Aden Rage
Blog

Alhaji Ismail Aden Rage, Hakuna mjinga mwenye ujinga mtupu.

Sambaza....

Athuman Idd Chuji ni shujaa kweli kweli, Mwaka 2011 alipopata Matatizo na timu yake ya Yanga aliamua kuvuka barabara na kuelekea Simba SC na kusajili kwa ajili ya msimu mpya na mashindano ya Kagame Cup, hili lilitokea japo mwaka 2008 Usajili wake wa Utata toka Simba kwenda Yanga ulizua sintofahamu kati ya vilabu hivi viwili Pinzani, kufikia hatua kwa Mchezaji huyu kuiambia TFF kuwa hawezi kurudi Simba na kama watamlazimisha kurudi Simba atarudi kwao Dodoma akauze Ndimu….. Kauli hii ilikuwa Gumzo kuu katika jiji la Dar es salaam na Tanzania kwa ujumla, lakini mwaka 2011 alikula matapishi yake.

Katika hili mimi naamini kwa asilimia mia moja Chuji alikuwa Mshindi kwa sababu Tanzania kwa Mchezaji wa Kariba ya Chuji kama huchezei Simba basi utakuwa Yanga, lakini kitu cha Kushangaza baada ya mashindano ya Kagame Simba wakaamua kumpeleka kwa Mkopo timu ya Villa Squad ya Magomeni kisa kiwango chake hakikuwa Bora, Mchezaji aliyeachwa na wapinzani wakubwa wenu na watani wenu wa jadi sababu ya kiwango Duni na matatizo ya matumizi ya madawa ya kulevya vipi Simba mumtake? Hili la kupelekwa Villa Squad Mchezaji mwenyewe alilikataa hapa ikabidi Simba wavunje Mkataba walitumia kiasi gani cha Pesa Kumlipa Chuji siri yao….. nani anajua? Mh. Rage alikuwa mwenyekiti wa Simba kipindi hiki na hili lilitokea kwenye Uongozi wake watu wakakaa Kimya kama hakuna lililotokea na huu ndio Mpira wetu ulivyo, lakini wadadisi wa Mambo tuliona hili ni Tatizo.

Sakata la Kelvin Yondani, hili ndilo haswa lilimchafua Mh. Rage, Yondani akiwa mchezaji halali wa Simba SC aliamua labda kwa kushawishiwa au kwa ridhaa yake mwenyewe kujiunga Yanga SC kwa mapungufu  makubwa yaliyokuwa kwenye Mkataba wake wa Simba ambao ulionyesha kuwa ataitumikia timu hiyo kuanzia Disemba mwaka 2012, Yanga wakapita kwenye Upungufu huo wakamsajili Yondani, Mh. Rage akatamba na kutumia viswahili vya mjini akisema  Yanga “Imekula kwao  na wakaonyesha Mkataba wao Yondani na Ule wa Yanga na Yondani Hadithi hii ilikuwa ndefu kweli kweli mwisho ikapewa Jina la Filamu ya Yondani,  siku zikapita wiki na miezi Yakaja Mashindano ya Kagame Cup, Yanga wakalipeleka jina la Yondani kama Mchezaji wao Halali na Simba wakafanya vivyo hivyo……. Unajua kilichotokea Simba chini ya Mh. Rage wakashindwa Vita hii, Baadae Ikaja Ligi Kuu ya Tanzania Simba Ikashindwa tena vita hii pia! Rage akabaki kulalama hujuma ndani ya TFF.

Ligi ya Msimu uliopita iliisha kwa Kishindo Mno kwa Upande wa Simba SC, kwasababu walimpa kipigo kikubwa mno cha kihistoria mtani wake Yanga cha mabao matano kwa Sifuri, na mara baada ya Kuisha kwa Ligi Simba iliingia katika Usajili akasajiliwa Kiungo Mahiri kutoka DC Motema Pembe Patrick Nkanu Mbiyavanga, usajili huu ulikuja kufatia mchezaji huyu kung’ara vilivyo katika mechi iliyoikutanisha Simba na klabu yake ya awali ya DCMP kwenye mashindano ya Shirikisho, pale uwanja wa Taifa Mpya na Simba kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri likifungwa na Mussa Hassan Mgosi.

