BlogSerie A

Gonzalo Higuain aomba radhi.

Sambaza....

Mshambuliaji wa AC Milan Gonzalo Huguain amewaomba radhi mashabiki wa klabu hiyo kwa kitendo chake cha kukosa penati lakini pia kupata kadi nyekundu ya kizembe wakati timu yake ikiadhibiwa mabao 2-0 na Juventus katika mchezo wa Seria A jana Jumapili.

Gonzalo ambaye alipata nafasi ya kuisawazishia timu yake kwa njia ya penati baada ya beki Medhi Benatia kuunawa mpira ndani ya 18 lakini akapiga pigo dhaifu amewaomba radhi mashabiki lakini pia refa wa mchezo huo Paolo Silvio Mazzoleni kwa kitendo ambacho alikifanya.

“Kwanza kabisa ningependa kuwaomba radhi wenzangu, kocha, mashabiki na refa wa mchezo kwa kitendo nilichofanya, ningependa kubeba lawana zote kwa chochote ambacho kimetokea, naamini hakitajirudia tena, ni miongoni mwa matukio ambayo yanatokea, … tulikuwa tumeshapoteza, nikakosa penati, sitaki kujitetea sana lakini,” mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid na Napoli amesema.

Gonzalo aliwahi pia kuichezea Juventus kabla ya kutolewa kwa mkopo wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kununuliwa moja kwa moja baada ya Juventus kumsajili Cristiano Ronaldo, ambapo alifanikiwa kufunga mabao 55 katika michezo 105 aliyocheza.

“Kwa sasa nipo AC Milan, nina furaha hapa, mimi ni mchezaji mwenye hisia kali, hivyo wakati mwingine nashindwa kujizuia, unaweza kuniona wazi katika sura yangu kama najisikia furaha au laa, lakini sisi ni mfano kwa watoto najua nilichokifanya sio mfano mzuri,” Gonzalo amesema.

“Niliwacharukia hata wachezaji niliowahi kucheza nao (wa Juventus) lakini walinituliza, wanajua wachezaji wanahisia kali, mchezo huo hakuwa mzuri na kwangu ilikuwa siku mbaya zaidi naomba radhi kwa wote,” Gonzalo akiwashuruku wachezaji wa Juventus ambao walijaribu kumtuliza.

Katika mchezo huo Juventus walipata mabao mawili kupitia kwa Mario Mandzukic na Cristiano Ronaldo na kuifanya AC Milan kusalia na alama 21 katika nafasi ya tano huku Juventus wakifikisha alama 34 katika nafasi ya kwanza.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.