangaza guu hili limerudi tena kwetu kwenye viwanja vibovu ambavyo vina hadhi ya mchangani.

Sambaza....