Sambaza....

Kocha wa Mbao FC Amri Said, amelalama kuwa sababu kubwa ya kupata matokeo mabovu katika mechi za hivi karibuni ni kutokana na kikosi chake kufa eneo la kiungo.

Said ambaye ni beki wa zamani wa Simba na Kocha wa Lipuli amesema eneo la kiungo limekuwa likimwangusha kwa kadri siku zinavyokwenda na ndio maana ameuomba uongozi wa klabu kumletea beki namba tano kutoka Simba SC ambaye hajamtaja jina lake ili kusaidiana na viungo wake, ila amethibitisha kuwa mazungumzo yanakwenda vizuri na pengine atajiunga kabla hata dirisha dogo halijafungwa Jumamosi wiki hii.

“Tatizo ambalo linanisumbua zaidi hivi sasa kwanza ni midfield, viungo vyangu kwa kweli havijaperform vizuri katika mechi hizi kadri siku zinavyokwenda lakini najaribu kurekebisha, ni tofauti tulivyocheza mechi ya Azam na hii ya African Lyon, lakini naamini kabisa mechi inayokuja nitacheza vizuri, mapungufu ninayoyaona ni kwenye kiungo na naamini nitayafanyia kazi,” amesema.

“Bado kwenye kikosi changu nafikiri namba Tano anatakiwa atafutwe, kuna mchezaji tunafanya naye mazungumzo ambaye ameshawahi kucheza Simba kipindi kirefu ni kijana chipukizi ataingia wakati wowote katika kikosi, tayari nishatoa maagizo kwa uongozi na wanalifanyia kazi, lakini pia tunahitaji Mshambuliaji mwingine ambaye naye Yupo naye kwenye mazungumzo ya mwisho,” amesema.

Ikumbukwe katika mechi tano za Ligi zilizopita Mbao FC haijafanikiwa kupata ushindi wowote wakiambulia alama nne kutoka katika sare na nne na kupoteza mara moja dhidi ya Azam matokeo ambayo yanawafanya kushika nafasi ya saba Baada ya michezo 16 wakiwa na alama 21.

Sambaza....