Baada ya Yondani kupitishwa kucheza Yanga kwenye Kagame Cup Simba wakasajili Beki kutoka Congo aliyejulikana kwa jina la Lino Masombo, kwa mtazamo wangu hakuwa Mchezaji sahihi kuja kuziba mahala palipoachwa wazi na Yondani na katika muda mfupi tu akafeli, sasa Swali hapa lakujiuliza inakuaje timu kubwa Kama Simba yenye Viongozi wanaoshika Nyadhifa kubwa Serikalini ifanye usajili mbovu kama huu?, baada ya mashindano yale ya Kagame lino Masombo pamoja na Nkanu Mbiyavanga walivunjiwa mikataba yao na Kulipwa mamilioni ya pesa na kutokomea nayo kwao Congo DRC.

Baada ya Hadithi ya Wakongo hawa wawili kuisha Ukaitishwa Mkutano wa kila mwaka wa Viongozi kukutana na wanachama, Haya mambo huwa hayasemwi popote pale.Mheshimiwa Ismail Aden Rage tena akaja na mada kuu mbili kubwa moja ya Kuchangisha pesa za kwenda kulipia gharama za umiliki  wa Ardhi yao na walikuwa wanatafuta kiasi cha shilingi mil 30 za kupata hati ya umiliki wa eneo hilo litakalojengwa uwanja wa kisasa, Rage aliwaeleza wanachama kuwa, kiasi hicho ndicho kilichobaki baada ya uongozi kulipa sh mil 50, kwani thamani halisi ya kumiliki eneo hilo ni mil.80., na Pili ni usajili wa beki mmoja wa Kati Imara na jina lililokuja lilikuwa ni la mchezaji Mbuyi Twitealiyekuwa akichezea timu ya APR ya Rwanda, Wanachama wa Simba SC wakatii Ombi la Mwenyekiti wao na zikachangishwa pesa zilizofika Milioni 30, Katika hatua hiyo, Rage na Makamu wake (Kaburu), kila mmoja alitoa kiasi cha sh mil tano, Hansi Pop (mil 10), Mjumbe Swed Mkwabi (Mil. 3), Said Pamba (mili 2), Lameck Patel na wadhamini TBL kupitia kwa muwakilishi wao George Kavishe, milioni moja.Hapa nakupongeza Mh. Rage lakini baada ya kuonyeshwa zile ramani za uwanja za wakandarasi toka Uturuki hatujui hadithi hii iliishia wapi usiulize utapewa majibu ya Mzaha hapa, Hakuna aliyeuliza na ukiuliza utapigwa Siasa hadi usikumbuke uliuliza swali gani.

Baada ya mkutano ule Mheshimiwa akafunga safari hadi Rwanda na kufanya usajili wa Mchezaji Mbuyi Twite kiholela holela wakitumia zaidi ya dola elfu 39 na kusema haikuwa kazi rahisi kumsajili mchezaji huyo kwani wapinzani wao wakubwa walikuwapo Kigali na kumpigia Simu Mchezajihuyo na kuwajibu kuwa yupo na watu wa Simba na amesha saini Simb SC kwa mujibu wa Mwenyekiti huyu wa SimbaSC, na kwenye Tamasha la Simba Day Mbuyi Twite akatambulishwa kwa kutumia Jezi ya Simba iliyokuwa na namba 4 mgongoni akisubiriwa kuwasili kuanza kuitumikia Simba SC.

