Sambaza....

Kocha wa timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ Sebastien Migne amewaengua ndugu wawili Victor Wanyama na McDonald Mariga katika majina ya mwisho ya kikosi cha timu kuelekea katika mchezo wao wa kundi F kuwania kufuzu kwa michuano ya Afrika dhidi ya Ghana kwa sababu mbalimbali.

Migne amemuondoa Wanyama kutokana na kuwa na majeraha ya goti wakati Mariga ameondolewa kikosini kutokana na kushindwa kuripoti kwenye kambi ya kujiandaa na mchezo huo bila kuweka wazi sababu za msingi.

Wanyama ambaye anaichezea Tottenham ya England alikuwepo kwenye benchi Jumapili wakati timu yake ilipochezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Watford huku Mariga anayekipiga Real Ovideo ya ligo daraja la kwanza Uhispania hakucheza katika mchezo wa ligi hiyo Jumapili dhidi ya Cadiz.

Victor Wanyama

Hofu na Mashaka imetawala Kenya kutokana na kuwakosa wachezaji hao hasa Wanyama huku wakiwa wanakabiliwa na mchezo mkali dhidi ya Ghana ambao wapo kambini Nchini Ethiopia toka Jumatatu kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa katika uwanja wa Kasarani siku ya Jumamosi.

Hata hivyo kocha Migne amewatoa hofu wakenya na kusema kuwa washapata mbadala wa Wanyama kwani hawawezi kumpotezea malengo yake kwa kumtumia ikiwa bado ana maumivu ya goti.

Mariga

“Hatuwezi kumtumia Wanyama, hatuwezi kumuharibia maisha yake kwa sababu ya mchezo huu, tunajua ni mchezaji mzuri na ni muhimu kwa timu lakini hatuwezi kujaribu kumtumia, tutatafuta mchezaji mwingine, tutatafuta namna nyingine,” Migne amesema baada ya kuwatangaza wachezaji 24 kwa ajili ya mchezo huo.

Wachezaji walioitwa kikosini:

Makipa: Patrick Matasi, Farouk Shikalo, Ian Otieno.

Walinzi: Philemon Otieno, Jockins Atudo, Dennis Odhiambo, Joash Onyango, Benard Ochieng, Abud Omar, David Ochieng, Erick “Marcelo”  Ouma, Joseph Okumu, Musa Mohammed, David Owino.

Viungo: Francis Kahata, Abdallah Hassan, Anthony Akumu, Eric Johanna, Ismail Gonzalez, Johanna Omollo.

Washambuliaji: Piston Mutamba, Jesse Were, Michael Olunga, Ovella Ochieng.

Sambaza....