Simon Msuva
Tetesi

Simba na Yanga Hawana Ubavu Wakumsajili Msuva

Sambaza....

Tangu jana nimepitia vijiwe vya kidigitali naona vimechangamka sana. Viko
moto. Nimeona taarifa ya Simon Msuva kuhusishwa kusajiliwa na Yanga Sc.

Sina hakika na taarifa hii. Wiki mbili zilizopita nilikutana na Msuva pale Escape One. Nilizungumza nae mambo mbalimbali ya mpira wetu na maisha kiujumla.

 

Sijui, narudia tena sijui, sijui tena. Lakini kiufupi tu, haiko timu ya kumsajili Msuva kwa hapa ndani kwa sasa. Haiko timu hii. Naamini hii itabaki kama tetesi na itaenda kujifia kifo cha kawaida. Kitakuwa cha kifo cha kawaida kabisa na hakitatushitua.

Yanga SC walikutana na jaribio dogo la kumbakisha Fiston Mayele wiki kadhaa zilizopita, wakashindwa. Simba nao wakashindwa pia. Ilikuwa miaka kadhaa iliyopita.

Wakubwa wameendelea kugawana mastaa wetu kadri wanavyojisikia. Chama alienda zake Morroco. Miqquessone akaenda zake Misri na Mayele nae kaenda Misri.

Luis Miquisone.

Kiurahisi tu wakubwa wanawasajili mastaa wetu tukiwa bado tunawatamani. Wao kiurahisi tu wanawachukua. Ni kama vile wanachanganya sukari na chai ndani ya kikombe kisha wanapeleka kinywani. Kwao ni jambo rahisi tu.

Kama hali ni hii, nguvu ya kumsajili Msuva inatokea wapi? Nawaheshimu mabosi wa Yanga SC na Simba SC wamefanya kazi kubwa kutuletea mastaa wa maana, lakini watu wanapaswa kujua thamani ya Msuva ni kubwa kuliko thamani ya hawa kina Chama, Mayele.

Ni ngumu kusema biashara hii haitowezekana lakini neno ngumu tunaweza kulitumia katika kuuzungumza usajili huu.

Simon Msuva akimiliki mpira.

Kama Msuva atasaini katika moja ya timu zetu kubwa atakuwa mchezaji ghali kuwahi kutokea kuanzia kwa wageni hadi ndugu zetu kina Feisal Salum na rekodi yake itachukua muda mrefu kuja kuvunjika.

Utakuwa usajili ghali tangu nchi yetu ipate Uhuru. Lakini nisijidanganye, siioni timu ya kufanya maajabu haya kwa kumsajili Msuva na kumpa fedha anazotaka.

Mwisho kabisa naweka kalamu yangu pembeni na kujisemea ngoja tuone.

 

Sambaza....