Yanga SC waliona nini sijui? Waligundua vipi mapungufu ya mkataba ule sijui? wakalivamia dili hili wakamsainisha mchezaji kwa kufuata utaratibu kwani chanzo kimoja kilipasha kuwa Mbuyi na Ndugu yake Kabange ni wachezaji wa FC Lupopo waliokuwa APR kwa mkopo hivyo wamiliki wa wachezaji hao ni FC Lupopo, Yanga wakawalipa Lupopo wakapewa haki zote za Mchezaji, Mh. Rage akikaribia kulia bila aibu akasema kuna mtoto wa kigogo mkubwa Nchini anatumiwa kuiua Simba lakini atashindwa, Washabiki na Wanachama wa Simba wakalishwa maneno haya mabaya yaliyopandikiza Chuki kati yao na Yanga, Mchezaji mwenyewe Mbuyi Twite na huyo mtoto wa Kigogo Mkubwa Nchini, suala likarudi TFF wakaamua kuwapa Yanga siku 21 wawe wamelipa hizo pesa za Simba, kimsingi hapa aliyetakiwa kurudisha pesa sio Yanga bali ni Mchezaji mwenyewe, lakini cha ajabu siku 21 zimepita kitambo saaana hadi leo Zile pesa hazijalipwa.

Usajili wa Konmabil Keita, Pascal Ochieng na Daniel Akuffor vilitumika vigezo gani kuwasajili wachezaji hawa? Hadi leo sijapata majibu ya swali hili, ama kwa hakika katika mwaka ambao Simba wametia aibu kwenye Usajili wa wachezaji wa kigeni ni Mwaka huu, ikiwa hata Ligi haijaisha ishavunja mikataba na wachezaji wa-nne wa Kigeni, Alichonisikitisha Mheshimiwa Rage kwenye kuvunja mikataba ya Wachezaji Akuffor na Ochieng ni kujifanya kuwa hakumfahamu mchezaji Daniel Akuffor kwa jina wala kwa sura, hii inakupa Taswira gani? Kwangu nilichoelewa Mhe. Rage anataka kuwaonyesha Wapenzi na wanachama wa Simba ni wajinga.

Wakati Mashindano ya BancABC SUP8R yanaanza Simba SC iliamua kuchezesha kikosi chake cha pili kiitwacho Simba B, Uongozi wa juu wa Simba ukasema kama Timu hiyo itatwaa Ubingwa basi pesa za Ubingwa itawapa wachezaji wao wagawane, Vijana wakavuja jasho kweli kweli wakashinda Kikombe na Pesa Taslimu za Kitanzania shilingi Milioni Arobaini unajua kilichofata baada ya hapo? Wale Watoto wakaonekana hawastahili kupewa zile pesa wagawane kama walivyoambiwa mwanzo badala yake pesa zitaingia kwenye Akaunti ya Timu na kufanya Shughuri nyingine, kwasababu wachezaji wale walikuwa wanalipwa mishara na Simba SC.Hakika jambo hili lilinisikitisha na sikutegemea lisemwe na Kiongozi mwenye nyadhifa mbali mbali kama Rage.Ninachokiamini ni kwamba wachezaji wale walijituma sana baada ya kuambiwa kuwa wakishinda kikombe kile watapewa pesa za Zawadi wagawane na wakafanikiwa kukitwaa, na upande wa Rage kwanini nisiamini alisema vile kwa kuamini kuwa vijana wale wasingekuwa na Ubavu wa kushinda kikombe kile kwa kuwa kulikuwa na Timu kama Azam Fc na Mtibwa Sugar zilizoingiza vikosi vyao vya kwanza, wakati mashindano yakiendelea kukaibuka mambo mengi sana kwamba Timu ya Simba B ilikuwa ikiongozwa na watu watatu tu ambao ndio walikiuwa wanafanya kila kitu kitokee kwa kushirikiana na wadau wa Simba wenye mapenzi na timu yao kama Mlamu Ng’hambi ambae alikuwa akitoa pesa za posho na maandalizi kwa timu hii B ya Simba SC, watu hao walikuwa Meneja Patrick Rweyemamu, Makocha Selemani Matola na Msaaidizi wake Amri Saidi, baada ya danadana za muda mrefu ikaripotiwa kuwa Vijana wale wamepewa sehemu ya pesa zile walizoshinda kwenye kombe la BancABC SUP8R kitu ambacho hakikuwa kweli, katika hili Rage unahusika asilimia mia moja.

