Blog

Amissi Tambwe na simulizi za Mario “Super” Jardel..

Sambaza....

-Makala hii imewekwa tena leo lakini ni ya mwaka 2014. Ni moja ya kumbukizi tukielekea sheherekea miaka 8 ya tovuti.-


Mário Jardel de Almeida Ribeiro alizaliwa tarehe 18 Septemba 1973 ni mchezaji mstaafu wa kibrazili. Jardel alikuwa anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kujua kujipanga vizuri uwanjani na uwezo wake mkubwa wa kupiga mipira ya vichwa. Jardel ni mchezaji wa kukumbukwa wa wakati wote wa Gremio, na alikuwa sehemu muhimu katika kikosi kilichoshinda Kombe la vilabu bingwa vya Amerika ya Kusini mnamo mwaka 1995 maarufu kama “Copa Libertadores”. Kwa uwezo wake wa kipekee wa kukaa katika nafasi muhimu uwanjani, alikuja kuwa Straika wa Kiwango cha Dunia huku akifunga magoli ya kutosha yaliyompambanua na kumfanya kuwa bora Ulaya nzima, na katika kipindi chake alichocheza katika vilabu vitatu vya FC Porto, Galatasaray, and Sporting CP, kwa nyakati tofauti alifunga magoli 266 katika mechi 274 kwa vilabu hivyo vitatu. Huku akishinda zawadi binafsi kama;
• European Golden Shoe: 1998–99, 2001–02
• UEFA Champions League top goals scorer: 1999–2000
• Portuguese Golden Ball: 1997, 1998

Mário Jardel de Almeida Ribeiro

Lakini kwa mshangao wa wengi pamoja na rekodi zote hizo za “kutisha” katika ngazi ya klabu Mario “Super” Jardel alicheza mechi kumi (10) tu za timu yake ya taifa ya brazil na kufunga goli moja tu katika kipindi chake cha miaka 22 ya kucheza soka la kulipwa akianzia klabu ya Vasco da Gama (1991–1995)nchini mwake Brazil alipocheza mechi 50 akifunga magoli (26) na kumalizia katika nchi ya Saudi Arabia katika Klabu ya Al Tawoun mwaka 2011 alipocheza mechi 17 na kufunga magoli 18.

Mwaka 1999 ndio mwaka niliopata kumfahamu Mario “Super” Jardel na kufanya jitihada za kumjua kiundani baada ya kufanya maajabu makubwa akiwa na klabu ya Porto FC kwa msimu wake wa tatu mfululizo alipofunga magoli 54 katika mechi 47 za mashindano yote, nikajiuliza huyu Jardel ni nani haswa? Na ni Raia wa nchi gani? Ndipo nilipokuja kuona rekodi nyingine nyingi za kutisha za mkali huyu aliyezaliwa huko Forteleza, nchini Brazil.

Miaka imepita na kwenda kwa kasi lakini ni miaka mitatu tu toka mkali huyu alipotundika daruga zake, kama nikiulizwa mchezaji ambae alikuwa ni namba tisa haswa mwenye kulijua goli na kujipanga vizuri uwanjani nitamtaja Mario Super “Jardel” bila kusita. Walikuwepo kina Hernan Crespo, Filipo Inzagi, Giovane Elber, Patrick Kluivert na siku za karibuni Javier Hernandez Chicharito lakini kati ya wote hao hakuna aliyemkaribia Mario Jardel kwa kulijua goli lilipo.

Wakati nikiendelea na masikitiko yangu ya Super Mario kutopata nafasi ya kutosha katika kikosi cha Brazil, nikakutana na majibu haya, Mario Jardel hakuweza kuuchezea mpira, Mario Jardel hakuweza kupiga chenga hata mchezaji Mmoja, Mario Jardel hakuweza kukota mpira hata hatua kumi kwa kasi ya kuwatoka mabeki! Nikabaki nimeduwaa kwa mshangao mkubwa, nikafadhaika sana, nikawauliza wataalamu hao wa masuala ya mpira wa wakati huo kwa jinsi huyu jama anavyofunga kadri anavyopenda na kuvipa vilabu vyake tofauti Ubingwa sisi tunataka chenga za nini? Tunataka akimbie na mpira aende nao wapi? Mwisho wa siku Brazil ikaja kuwapa nafasi washambuliaji wa hovyo kabisa waliokuwa na kazi ya kupiga machenga bila faida kina Denilson, Marcelinho Paraiba na Franca ambao muda wao wa kucheza mpira ulikuwa mfupi kuliko ulivyo mkia wa mbuzi.

Edson Arantes dos Nascimento Pele aliwahi kumponda Mario Jardel kwa kusema anafunga magoli lakini sio “magoli matamu”, katika kujibu kijembe hicho Mario alisema hakuna goli lisilokuwa “tamu” kwenye macho ya mashabiki, magoli yote ni “matamu” na ndio maana kila linapofungwa goli iwe limefungwa kwa mguu au pua kama nyavu za wapinzani zitatingishika basi washabiki watalipuka kwa shangwe.

