Naamini kupitia miguu ya Ibrahim Ajib Migomba, naelewa kupitia kipaji chake kabisa. Mimi ni mmoja wa watu ambao najivunia mboni za macho yangu kuona kipaji kikubwa kwenye miguu ya Ajib.
Miguu ambayo huufanya mpira umtii, umwelewe na autumikishe vile anavyotaka yeye kuufanya. Kwa kifupi Ajib Migomba ana kipaji ambacho ni dhambi kila weekend kuonekana kwenye kioo cha Azam TV.
Hajaamua kuondoka, bado anasita. Na bado hajaamua kuwa mkubwa, ukubwa wake huonekana sehemu ambayo anakutana na wadogo. Huwezi kumuona siku ambayo amekutana na mtu mkubwa.
Utamhurumia sana na unaweza kukataa kuwa huyu siyo Ajib ambaye ulimuona mechi iliyopita dhidi ya timu ya mkoani. Huwezi kuwa mkubwa kama hujapambana na wakubwa.
Lazima upambane na wakubwa, lazima miguu yako iweze kufanya vyema katika mechi kubwa. Mechi kubwa ndizo mechi ambazo macho ya wengi hutazama.
Mechi kubwa ndizo mechi ambazo hubeba hisia za watu wengi, ndizo mechi ambazo huitaji shujaa katika timu ili aibebe timu.
Kuna wakati timu hubanwa na ndiyo wakati ambao inahitaji ushindi. Wakati huu huitaji mtu ambaye anaweza kuibeba timu mgongoni na kukimbia nayo, hapa ndipo unapokuja kuiona taswira ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Hutumika katika kuibeba timu nyakati ngumu. Hujituma sana, wao ndiyo huwa watu wa mwisho kukata tamaa kwa sababu moja tu hawapendi kushindwa!.
Na hii ndiyo nguvu kubwa ya mafanikio ya mwanadamu yeyote duniani, kutopenda kushindwa, tena katika mechi ambazo zinaonekana ni kubwa.
Mchezaji mkubwa hufikia kuitwa mchezaji mkubwa siku ambayo anakuwa na mwendelezo wa kiwango chake, yani katika mechi ambazo zinaonekana ni ndogo acheze sana na mechi ambazo zinaonekana kubwa acheze zaidi.
Asiruhusu kushuka kwa kiwango katika mechi hizo, kuwe na mwendelezo wa kiwango chake kutoka mechi moja hadi mechi nyingine. Hapa ndipo ugonjwa wa Ibrahim Ajib Migomba ulipo.
Leo atacheza sana lakini akashindwa kucheza zaidi kesho hasa hasa hiyo kesho iwe na mechi ambayo inaonekana ni kubwa!. Ni ngumu sana kumuona anacheza katika kiwango kile kile ambacho ulimuona anacheza kwenye mechi ambayo ni ndogo.
Hapa anakosa sifa ya kuwa mchezaji mkubwa, mchezaji ambaye ana njaa ya mafanikio. Mchezaji ambaye hatamani kuendelea kuwepo katika kiwango kile kile kila uchwao.
Ndiyo maana niliandika kuwa Ibrahim Ajib Migomba ni mchezaji wa mechi ndogo tu. Hawajawahi kutamani kucheza katika kiwango kikubwa katika mechi kubwa.
Kwa kifupi hajawahi kuwa na mwendelezo wa kiwango chake!. Hapa ndipo tunapokuja kuzungumza lugha inayorandana na kocha wa Yanga Mwinyi Zahera .
Tunaweza tusizungumze kitu kile kile lakini kikawa kinarandana kwa asilimia kubwa. Kwanini ? , Mwinyi Zahera mpaka sasa hajaridhika na bidhaa ambayo inazalishwa kwenye miguu ya Ibrahim Ajib Migomba.
Macho yake yanaona kitu kikubwa ndani ya miguu ya Ibrahim Ajib Migomba. Hajataka kutumia macho ya nyama kuona hiki, na hajataka kuingia kwenye mkumbo wa kumsifia Ibrahim Ajib Migomba kama ambavyo sisi tunavyofanya.
Hajataka kabisa kuamini kile ni kiwango cha Ibrahim Ajib Migomba. Macho yake yanamuonesha kitu kikubwa ambacho hakijatoka kwenye njumu za Ibrahim Ajib Migomba.
Nafsi yake inazungumza ukweli, mdomo wake unazungumza nusu ukweli, mdomo wake unazungumza kwa lugha ya picha. Lugha ambayo ina ujumbe mzito.
Ujumbe ambao unamtaka Ajib apigane zaidi ya hapo. Ujumbe ambao unamtaka Ibrahim Ajib Migomba asibwete na sifa ambazo hazina faida. Ujumbe ambao unamtaka Ibrahim Ajib Migomba awe na mwendelezo wa kiwango chake.
Yani kwa kifupi kiwango ambacho anakionesha kwenye mechi dhidi ya Stand United kiwe kiwango zaidi na kile atakachokionesha dhidi ya Simba , au akiwa na jezi ya timu ya taifa ya Tanzania.
Kwa kifupi Mwinyi Zahera anaongea Lugha ambayo ina mirindimo sawa na Lugha yangu ambayo nishawahi kuiongea kwenye makala yangu ambayo nilisema “Ajib ni mchezaji wa mechi ndogo”. Sijawahi kuridhika na mwendelezo wa kiwango cha Ibrahim Ajib Migomba, siku akifanikiwa kuwa na mwendelezo mzuri nitakaa chini na kuandika pongezi zangu kwake, kwa sasa bado ana kazi ya kuishawishi kalamu yangu kumwaga wino kwa akili ya kumsifia yeye.