Mashindano ya UHAI Cup yaliyoisha wiki moja iliyopita yameniacha na Maswali mengi mazito ikiwemo Taarifa kuwa Uongozi wa Simba uliamua kuwatimua Meneja wa timu ya Simba B na Kocha wake Mkuu Selemani Matola, ilihali vyombo vya habari viliripoti kuwa Patrick na Matola waliamua kuachana na timu hiyo baada ya kuona hakuna uelekeo wowote, namnukuu Patrick “…uongozi wa klabu hiyo umeoza na hawawezi kuongoza kwa ufanisi kwa ajili ya maendeleo ya klabu yao” akaendelea Patrick alisema “…viongozi wa Simba hawana jipya na wameshindwa kabisa kuongoza kwa ushirikiano. Alisema kwamba wameshindwa kuiandaa timu pamoja na kutoa walau fedha ndogo za nauli, huku wakiwa wepesi kushangilia matokeo ya ushindi uwanjani. Hii ni mbaya kwa timu kama Simba inayoangaliwa na kila mmoja wetu, hivyo nadhani suala hili haliwezi kuibeba timu yetu ndani na nje ya nchi ikiwamo hiyo ligi ya Mabingwa, Viongozi hawapo makini na ndio maana kwa pamoja tumeamua kujiondoa katika timu, huku nikiwataka kuacha kupotosha umma kuwa wametuondoa klabuni,”mwisho wa kumnukuu. Hapa napata wasi wasi na maneno aliyosema Mhe. Rage baada ya timu hii ya Simba B kushinda kikombe cha BancABC kwa kusisitiza kuwa watawasaidia kadri wawezavyo sasa iweje washindwe hata kutoa pesa ya Nauli kwa timu hiyo? Huku siku chache zilizopita wakitumia zaidi ya dola elfu arobaini kumsainisha mchezaji Emmanuel Okwi na kiasi kingine kikubwa kwa Abel Dhaira.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kilicho karibu na timu hiyo ya Simba B kimesema uongozi wa klabu hiyo umekuwa ukiwatelekeza wachezaji wa timu hiyo kwa muda mrefu katika kuwapa mahitaji yao ya kimsingi – “Kiukweli uongozi hauna habari hata kidogo na hii timu B, wamewaachia Matola na Rweyemamu kila kitu. Wachezaji wanadai mishahara ya miezi mitatu sasa, fedha zao za ushindi wa Kombe la BancABC hawakuambulia kitu chochote. Na juzi zile fedha za maandalizi walizotoa wadhamini wa Uhai Cup, wamechukua na kwenda kulipia gym kwa ajili ya timu A huku wakishindwa kutoa hata senti tano kwa ajili ya timu husika yenye kushiriki kombe la Uhai ambayo ni timu B. hapa ilikuwa inasubiriwa timu ishinde kikombe Mhe. Rage uwe mstali wa mbele kupiga picha na kikombe kama ulivyofanya kwenye makombe mengine kama vile UHAI Cup mwaka jana, BancABC SUP8R na Kombe la KINESI kama unaifanyia chochote cha maana timu hii kumbe hakuna lolote.

