Sambaza....

“ Nimefurahishwa na kiwango cha wachezaji wangu, lakini kwa upande wa Simba ni kengele ya kuwaamsha hasa eneo lao la ulinzi, unajua leo hatukuwa wepesi katika matumizi ya nafasi za kupachika mabao, tungewafunga hata goli 3 “

“Bila shaka uliitazama Simba iliyocheza kule Zambia, na ndio maana nasema, inabidi waamke sasa, wanaenda katika hatua ya makundi, watakutana na waarabu, na kama watacheza vile, basi hawatofika mbali” Zeddy Saileti

Hayo ni maneno ya kocha mkuu wa Nkana Red Devils baada ya mchezo wao dhidi ya Simba jijini Dar Es Salaam baada ya kukubali kichapo cha goli 3-1, matokeo hayo yanaifanya Simba ifuzu katika raundi ya makundi kwa jumla ya magoli 4-3 dhidi ya Nkana.

Wawa (aliyeruka juu kulia), beki wa Simba akiwa katika majukumu yake

Kufuzu huko kunaifanya Simba SC iungane na timu zingine 15 zilizofuzu ikiwemo timu bingwa mtetezi, Esperance De Tunis na kuunda makundi manne, yatakayopatikana baada ya droo itakayofanyika desemba 28 siku ya ijumaa.

Kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka Afrika (Caf) juu ya uendeshaji wa mashindano ya klabu bingwa, katika Sehemu ya (iii) kifungu namba 16 kinataka timu zilizofuzu zigawanywe katika makundi manne, katika vyungu vinne vitakavyokuwa na timu nne kila kimoja, zenye kuleta jumla ya timu 16.

Katika sehemu hiyohiyo, kifungu namba 17, kinaelezea juu ya upangaji wa timu katika vyungu hivyo vinne. Upangaji utategemeana na alama zilizokusanywa na timu husika katika mechi ilizocheza katika mashindano yote yaliyo chini ya Shirikisho kwa kipindi cha miaka mitano. Timu zenye alama kubwa huwekwa katika chungu cha kwanza, zitaendea hivyo hadi chungu cha mwisho. Kwa mujibu wa kigezo hiki, Simba itakuwa katika chungu cha tatu.

Chungu cha kwanza kitakuwa na timu za TP Mazembe, Al-Ahly, Wydad Casablanca na Esperance De Tunis, Chungu cha pili kitakuwa na timu kama, Mamelodi Sundowns, AS Vita Club, Horoya na Club African, chungu cha tatu kitawabeba ASEC Mimosas, Orlando Pirates, Simba SC na Constantine na chungu cha nne kitakuwa na timu kama Ismaily, Lobi Stars, FC Platinum na JS Saoura.

Jeremy Brockie wa Mamelodi Sundowns

Kila chungu kitatoa timu moja, kwa kila kundi , hii ina maana kuwa timu zinazopatikana katika chungu kimoja haziwezi kukutana. Usitarajie Simba kukutana na timu kama ASEC Mimosas,Orlando Pirates na Constantine, lakini inaweza kupangwa kundi moja kati ya hizo zote zilizobaki nje ya chungu cha tatu.

Hii ina maana kuwa, Simba itacheza mechi 6, tatu za nyumbani na tatu za ugenini. Michezo ya kwanza ya makundi inatarajiwa kuchezwa januari 11 hadi 13, mechi za pili januari 18 hadi 20, mechi za tatu zitachezwa februari 1 hadi 3, mechi za nne ni Februari 12 hadi 13, mechi za tano ni machi 8 hadi 11 na mechi za mwisho zitachezwa machi 15 hadi 18.

Kwa mujibu ya Sehemu ya III, kifungu namba 18 cha sheria za uendeshaji wa klabu bingwa barani Afrika, inazitaka timu zilizofuzu katika hatua ya makundi kuwa na muwakilishi wakati wa uendeshaji wa droo ya makundi. Kwa upande wao Simba watawakilishwa na mwenyekiti wa bodi Swedi Kwambi.

TP Mazembe

Hadi mashindano haya yanafika katika hatua hii, tunamshuhudia Moataz Al-Mendi wa Al-Nasr ya Libya akiongoza kwa kupachika magoli 7 hadi sasa huku timu yake ikitolewa na Horoya ya Guinea kwa jumla ya mabao 5-6, Clatus Chama wa Simba akishika nafasi ya pili akiwa na magoli 4, Sikiru Alimi wa Lobi Stars naye akiwa na magoli 4, Jeremy Brockie, Meddie Kagere , Mamadou Sidibe na John Bokko wote wakiwa na magoli 3.

Hadi sasa hivi Simba imefunga jumla ya magoli 12, na ikifungwa magoli 4 ikiwa ni tofauti ya magoli 8. Katika michezo yote waliyocheza katika hatua ya mtoano hadi kufuzu, washambuliaji wa timu pinzani walionekana kukosa umakini wa kufunga kutokana na makosa mengi yaliyotengenezwa na beki ya Simba, ikiongozwa na Mohamed Hussein, Erasto Nyoni, Paschal Wawa na Nicolus Gyan.

Bolaji Sakin, Horoya

Udhaifu wa beki ya Simba umeonekana ndio kikwazo kikubwa kwa Klabu kusonga mbele, kuelekea robo fainali. Miongoni mwa watu walioishauri Simba juu ya kufanyia kazi eneo lao la ulinzi ukiachana na kocha wa Nkana, ni kocha na mchezaji wa zamani wa wekundu hao, Abdallah Kibadeni Mputa. “king”
“……. Simba imeonekana kutokuwa vizuri katika eneo la ulinzi, naamini mwalimu atalifanyia kazi hasa eneo hilo….. marekebisho katika eneo hilo yatafanywa na mechi za ligi watakazocheza na mashindano mengine…. “

Hivi ni nani asiyejua kwamba, hatua waliyoifikia Simba ni ngumu? Bila shaka watafanya mabadiliko makubwa katika safu yao ya ulinzi ambayo kwa sasa ina sifa nyingi ikiwemo kukaba kwa macho, hakuna kiongozi katika safu nzima ya ulinzi, uwezo mdogo wa kuziba mapengo na kuzuia pasi mpenyezo, mabeki wazito, uzembe katika kuokoa mipira na ukabaji “tight marking” haya yote yasiporekebishwa hasa kupitia mazoezi na mechi watakazocheza za ligi na kombe la TFF, zitawafanya wafanye marekebisho makubwa katika kikosi.

Sitarajii kumuona Kocha Patrick Aussem akianzisha wachezaji ambao huwa hawapati nafasi katika mechi za ligi na mashindano mengine kwa sababu atahitaji kufanya marekebisho ya kikosi chake hasa eneo la ulinzi, natarajia eneo hilo litakuwa na maingizo mbalimbali ili kuunda muunganiko kati ya wachezaji. Mfano muunganiko wa Juuko na Wawa, au muunganiko wa Juuko na Erasto na hata mabeki wa pembeni, Zimbwe dhidi ya Asante Kwasi, na Zana Coulibaly dhidi ya Nicolus Gyan.

Sambaza....