Ligi Kuu

Hivi Messi alikuwa mzito kwenye miguu ya Singano?

Sambaza....

Ramadhani Singano “Messi”, ndivyo tulivyoamua kumbatiza hilo jina baada ya kuhadaika na mguu wake wa kushoto.

Mguu ambao alikuwa akiutumia vizuri kukokota mipira na kupiga vyenga ambavyo viliwafanya mashabiki kutoa tabasamu.

Tabasamu ambalo lilikuja na ubatizo mkubwa kwa Ramadhani Singano, jina lake lilionekana halifai tena kutumika, Messi akawa mtu sahihi kumweka kwenye miguu ya Ramadhani Singano.

Singano alibeba jina la Messi kwa matumizi ya guu la kushoto

Imani ilikuwa kubwa kwake, mategemeo yakawa makubwa pia , wengi tukawa tunategemea kitu kikubwa kutoka kwa Ramadhani Singano “Messi”.

Kwenye ile orodha ya kupanda ndege tukawa tumemweka tukiamini kabisa yeye ndiye atakayefuata baada ya Mbwana Samatta.

Tulitamani afike mbali kwa sababu ya kipaji chake kikubwa, kipaji ambacho kilikuwa hakitakiwi kucheza mpira wa Tanzania kwa muda mrefu.

Lakini kwa sasa imekuwa tofauti, Ramadhani Singano “Messi” bado yupo Tanzania.

Tena akiwa hana uhakika wa namba kwenye timu anayocheza kwa sasa (Azam FC)

Huwa inaumiza kipindi ambacho kipaji kikubwa kama cha Ramadhani Singano “Messi” kikipotea bila msaada mkubwa kwenye Taifa.

Kipaji ambacho ƙkingekuwa chachu kwa vijana wengine kupigana zaidi ili waende kucheza nje, lakini imekuwa tofauti kabisa, kwa sasa benchi la Azam Fc limekuwa sehemu sahihi kwake yeye.

Na anavyoonekana hakuna jitihada zozote kwake yeye binafsi anazozifanya kupigana ili asiendelee kukaa kwenye benchi la Azam FC.

Kushindwa kwake kumshawishi kocha kunampa maisha yenye urefu wa maisha ya funza pale Azam FC, ndipo hapo ndoto yake itakuwa imeingia kwenye giza totoro.

Itakuwa kazi ƙkubwa kwake yeye kutafuta mwanga wa kupigana na giza hilo totoro kipindi ambacho atakuwa ameenda Njombe mji.

Sehemu ambayo hakuna huduma za muhimu na msingi kama Azam FC, sehemu ambayo hakuna mechi za kimataifa za kujitangaza kama Azam FC.

Ndipo hapo mwanzo wa kumpoteza Ramadhani Singano “Messi” utakavyoanza.

Kuna kitu kikubwa sana ambacho mpira wetu unakosa nacho ni wasimamizi wa wachezaji (Managers)

Hatuna wasimamizi bora wa hawa wachezaji, wasimamizi ambao watawasimamia wachezaji katika misingi ya soka la kisasa.

Wasimamizi ambao watasimamia ratiba binafsi za mazoezi ya mchezaji, kumkumbusha wakati gani anafaa kufanya mazoezi gani binafsi tofauti na ya timu.

Wasimamizi ambao watawakumbusha muda sahihi wa kupumzika baada ya kumaliza mazoezi.

Wasimamizi ambao watawakumbusha kula mlo gani kulingana na ushauri wa wataalamu wa wanaohusika na vyakula vya wanamichezo.

Wasimamizi ambao watapata muda na kuwashauri wachezaji kipi sahihi ambacho mchezaji anatakiwa kufanya kwa manufaa ya kipaji chake, ƙkipi ambacho siyo sahihi mchezaji kukifanya, ambacho kinaweza kuharibu ndoto za mchezaji huyo.

Wachezaji wetu wametokea kwenye mfumo ambao siyo mfumo wa mpira wa kisasa, hivo ni rahisi kwao wao kupotea kama wakikosa msimamizi ambaye anaweza kuwasimamia katika njia sahihi.

Wengi wanapotea kwa kukutana na washauri ambao hawawezi kuwapa ushauri ambao unaweza kuishi milele kwenye maisha yao ya mpira.

Wasimamizi ambao watasimamia shughuli za nje ya uwanja za mchezaji kama kupata ubalozi wa kibiashara na kampuni mbalimbali za kibiashara ili mchezaji anufaike kulingana na kipaji chake

Hapa ndipo Ramadhani Singano “Messi” alikosea ndiyo maana kwa sasa ukungu mzito umetanda kwenye mboni za macho yake, kibaya zaidi jua linashazama

Na kibaya zaidi kwa wakati huu inaonekana hakuna mtu anayenshauri namna ya yeye kujaribu kurudi katika kiwango chake.

Mwili wake unaonesha kabisa amekosa kujiamini ndani yake, na hakuna tena mtu wa kumwingizia sumu ya kujiamini ndani ya miguu yake ili angalau arudi sehemu ambayo tuliyomzoea.

Mimi bado naamini kupitia miguu ya Ramadhani Singano “Messi”, cha muhimu ni yeye kuongeza jitihada binafsi za kuweza kumrudisha sehemu aliyokuwa awali, hapo alipo kwa sasa hakumpi nafasi ya kusogea mbele, jina la Messi lilikuwa zito sana kwake ni wakati sahihi wa kulivua na kumtengeneza Ramadhani Singano maana kumtengeneza Messi kwenye miguu ya Ramadhani Singano imeshindikana.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x