Tetesi

Yanga Yapata Upinzani Katika Usajili wa Nyota Kutoka Afrika Kusini

Sambaza....

Young Africans iliyowatoa Gallants katika nusu fainali ya mashindano ya CAF haitaki kuwaacha hivihivi wababe hao wanaotoka Limpopo kwani wanataka saini ya mshambuliaji wao Rango Chivaviro mwenye mabao 17 msimu huu katika michuano yote.

Rango Alifunga bao lao pekee katika nusu fainali wakiwa nyumbani walipotoka kwa jumla ya mabao 4-1. Baada ya kucheza Kombe la Shirikisho, alizivutia klabu za Yanga, Azam FC, Kaizer Chiefs, Pyramids ya Misri na vigogo wa Cairo Zamalek, mshambuliaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Marumo Gallants.

Alipoulizwa kuhusu ofa hizo, fowadi huyo mzaliwa wa Afrika Kusini alisema: “Nitamwachia wakala wangu hilo. Kwa sasa, nataka kwenda nyumbani, na kuwa na mke wangu na binti yangu. Kuhusu ni wapi nitacheza msimu ujao, nitamwachia wakala wangu. Atanipigia simu na kunipa taarifa. Anajua ninachotaka.” 

Rango Chivaviro.

Chivaviro ameutaja msimu huu kuwa bora kwake kama mwanakandanda katika maisha yake ya soka. Kocha mkuu wa wakati huo wa Gallants Romain Folz alimsajili baada ya kufanya vyema majaribio mwanzoni mwa msimu.

“Kwangu mimi binafsi, huu umekuwa msimu wangu bora kama mwanasoka. Nimefunga mabao mengi, nimecheza michezo mingi. Ni kile unachokitaka kama mwanasoka anayecheza katika nafasi yangu ya ushambuliaji. Unataka kucheza michezo mingi iwezekanavyo na kufunga mabao mengi,” alimalizia Chivaviro.

Yanga wapo katika mawindo ya mshambuliaji mpya huku wakijiandaa na maisha mapya bila nyota wake Fiston Mayele ambe huenda akaachana na Wananchi mwishoni mwa msimu huu.

Sambaza....