Pesa za RAMBIRAMBI zilizochangishwa na wapenzi wa mpira siku ile ya Kuuaga mwili wa Marehemu Patrick Mutesa Mafisango ‘petit’ pale TCC club Chang’ombe, ili zipelekwe kwa familia yake maana hawakuwa washabiki wa Simba pekee, hii ni AIBU nashindwa kuelewa kama hata kwenye vikao vyako vingine watu hawakuulizi, mmepiga danadana zile pesa hadi watu wamesahau, katika kauli iliyonisikitisha ni ile iliyotolewa na msemaji wa Simba kuwa zile pesa zilichangwa kwa wafiwa ambao ni Simba na Mafisango alikuwa muajiriwa wa Simba, kauli hii niliipinga, nikajiuliza mimi ni muajiriwa wa kampuni ya GALACHA nikapata ajali nikafa, watu wananitambua kupitia GALACHA wakanichangia michango ya Rambirambi wakiipeleka kwa mwajili wangu ambae ni GALACHA ili anifikishie kwa urahisi, hivi GALACHA ina haki ya kuizuia na kusema kuwa zile pesa wamechangiwa wao wakiwa kama wafiwa ilihali mimi nimeacha Familia yangu iliyokuwa inanitegemea, sikupata majibu lakini kama ni hivyo basi naamini Kampuni yangu ilibidi itumie Busara kubwa, haya Pesa za watu waliochanga mmekula, Pesa za Simba kama Rambirambi kwa Familia ya Mafisango nazo ziko wapi? Hivi Mhe. Ismail Aden Rage unajua unaongoza watu wa aina gani kweli? Unataka kuionyesha nini Jamii muonekano wa Simba SC kwao?Wachezaji nao ni binadamu wanalichukuliaje hili suala la RAMBIRAMBI za mwenzao?

Kuna yule aliyekuwa msemaji wa Simba SC Bwana Cliford Mario Ndimbo, ulipomwita Karani ulitaka tujifunze nini kutoka kwako? Yaani Mwenyekiti ni wewe, Msemaji wa timu ni wewe, Katibu ni wewe, Anaehusika na kusajili wachezaji ni wewe, Anaepokea vikombe timu ikishinda ni wewe, Anaefungua Matawi ni wewe, Kupokea wageni ni wewe, basi fukuza wote ubaki peke yako na Simba yako lakini jua kuwa neno KIONGOZI lina maana nzito sana, nayo ni:

K Kubali Ushauri
I- Ielewe Hali ya Mahali Ulipo
O Ondoa Upendeleo na Uonevu
N Nena Kauli Thabiti Daima
G Gawa Madaraka Kwa Unao Waongoza
OOnyesha Mfano Kwa Vitendo
Z Zuia Migogoro Kazini (Klabuni)
I Inua Kiwango Cha Utendaji Kazini (Klabuni)

Mhe. Rage kuendelea kuwa mbunge hainipi shida aukuongoza jumuia ya wazazi CCM Tabora sioni tabu…. shida inakuja anapoiongoza Simba kwa mtindo wa mwaka huu kuanzia uzembe wa kumsajili Yondani mpaka usajili mbovu kabisa wa wachezaji wa nje ya Tanzania ,ahadi hewa za ujenzi wa uwanja, kutopeleka pesa ya Rambirambi ya Marehemu Patrick Mutesa Mafisango mpaka aibu ya kuwalipa U-20…… naipenda sana Simba ila uongozi huu wa Mhe. Rage hapana.

Kali ya kufungia mwaka ni pale ulipoambiwa Tawi la Mpira Pesa limedhamiria kukutoa madarakani kwa sababu ya utendaji wako Mbovu walikuwa wanakusanya kura za maoni toka kwa wanachama wa Simba ili wakuondoe Madarakani, ulikuwa mkali kwelikweli kwanini uliumia sana, siku ya pili ukaja kwenye vyombo vya habari ukifura kwa hasira kwa kusema hukulala usiku kucha unapitia makabrasha yako kujua kama hao Mpira pesa wanaweza kukutoa madarakani, kwangu lile lilikuwa Fundisho sasa sijui kama wewe umepata Somo lolote pale, kama hukupata somo basi ngoja nikudokeze hapa, hili niliambiwa na rafiki yangu Ismail Mohamed, inawezekana wanachama na washabiki wa Simba pamoja na viongozi wa matawi mbali mbali ya klabu ya Simba ya zamani na yanayofunguliwa hivi sasa wakawa wajinga tena mbumbumbu wasio na Akili kabisa lakini jua kuwa

…….HAKUNA MJINGA MWENYE UJINGA MTUPU!


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.