Sambaza....

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya wanawake nchini (WPL) JKT Queens, kesho wataanza kutupa karata yao ya kutetea ubingwa wao katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo dhidi ya Evergreen ya Jijini Dar es Salaam, JKT wakiwa wageni katika dimba la Karume.

Akizungumzia maandalizi ya timu ya JKT Queens, Afisa Habari Koplo Elizabeth Buliba, amesema maandalizi yako salama na wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatetea ubingwa na wamewaahidi mashabiki wa timu hiyo kupokea zawadi ya ubingwa huo kwa mara nyingine.

Aidha amesema uwepo wa timu za Yanga Princess na Simba Queens utaleta changamoto kubwa katika ligi hiyo huku akiweka wazi kuwa Simba Queen na Yanga Princes ni timu za kawaida kwao, pamoja na kuwaomba wadau kushirikiana kwa pamoja katika kupeleka mbele soka la wanawake kwani wanafanya vizuri hata kwenye timu ya taifa.

“Kesho tunakuja na zawadi ya mwaka mpya, zawadi ambayo ni pointi tatu muhimu, najua ligi ya mwaka huu itakuwa na ushindani, timu zote zimejipanga na zipo vizuri hata ukiangalia ligi hii imezidi kukua, lakini kwa mashabiki wetu watarajie radha tofauti, ule mpira wa kitanzania,” Buliba amesema.

JKT Queens wataingia katika mchezo huo wakiwa ni Mabingwa wa msimu uliopita wakiwapokonya Ubingwa Mlandizi Queens waliombulia nafasi ya nne na Kuwaacha Alliance Girls kutwaa nafasi ya pili ikiwa ni Mara yao ya kwanza kushiriki ligi hiyo.

Sambaza....