Sambaza....

Hapana shaka ndiye aliyewafanya wanachama na wapenzi wa klabu ya Yanga watembee wakiwa wametunisha vifua vyao. Wao ndiyo walikuwa wababe sana!, hakuna ambaye alikuwa anawatisha. Waliamini mitaa yote ilikuwa chini yao. Waliimiliki mitaa yote na kuiweka katika mikono yao.

Hakuna ambaye aliweza kuwatisha kwa sababu walikuwa na kikosi imara sana. Kikosi ambacho kiliweza kubeba ligi mara tatu mfululizo. Kikosi ambacho kilifanikiwa kutoa dozi kwa wapinzani wake. Kikosi ambacho kilikuwa kinaishi kitakavyo. Kwa kipindi kile cha Yusuph Manji ni kipi wachezaji wa Yanga walikuwa hawakipati?

Mshahara ulikuwa unafika kwa wakati. Ni nadra sana kusikia wachezaji wa Yanga wamegoma kisa hawajapewa mishahara kwa muda wa miezi minne. Kwao wao “njaa” ulikuwa msamiati sana. Hawakuwahi kujua maana yake na hawakutaka kabisa kujishughulisha kujua maana ya neno “njaa” kwa sababu walikuwa na shibe sana.

Mashabiki wa Yanga

Waliishi kana kwamba maisha yanaisha Leo. Hawakuwa wanawaza kesho itakuwaje. Hawakutaka kabisa kufikiria siku Yusuph Manji atakapoondoka ni aina gani ya maisha watayaishi? Hawakuayaandaa kabisa maisha ya kesho, wao waliamini Yusuph Manji ataishi milele na atabaki kuwa kiongozi wa Yanga wa milele. Hakutofanyika tena uchaguzi kwa sababu walikuwa na Yusuph Manji.

Huyu alifanywa MUNGU mtu na wana Yanga. Ndiyo maana hata alipotishia kuondoka Yanga kwa vipindi tofauti , wanachama wa Yanga walienda kumpigia magoti ili arudi tu.Alishujudiwa sana, alibudiwa sana, na waliamini yeye ni mkubwa kuliko Yanga. Na waliamini yeye ataishi muda mrefu kuliko Yanga. Na haya ndiyo maisha ambayo Yusuph Manji alikuwa anayafurahia.

Alikuwa anafurahia sana kuabudiwa. Na hapo ndipo alikuwa anapata nafasi ya yeye kutoa pesa ambayo iliwafanya Yanga iwe Yanga ya kutisha.

Yanga ambayo ilikuwa na wachezaji bora na waliokuwa wanaishi vizuri. Wanalipwa mishahara na posho vizuri tena kwa wakati bila malalamiko mengi.

Na kuna wakati walikuwa wanaenda kuweka kambi nje ya nchi. Hii ilikuwa jeuri ya fedha ya Yusuph Manji. Jeuri ambayo iliwafanya Yanga wawe na jeuri sana katika vijiwe mbalimbali.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji.

Jeuri hii kwa sasa haipo kabisa!, hawawezi kuongea kwa kujigamba tena katika vijiwe mbalimbali vya mpira kwa sababu sasa hivi ule msamiati wa neno njaa wameshapata majibu yake.

Wanaishi kwenye msamiati huo kwa sasa. Wachezaji wanacheleweshewa kulipwa mishara yao pamoja na posho. Hali ambayo iliwafanya wapoteze ubingwa wa ligi kuu msimu Jana.

Hawana wachezaji tena wengi wa kutisha. Wanarundo la wachezaji wa kawaida sana kwa sasa, na hayo yote ni kwa sababu uwezo wa kununua wachezaji bora kwa gharama kubwa hawana.

Walitegemea uimara wa mtu, hawakufikiria kabisa kutengeneza uimara wa taasisi yao. Hawakufikiria kabisa kuwa ipo siku Yusuph Manji ataondoka.

Hawakujiandaa kabisa na maisha ya wao kuishi bila Yusuph Manji. Hawakuamini katika kuiendesha timu yao kibiashara. Waliamini katika nguvu za mtu mmoja.

Ndiyo maana sasa hivi Yusuph Manji amewasusa na wao wanataka arudi tena. Hawaamini kama kuna kiongozi mwingine ambaye anaweza kuiongoza Yanga zaidi ya Yusuph Manji.

Sambaza....