Sambaza....

Baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa goli 1-0 ikiwa nyumbani dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki,timu ya Boma FC ya wilayani Kyela mkoani Mbeya inayoshiriki ligi daraja la kwanza imesema imejipanga kuchukua pointi tatu kwa kila michezo iliyosalia.

Boma FC iliyopo kundi B katika ligi daraja la kwanza inashika nafasi ya pili ikiwa na jumla ya alama 21 nyuma ya vinara Geita wenye alama 23 ambapo kwa michezo iliyocheza nyumbani haijafungwa bali ilitoka sare ya 0-0 na Geita na goli 1-1 na Rhino FC ya Tabora.

Akizungumza na mwandishi wa habari jana, Afisa habari wa Boma FC, Aidan Mwasampeta amesema baada ya mchezo na Polisi wachezaji walipewa mapumziko ya siku moja na juzi wameanza mazoezi ya asubuhi na jioni kwaajili ya kujiandaa na mchezo wa Kombe la FA utakaocheza Dar es salaam dhidi ya Reha FC inayoshiriki pia ligi daraja la kwanza.

Mwasampeta amesema kikosi hicho kilitarajia kuanza safari leo kuelekea Dar es salaam lakini kutokana na sababu mbalimbali kitaanza safari kesho(Jan 23) kwaajili ya mchezo na Reha na baada ya hapo watarejea Kyela kwaajili ya maandalizi ya michezo ya Ligi daraja la kwanza dhidi ya Trans Camp na Arusha United.

Mwasampeta amesema wamejipanga kuhakikisha michezo yote ya nyumbani wanaibuka na ushindi na kama itatokea kupoteza basi iwe ni kwa kutoka suluhu.

Aidha alisema kama timu wanampongeza sana mbunge wa Kyela Dk Harison Mwakyembe kwakuwapa hamasa kwani katika mchezo wa juzi aliahidi na akatoa pea ya viatu vya kuchezea kwa kila mchezaji na vocha kwaajili ya mawasiliano.

Amesema kwenye mchezo wanaokweenda kucheza Dar es salaam wa FA pia amewaahidi watavaa jezi mpya zitakazokuwa na majina ya wachezaji jambo alilosema kwao ni hamasa kubwa.

Sambaza....