John Bocco
Stori

Azam Fc: Ni Rahisi kwa Mchezaji Kutoka Azam na Kwenda Kung’aa Yanga na Simba. .

Sambaza....

Katika kile kinachoonekana kuendelea kumjibu mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele baada ya kusema Azam ina wachezaji wanaokamia timu kubwa, Zakaria Thabit ameendelea kumjibu nyota huyo.

Katika andiko hili ameonyesha jinsi ambavyo timu ndogo zinavyowakamia wao Azam kutokana na umiliki wa klabu yake.

“Ukitaka kujua kuchezea Azam FC ni kazi kiasi gani, waulize wachezaji waliokuwa Azam FC kisha wakaenda Simba au Yanga, au waliokuwa Simba au Yanga kisha wakaenda Azam FC,” alisema na kuongeza

Salum Aboubacar “Sure Boy” akipiga mpira mbele ya kiungo wa timu pinzani.

“Hizi timu aina ya Namungo ambazo dogo Mayele anaziletea dharau, huwa zinauma meno dhidi ya Azam FC kuliko dhidi ya timu nyingine yoyote ile.

Ndiyo maana ni rahisi sana mchezaji kutoka Azam FC akaenda kung’aa Yanga au Simba kuliko kinyume chake. Mfano, Novemba 27, 2022, Coastal Union walikuja Chamazi kucheza na Azam FC, wakitoka kupata alama mbili tu katika michezo yao mitano iliyopita.”

Zaka za Kazi alitolea mfano mchezo wao Azam fc dhidi ya Coastal Union ulivyokua msimu huu katika dimba la Chamanzi halafu wakaenda kupoteza kirahisi dhidi ya Simba.

Azam Fc dhidi ya Coastal Union katika Dimba la Chamanzi.

“Walifungwa mitatu na kutoka sare miwili. Katika mechi zote hizo, Coastal Union waicheza kama hawataki. Lakini siku ya kucheza na Azam FC ikawa tofauti. Kuanzia vyumba vya kubadilishia nguo wanahimizana, “leo hakuna kufungwa wana, tuwafunge hapa hapa kwao na basi lao”.

“Uwanjani ndiyo ikawa balaa. Unajiuliza, hivi wangecheza namna hii huko nyuma si wangekuwa mbali. Dakika ya 84, wakiwa nyuma 2-1, wakasawazisha…baada ya hapo wakawa hawataki kucheza tena…wanapoteza muda tu.

Dakika ya 87, kipa wao akaanguka kwamba kaumia. Akatibiwa hadi saa ikasoma dakika 90.
Refa akaongeza dakika 4 ambazo ziliisha wakati kipa amelala chini akitibiwa…akapona dakika 94, alitumia dakika 7 kutibiwa. Alipopona, kocha wao akafanya mabadiliko. Mchezaji aliyetakiwa kutoka, akagoma…akamtumia dakika tatu anafukuzwa kama mwizi uwanjani. Dakika zikapotea, jumlisha na zile nne zilizoongezwa.”

Moses Phiri akiliga mpira na kufunga mbele ya walinzi wa Coastal Union katika Dimba la Mkwakwani.

“Mchezo uliofuata baada ya huu walifungwa 3-0 na Simba nyumbani kwao Tanga. Bao la pili la Simba lilitokana na penati. Lakini kabla ya hapo, wao walistahili penati baada ya Onyango kumuangusha Majimengi ndani ya eneo la hatari…hawakuidai wala hawakulalamika, ilikuwa poa tu. Shida yao ilikuwa Azam FC na basi lao, siyo wengine”

Haya ndiyo maisha ya Azam FC dhidi ya hao akina Namungo unaowatolea mfano.
Maisha kama haya wewe dogo Mayele hujakutana nayo, kwa hiyo huwezi kuwaona akina Namungo wagumu, kama nitakavyofafanua kwenye posti inayofuata nikitumia mfano wa mechi zako dhidi ya hao hao Namungo,” alimalizia Zaka za Kazi msemaji wa Azam Fc

Sambaza....