Blog

Yanga inahitaji ubora, haihitaji kinywa cha ‘Manara wao’

Sambaza kwa marafiki....

RAFIKI yangu Dismas Ten ana vyeo viwili ndani ya Yanga. Cha kwanza ni Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, cha pili ni Ofisa Habari ‘kivuli’ wa timu.

Katika vyeo vyake viwili, cheo kimoja kimemuweka kikaangoni na watu wa Yanga. Baadhi yao hawalidhishwi na utendaji kazi wake katika idara ya habari. Wanamuona ni moja ya sababu ya wao kutojaa kiwanjani kwa wingi. Hapa kunashangaza.

-Disma Ten (Kushoto)

Dismas awakumbushe mashabiki majukumu yao asipowakumbusha wanamjia juu? Ni hapa kulikonishangaza. Shabiki anakumbushwaje kwenda kiwanjani? Hii inatokea Tanzania tu.

Mashabiki wanamuona Dismas yuko kitendaji zaidi ofisini na hayuko nje ya ofisi kama alivyo Ofisa Habari mwenzake wa Simba, Hajji Manara.

Mashabiki hao wanafura hasira wakiona jinsi Manara anavyofanya kazi zake, kisha wakimgeukia ofisa wao, wanaona kuna ‘gape’ kubwa aliloachwa.

-Mashabiki wa Yanga wakati wa mechi ya ligi ya mabingwa Afrika

Baadhi yao wameenda mbali na kusema kuwa msemaji wao haihitaji kuwa na elimu ya kiwango cha shahada. Dismas yuko zake kimya, hajamjibu yeyote yule. Anaishia kuzisoma comment za mtandaoni tu. Hajainua mdomo wake kumjibu mtu.

Kuna ukweli hauzungumzwi kwa Manara na hamasa zake na Dismas na ukimya wake. Kinywa ‘kichafu’ cha Manara, nyuma yake kina nguvu ya Mohamed Dewji ‘MO’. Jeuri ya kinywa cha Manara inaanzia katika pochi la MO kwenda maeneo mengine.

Manara hatumii nguvu kuwakumbusha mashabiki wa Simba juu ya kujaa kiwanjani kuishangilia timu yao. Pochi la MO limerahisisha kazi yake na kile
anachokisema mashabiki wanakielewa kiurahisi.

Hata wakati ule ambao Yanga walikuwa na Jerry Muro katika nafasi ya Dismas, nyuma ya ‘nyodo’ zake kulikuwa na mtu aliyeitwa Yussuph Manji.

Kwa kiasi kikubwa Manji aliirahishisha kazi ya Muro. Lakini kwa Yanga hii ambayo inaishi kwa nguvu ya buku, Dismas ana maajabu gani ya
kuwavuta mashabiki kwa wingi kiwanjani?

Dismas amekuja Yanga kipindi kibaya. Kama angekuwepo wakati ule wa Manji, tungeweza kukaa chini kumjadili, lakini kwa Yanga hii
inahitaji nguvu za hawafu mwenye nguvu ili kuwavuta kwa wingi mashabiki kiwanjani.

Ni rahisi kusema Yanga imedorora kwenye idara ya usemaji na uhamasishaji, lakini kwa Yanga hii ambayo haina uhakika kuifunga hata Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Dismas atoe neno gani kuwavutia watu waje kwa wingi kiwanjani?

Mashabiki wa Yanga wamekwenda mbali na kusema idara hiyo haiwezi kukwepa
lawama kwa kinachofanyika na kueleza kuwa tangu ameondoka Muro, idara hiyo
imepwaya. Ni rahisi kutamka hivi na ukaeleweka, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa Yanga ya Muro ilikuwa na Manji nyuma yake. Hii ina nani?

Yanga hii inayoishi kwa kutegemea michango ya wanachama ni ngumu kuwahamasisha watu na wakahamasika. Kuna sehemu lazima mtakwama.

Mashabiki wanaunganishwa na ubora wa timu kiwanjani, huku wakijua timu yao ina mtu wa uhakika kulipa mishahara na kusajili kila aina ya staa wanayemtaka. Ni rahisi kwenda viwanjani.

Mashabiki wanaunganishwa hivyo, hawaunganishwi kwa kinywa chenye maneno matamu na hamasa, huku timu ikiwa haina ubora wa kuwavutia.

Kazi ya Dismas inabezwa kutokana na Yanga kupitia nyakati ngumu kwa sasa tofauti na zama za Manji. Yanga wanahitaji kujihamasisha kabla ya Dismas kuwahamasisha wajae kiwanjani.

Leo hii Manara anaonekana kivutio kutokana na MO. Kabla ya MO wote tunakumbuka jinsi Manara alivyokuwa anatumia muda mwingi kulalamika. Leo angemlalamikia refa huyu, kesho angekuja na TV kwenye Press kuonyesha Simba inavyoonewa, keshokutwa angeilalamikia TFF kujaa Uyanga na angefungiwa. Haya ndiyo yalikuwa maisha yake. Muda mwingi alitumia kushusha lawama.

Lakini MO amekuja kumbadili Manara. Kazi yake kuu hivi sasa ni kuinadi Simba vyema, kuwaita mashabiki na kuwapiga vijembe Yanga. Zamani hakuwa hivi. Siku hizi ana kazi nyepesi. Ni kama anapaka siagi kipande cha mkate na kukila.

-Haji Manara, msemaji wa Simba Sc

Mazingira yaliyoko Yanga kwa sasa hayamsaidii Dismas kurahisisha kazi yake. Kama angekuwepo Yanga ya Manji, tungeweza kumpima na kujiridhisha, lakini kwa sasa tunamuonea bure.

Tujiulize kitu. Dismas hawezi kuwaita mashabiki kuja kiwanjani, mtu gani wa Yanga au nje ya Yanga anayeweza kuwaita mashabiki? Mshindo Msolla? Frederick Mwakalebela? Mzee Akilimali? Jimmy Kindoki? Mbwiga Mbwiguke? Masau Bwire? Utamtaja kila mtu, lakini jibu ni HAKUNA.

Msimu uliopita Simba iliwatumia MO na Sweddy Mkwabi kuwaita mashabiki uwanjani katika mchezo mgumu na mkubwa wa Al Ahly na uwanja ulijaa. Ni wao waliotangaza viingilio vya mchezo bila ya maneno ya shombo, lakini uwanja ulitapika.

Simba wamefanya hivyo na Manara akikosekana katika press na mashabiki wakajaa kiwanjani. Timu ikiwa bora haihitaji kunadiwa sana kama mashati mtumbani. Yenyewe inajinadi. Hesabu za kawaida tu kama Manara asiposema neno lolote kuelekea mchezo wa marudiano na wale Wamakonde wa Msumbiji UD Songo uwanja wa Taifa hautajaa?

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.