Blog

Wanayanga wanalazimisha kuona wakiwa wamefumba MACHO!

Sambaza....

Hakuna mtaji mkubwa duniani kama maarifa, maarifa ndiyo mtaji mkubwa na wa kwanza kwenye dunia hii ambayo taarifa ndiyo mfalme wa mafanikio yote. Huwezi kupata mafanikio makubwa kwenye kitu unachokifanya bila kuwa na “taarifa” na huwezi kufikiria kupata taarifa kama huna “maarifa”.

Ni vitu viwili muhimu sana ambavyo vinategemeana sana tena kwa kiasi kikubwa kujenga daraja la kuyafikia mafanikio yako ambayo unayaota!. Unaweza ukawa na “wazo”, lakini ubora wa wazo hutokana na sehemu ambayo wazo hilo linatoka. Ni ngumu kupata wazo bora kwenye kichwa kisicho na maarifa.

Jack Ma

Na huwezi ukalifanya wazo lako lisimame ipasavyo tena imara bila kuwa na taarifa sahihi ya hicho kitu ulichokiwaza. Umewaza kuwa na biashara ya mihogo?, ukawaza jinsi ya kuifanya ili uwavutie wateja?, lakini lazima upate taarifa ya soko la mihogo.

Ndipo hapo unapoona vitu hivi vinaendana sana kwenye dunia hii ya mapinduzi makubwa ya kibiashara. Dunia ambayo kila kitu unachokifanya unatakiwa ukifanye katika jicho la kibiashara.

Ndiyo dunia ambayo tunaishi na kupumua hewa moja ambayo Jack Ma anaivuta na kupumua. Lakini kinachokuja kututofautisha ni jinsi ambavyo tunavyofikiria. Sisi tunafikiria kupata mlo tu , yeye anafikiria kuongeza kuni nyingi za kupikia huo mlo. Na ndiyo dunia ambayo ilimfanya yeye afikirie kukifanyia kazi kitu ambacho hakuwahi kukisomea.

Hakusomea kabisa Computer, na hakuwa anajua kuitumia kabisa Computer lakini alikuwa na maarifa ya kutengeneza kitu ambacho kitawawezesha wafanyabiashara kuuza bidhaa zao dunia nzima.

Akaja na Alibaba. Maarifa yake aliyachanganya na taarifa sahihi ambazo zilimwezesha afanikiwe kwenye biashara yake. Leo hii tajiri mkubwa sana duniani.

Kila jicho linamtazama kama mfano sahihi wa kuiga ili kufikia kilele cha mafanikio. Tunatamani sana kufikia mafanikio yalipo lakini hatujawahi hata siku moja kudhubutu kutembea kuelekea kwenye hayo mafanikio.

Kila tukijaribu kwenda tunatumia akili za jana, akili ambazo mpaka sasa zimetufanya tuendelee kuwepo hapa. Akili ambazo zimetufanya tupende kushikiria vibovu. Akili ambazo zimetufanya tuishi kwenye giza, tumelizoea sana hili giza na tumelipenda sana hili giza kiasi kwamba hatutaki hata kutoka kwenye hili.

Hata akitokea mtu akiwa na mwanga wa kutuwezesha kuona, sisi ndiyo huwa wa kwanza kumshambulia kwa kiasi kikubwa. Hatutaki mwanga lakini tunatamani mafanikio makubwa!. Tuko kwenye njia ambayo inagiza, njia ambayo huwezi kuona vizuri unapoelekea kwenye kilele cha mafanikio. Lakini tunatamani kutembea kwenye hali hiyo hiyo!, bila kujali hatari ambazo tutazikuta kwenye hilo giza!.

Tunatamani kutembea kwenye giza hilo hilo bila kujua njia sahihi ya kuelekea palipo kilele cha mafanikio!, ndiyo maana ni jadi yetu kuwashambulia wale ambao hujitolea kuleta mwangaza kwenye njia zetu. Ni ngumu sana kuelewa ni kipi ambacho tunakita. Inachosha sana , hasa hasa ukifikiria sana. Tunatamani kufikia mafanikio makubwa lakini hatuna “maarifa na taarifa” sahihi ya kutufikisha huko!.

Ni dunia hii hii ambayo kila kitu kinatakiwa kufanyika kwa njia ya kibiashara ndiyo ambayo imebeba watu ambao wanajua kupinga vitu bila maarifa ya kuyapa kipaumbele katika akili zao.

Hawana maarifa kabisa!, wanajiona wana maarifa ndiyo maana kila anayekuja kuwapa taarifa sahihi humpuuzia. Ndiyo maana ni jambo la kawaida sana kwao wao kuanzisha migogoro ya ajabu kila jambo zuri linapotaka kufanyika.

Wanachama wa Yanga

Inasikitisha sana kuona mpaka sasa hivi wanachama wa klabu ya Yanga baadhi yao hawaoni kabisa umuhimu wa kuwa na uchaguzi kipindi hiki ambacho nusu ya viongozi wake wamejiudhulu. Wanaamini pasipostahili kuaminika. Wanaamini vitu ambavyo ni vigumu kwa mtu mwenye maarifa kuanza kuvifikiria. Hatuna kabisa maarifa na taarifa sahihi kwenye tasnia hii ya mpira.

Ndiyo maana tunapenda sana kuishi maisha duni. Maisha ambayo hayana nafuu kubwa kwetu sisi. Maisha ambayo yanatufanya kuwa omba omba kila siku. Hatutaki kabisa maisha ya kujitegemea kwa sababu tumekosa maarifa ya sisi kujitegemea na hatuna taarifa sahihi za umuhimu wa kujitegemea, ndiyo maana tunajifanya tunaona kila kitu ilihali tumefumba macho tena kwenye giza totoro.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x