Sambaza....

Kocha wa makipa wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar Patrick Mwangata ameeleza kwamba wanaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wa hatua  ya kwanza ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya KCCA ya Uganda Disemba 15 mwakahuu.

Mwangata amesema wameshaanza mazoezi kwa siku ya nne sasa nawanacholenga kwa sasa ni kufanya mazoezi ya kuangalia namna ya kushinda mchezo wa ugenini kwani wanafahamu ugumu wa kucheza ugenini kwa timu kama Mtibwa ambayo haijacheza kwa muda mrefu mashindano kama hayo.

“Maandalizi yapo vizuri, tushaanza maandalizi takribani tunasiku ya nne sasa hivi, maandalizi yanakwenda vizuri tunashukuru Mwenyezi Mungu tupo sawa wote……tunajipanga kwenda kucheza ugenini, kama unavyojua mechi za ugenini zina mipango yake kwa hiyo tunajipanga kwa hilo na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutakipata tunachokitaka,” amesema.

Mwangata ameendelea kufunguka kuwa hakuna mchezaji aliyekuwa na majeraha mpaka sasa na kwamba wanajua ugumu wa wapinzani wao wanaokwenda kukutana nao licha ya kukiri kuwa bado hawafahamu sana namna ya uchezaji wao kwa maana ya udhaifu na ubora wao ulipo.

“Baada ya kupangiwa nao tulianza kuwafuatilia, tuliwaona ni timu nzuri ambayo inaweza kuleta upinzani, lakini naamini sisi tutakuwa timu nzuri zaidi na kuweza kusonga mbele, muhimu watanzania watuombee, tunakwenda kupambana tupate matokeo mazuri,” amesema.

Mechi hiyo itafanyika kwenye uwanja wa Phillip Omondi Disemba 15 kabla ya kurudiana Disemba 21 kwenye uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Mtibwa Sugar imefanikiwa kufika hatua hiyo baada ya kuiondoa Northern Dynamo ya Ushelisheli kwa jumla ya mabao 5-0, na kama watafanikiwa kuiondoa KCCA watavuka raundi ya pili ambapo watakutana na timu washindwa kutoka Klabu Bingwa Afrika.

Sambaza....