Sambaza....

Yanga ipo katika kipindi kigumu sana kwa sasa. Kipindi ambacho unahitaji moyo kukipitia. Ndicho kipindi ambacho kama mwanadamu wa kawaida unaweza kupoteza marafiki wengi sana na ndicho kipindi ambacho unaweza kuwajua marafiki wa kweli.

Hakuna mwanadamu anayependa shida hata kidogo, binadamu wote tunapenda tuishi maisha ya amani na furaha tele, ndiyo maana shida zinapogonga katika milango yetu chozi huteremka taratibu na kwikwi za kilio husikika sana.

Maumivu hujaa katika mioyo yetu, miili yetu hudhoofu hata nguvu za kufanya kazi hupungua na kuna wakati mwingine huwezi kutamani kufanya chochote cha muhimu kwa sababu huu ndiyo wakati ambao huwezi kuona thamani ya maisha.

Ndiyo wakati ambao wengi wanaweza kukukimbia, hata mchumba wako unayemwamini na kuhisi kuwa unaweza kuishi naye muda wote wa maisha. Hapo ndipo uhalisia wa maisha hujionesha mbele ya mboni za macho yako.

Uhalisia wa maisha uko hivo siku zote. Maisha yameumbwa kwa pande mbili. Upande wa furaha na upande wa maumivu. Na ukamilifu wa maisha hutimia kama hizi pande mbili hujionesha katika maisha ya mwanadamu.

Maisha hayawezi kukamilika bila mwanadamu kupitia pande hizi mbili, huwezi kuzikwepa lazima uzipitie, sema kinachokuja kutuumiza wengi wetu ni pale ambapo mioyo yetu tunapokuwa hatujaiandaa kwa ajili ya upande wa maumivu.

Manj (Katikati mwenye Fulana ya Njano) kwenye moja ya Mechi za Yanga

Wengi huwa hatutaki kabisa neno “Maumivu” kwenye maisha yetu. Hatupendi shida kabisa, ndiyo maana huwa hatujiandai kabisa kuingia kwenye shida kwa sababu hiki ndicho kipindi ambacho maumivu huenea kwenye kila kona ya maisha yetu.

Ndicho kipindi ambacho Yanga wanakipitia kwa sasa. Huitaji utabiri wa nabii yeyote kujua kuwa Yanga inapitia kipindi kigumu kwa sasa. Kipindi ambacho wanatumia nguvu kubwa tena kwa shida kuihudumia timu.

Wanakimbia nayo timu hivo hivo, ni jambo la kushukuru Mungu, wanaenda nayo kwa ugumu huo huo. Na kuna wakati wakishindwa wanakuja kwa wanachama na wapenzi wao kuomba msaada.

Kitu ambacho siyo dhambi kuomba msaada kwa wanachama nao, lakini ni kitu ambacho kinatakiwa kufikiriwa kwa ukaribu sana. Wataendelea kuwapigia magoti wanachama wao mpaka lini?.

Hao wanachama wakifikia hatua ya kuchoka ya kutoa hiyo elfu moja moja watatumia njia ipi ya ziada? Na mpaka lini wataendelea kuishi kiUJAMAA kwenye dunia hii kiBEPARI?

Tuko kwenye dunia ambayo maisha ya kijamaa yameshapigwa teke , hayapo tena na hayana faida sana katika maendeleo yetu. Ujamaa unachosha, ujamaa unaukomo wa uvumilivu, ujamaa una masimango, ujamaa hauna faida tena katika dunia ya Leo.

Dunia ya leo ni dunia ya kibepari, dunia ambayo vitu vingi vinafanyika kibiashara, dunia ambayo mpira ni biashara kubwa sana. Dunia ambayo mfanyabiashara yeyote hatakiwi kulia lia ili aonewe huruma.

Dunia ambayo mfanyabiashara anatakiwa atengeneze mazingira mazuri ambayo yatamwezesha mdhamini aje aweke fedha zake kwake ili apate faida ya uwekezaji wake.