Leo hii ukisikiliza mijadala ya wanaojiita watu wa mpira wanakwambia Amissi Tambwe hana jipya, hana radha, kaishiwa na watu wa Simba SC na Viongozi wa Simba SC wameenda mbali zaidi walisema wanaachana na Tambwe katika dirisha la usajili lililopita kwasababu kila kitu anachokifanya uwanjani hata Edward Christopher alikuwa anafanya sana, lakini kelele za mashabiki kwa mchezaji wao kipenzi ambae alifunga magoli 19 katika mechi 22 za msimu wa ligi huku timu ikiwa dhofli hali ikimaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, ziliwazuia kufanya maamuzi yao yale ya kifedhuli.

Okwi

Ujio wa Emmanuel Arnord Okwi na Rafael Modo Kiongera huku nguvu za Elius Maguli zinafifisha safari ya mfungaji huyu maridhawa wa magoli ya mguu wa kushoto, magoli ya mguu wa kulia na magoli ya vichwa, watoto wa uswahilini wanakwambia “maisha hayapo fair” kila nikitafakari alichofanyiwa Amissi Tambwe katika mechi saba za ligi nashindwa kuelewa kama watu wa Simba wapo makini, lakini hii yote ni katika kuwaaminisha tu washabiki kuwa kile ambacho walitaka kukifanya kabla kuanza kwa msimu huu mpya kwa kumuacha Tambwe walikuwa sahihi kabisa.

Dirisha dogo limefunguliwa kila siku mpya ya vyombo vya habari vya hapa nyumbani vinataja majina ya washambuliaji wengi mno wakihusishwa na ujio wa kuja kuchukua nafasi ya Tambwe, wametajwa washambulizi wengi wengi kuanzia Emmeh Ezechukwu, Dan Sserunkuma wa Gor Mahia, Dan Mrwanda, Hamisi Kiiza ambaye hali yake si shwari kwenye klabu yake ya Yanga, Ame Alli na wengine wengine.

Kila nikijiuliza nafasi aliyopewa Amissi Tambwe na dakika zake uwanjani inasikitisha kusikia hizi shutuma za kushuka kwa kiwango chake, kuna muda najiuliza kama kocha Patrick Phiri alipata hata muda wa kuangalia timu ya Simba SC ilivyocheza msimu uliopita na nafasi ya Tambwe uwanjani, nashindwa kuelewa kwa Mshambuliaji aliyefunga magoli 19 ya msimu kocha mpya anaekuja anashindwa kumuelewa? Anashindwa kumtafutia mfumo ambao unaweza kumfanya acheze huru, anashindwa kuangalia mfumo uliokuwa unatumiwa na mtangulizi wake na kuona ni jinsi gani ya kuuboresha.

Nimemuona Tambwe akicheza mechi 6 msimu huu tatu kati ya hizo akiwa ameanza na tatu akiwa ameingia akitokea benchi huku mechi moja tu akicheza kwa dakika 90 akifunga goli moja tu hadi sasa, na nikiifikiria ile rekodi ya Mario “Super” Jardel ya mechi 10 tu za Timu ya Taifa ya Brazil katika kipindi chake chote cha uchezaji wa soka la ushindani namuona Tambwe akiwa kabakisha mechi nyingine tatu tu za kuendelea kuwapo Simba SC kwa maana ya kucheza, sioni ni vipi watu wa Simba SC na viongozi wake wanaweza kukubali na kuendelea na mchezaji ambae wanamuona ni goigoi, mchezaji anaesubiri kufunga tu, mchezaji asie na ladha.

Amissi Tambwe umeponzwa na mabao yako mepesi uliyokuwa ukifunga kwa kushirikisha akili nyingi na uwezo mkubwa wa kuwasoma mabeki na kujua jinsi ya kukaa kwenye maeneo ambayo ulionekana na kuchezeshwa na kufunga, kama alivyoponzwa Super Mario Jardel, na sio uwezo wako wa kujipanga vyema kwenye nafasi na kufunga mabao rahisi akili ambayo wachezaji wengi hawana na kuishia kufunga magoli ya kupambana na mabeki kwa kutumia nguvu nyingi bila akili na kuonekana kama mashujaa na kupewa sifa ya kufunga magoli magumu, kwa sasa nimetega macho yangu kuona Mshambuliaji ajae wa Simba SC atakuwa yupi katika mlolongo uliotajwa.

Nachokiamini ni mazoea yetu mabaya ambayo leo yanakuondoa, tumekuzoea kiasi kwamba tunakuona wewe sio hatari tena, dah! Namsubiria huyo mshambuliaji wao mpya akifika atakuwa na nini cha ziada, ila kama atafunga kwa mguu wa kulia ama kushoto ama kwa kichwa kama ulivyokuwa ukifunga basi ni muda tu ndio utakaowatenganisha katika kuondoka kwenu Simba SC, naamini nae atakuja tutamzoe mwisho tutasema Striker wa kati hawezi kuwa “mbilikimo” Tutasema Striker wa kati hawezi kuwa “Mpemba” tutasema ndio kawaida yetu!

Dizo Moja

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x