Blog

Babu wa Mkude.

Sambaza....

NIMEMKUMBUKA Mzee Masharubu babu yake na kiungo wa Simba Jonas Mkude. Nyakati ziko wapi? Zimekwenda zake kama kipande cha barafu kilichoyeyushwa na ndoo ya maji.

Mzee Masharubu alikuwa shabiki na mwanachama kindakindaki wa Simba. Mbele ya nyumba yake kulikuwa na Tawi la Simba na yeye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Tawi lile.

Mjukuu wake Mkude anacheza soka na anaichezea Simba timu aipendayo babu yake. Mzee Masharubu ameagana na uso wa dunia. Mkude amepishana na babu yake. Mungu amuweke mahala pema peponi Mzee Masharubu.


D 🅾️ K E Z 🅾️ L 🅰️ Ⓜ️ K E Y E N G E


Kwa macho yangu kuna matukio mawili ya Mzee Masharubu nimeyaona juu ya Simba yake. Nilibaki kinywa wazi. Mosi aliletewa kreti la Soda alinywe na manazi wa Yanga baada ya Simba kulala katika mechi moja dhidi ya Yanga.

Tukio la pili niliona Mzee Masharubu akimwagika machozi ya furaha baada ya Simba kushinda dhidi ya Yanga. Mzee Masharubu alikuwa ‘ Mwehu ‘ linapokuja suala la Simba.

Mwisho wa kila kitu Mzee Masharubu alibaki kuwa mtu muungwana. Ni muungwana sana. Mara kadhaa nimewahi kuongozana na Jonas mpaka Kanisani na akatupa Pipi, Biskuti, Juice.

Juzi niliitazama mechi ya Tanzania Prisons na kijana wa zama zile za Mzee Masharubu ambaye sasa umri wake umesogea kidogo. Anaitwa Uncle Double. Huyu nae ni mnazi wa Simba. Aliruka ruka kwa furaha baada ya bao la Jonas.

Uncle Double alifurahia vitu viwili jioni ile ya Jumatano. Mosi, Simba kushinda. Pili bao kufunga Jonas mtoto wa nyumbani. Alipokaa chini baada ya kumaliza kushangilia akaniuliza ” Hivi Abdul ingekuwaje bao hili amelishuhudia na Mzee Masharubu” ? Nilibaki kutabasamu.

Swali la Uncle Double limenikumbusha matukio mengi ya Mzee Masharubu miaka mingi iliyopita. Namfahamu mzee yule sijui angeshikiwa wapi muda ule Jonas alipofunga bao. Sijui watu wangemshikia wapi.

Kivyovyote vile angetamba sana. Kwa nyodo na maneno yake ya shombo angepita nyumba moja hadi nyingine wanakoishi mashabiki wa Yanga kwenda kuwakoga.

Nilivyomtafuta Jonas baada ya mechi ile na kumuuliza hivi ingekuwaje bao lake angelishuhudia Mzee Masharubu katika kiti chake cha kamba? Jonas alibaki kucheka tu.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.