Dunia ambayo klabu hatakiwi kulia lia inakosa vitu muhimu kwa ajili ya timu. Tena klabu kubwa kama Yanga. Yanga ambayo inaweza kutengeneza mazingira mazuri ambayo yanaweza kuwapatia GYM ambayo wanaweza kwenda kupiga mazoezi na wao kuitangaza hiyo GYM.

Dunia ambayo Yanga wanaweza kutengeneza mazingira mazuri wakapata hotel ambayo wanaweza kuweka kambi kwa makubaliano ya kibiashara, dunia ambayo Yanga wanaweza kuingia makubaliano ya kibiashara na kampuni moja la mafuta kwa ajili ya kupata mafuta ya kwenye basi lao kwa safari za kwenda mikoani.

Dunia ambayo inawapa nafasi Yanga kuzungumza kibiashara na kampuni ya ndege kwa ajili ya kuwasafirisha wachezaji wao kwa nusu bei huku wao wakiwatangaza kwa sababu Yanga ni sehemu kubwa ya kutangazia bidhaa kwa sababu ya idadi ya mashabiki waliopo ndani ya klabu hiyo.

Dunia ambayo inawaoa nafasi kubwa sana Yanga kuzungumza hata na mfuko wa jamii, au shirika la nyumba la Taifa au bank yoyote kuwajengea uwanja ambao watakuwa wanalipa pole pole kwa muda wa miaka kadhaa.

Dunia ambayo inawapa nafasi Yanga kuongea na shirika la Bima kwa ajili ya kuwakatia Bima wachezaji wao na wao kulitangaza kibiashara shirika hilo la Bima.

Hatuko kwenye dunia ya kumtegemea mtu atoe pesa zake mfukoni ili klabu iende. Tuko kwenye dunia ya kutengeneza taasisi ambayo inaweza kujiendesha kibiashara.

Ndiyo maana mimi siamini ujio wa Yusuf Manji kama mwenyekiti na kama ambayo wengi wanavyotamani iwe. Yusuf Manji amekaa Yanga kwa muda wa miaka 11 toka mwaka 2006 mpaka mwaka 2017.

Hakuna mazingira yoyote aliyoyatengeneza kwa Yanga kusimama kama wao kwa miguu yao. Alitengeneza mazingira ambayo Yanga walijiona matajiri , aliuficha ukweli halisi na alipoondoka ukweli ukawa wazi.

Yanga iliachwa ikiwa imedhoofika sana. Ilikuwa haina uwezo tena wa kusajili wachezaji imara na kuwalipa mishahara. Yanga ikawa inapoteza ushindani halisi ambao tulikuwa tumeuzoea kwa sababu tu iliiishi maisha ya uongo sana kipindi cha Yanga.

Iliishi maisha ambayo siyo yake. Wanachama wengi wamechoka kuishi maisha ya sasa, maisha ambayo ni sura halisi ya Yanga. Wanataka tena kuishi maisha ambayo siyo yao. Wanataka Yusuf Manji aje awe mwenyekiti ambaye atakuwa anatoa pesa zake kwa ajili ya Yanga, na siku akiondoka aiache Yanga isiyo imara.

Image result for mashabiki wa yanga

Hiki ndicho kipindi ambacho wana Yanga wanatakiwa kufikiria Mara mbili, na kufanya maamuzi magumu. Maamuzi ambayo yatawafanya waache kufikiria kuishi maisha ya kijamaa kwenye dunia hii ya kibepari.

Wachague viongozi ambao wataiwezesha Yanga iishi Kibepari na siyo kijamaa tena kwa kutegemea mtu na huruma ya elfu moja ya mashabiki wao.

Ndiyo wakati ambao wanatakiwa kuchagua akili na siyo pesa. Ndiyo wakati ambao wanatakiwa kupata kiongozi ambaye atakuwa na akili ya kuifanya Yanga iishi kibepari na siyo kijamaa. Ndiyo maana naamini Dr. Tiboroa anatakiwa kuingia kama mwenyekiti na Manji aje awekeze pale , apate faida na siyo kutoa pesa zake kwa hisani.

Sambaza....