Mabingwa Afrika

Hofu yangu kwa Simba ni sehemu 4 pekee, Hizi hapa.

Sambaza kwa marafiki....

Haya! haya! Haya!, kumekucha Afrika Mashariki, kumekucha Tanzania, kumekucha uwanja wa taifa, kumekucha kwa Mkapa!. Ni Simba SC dhidi ya AS Club Vita kutoka Congo, Kinshasa.
Msimamo wa kundi D, uko hivi, AS Vita ina alama 8, Al-Ahly 7, JS saoura 7na Simba SC ina alama 6. Mechi za mwisho ni Al-Ahly vs Saoura na Simba vs AS Club Vita (Pomboo Weusi).

Mechi ya Al-Ahly na JS Saoura, Ahly atakuwa nyumbani anahitaji ushindi au sare ya kutofungana, JS saoura naye anahitaji ushindi au sare ya kufungana kuanzia goli mbili. Hii ni kutokana na sare ya mechi ya kwanza nyumbani kwa Saoura ya 1-1.

#TimuPWDLFAGDPts
1Al Ahly6312113810
2Simba SC6303613-79
3JS Saoura622269-38
4AS V.Club62139727

Mechi ya Simba dhidi ya AS Vita, Simba nahitaji KUSHINDA PEKEE, yaani hapa hakuna uwezekano mwingine, matokeo mengine yote kinyume na ushindi ni kushindwa kufuzu roba fainali. AS Vita yeye anahitaji sare tu, tena ya aina yoyote. Hii itamfanya afikishe alama 9.
Matokeo ya Mwisho yanaweza yakamvusha Al-Ahly na Vita au Al-Ahly na Simba. Saoura kupata ushindi ugenini ni kazi ngumu sana, yaani njia yake ni nyembamba mno. Na kama atapata ushindi ugenini basi atafuzu yeye, na mwingine kutoka mechi ya Dar es salaam.

“Simba ni Simba tu, hata akilowa hawezi geuka na kuwa paka, nyumbani hatoki mtu, iwe kwa mvua ama jua, heri kufia uwanjani kuliko kurudi nyumbani bila alama tatu”

Hayo ni maneno ya jamaa mmoja hata simfahamu lakini tumekutana kwenye banda umiza baada ya Simba kukubali kichapo cha goli 2-0 mbele ya JS Saoura. Maneno yake siyatilii maanani lakini najua ni zile amsha amsha na hamasa za kuujaza uwanja wa taifa.

Silaha kuu ya Simba katika michuano ya kimataifa, kwa uwanja wa nyumbani inaonekana ni kuujaza uwanja tu. Na nikweli uwanja huwa unajaa lakini cha ajabu, amsha amsha (vibe) za uwanjani haziendani na idadi ya watu iliyopo. Maana yake kuna mashabiki huingia uwanjani kama watalii tu, kushangilia haiwahusu.

Na hii ndio hofu yangu ya kwanza, huenda Mashabiki wakajaa lakini wasilete hamasa inayokadiliwa kwa wachezaji kujituma zaidi. Imekuwa ni mazoea sasa kwa mashabiki kugeuka watalii uwanjani. Asilimia 45 tu kati ya 100 huenda ndio hushangilia wengine wotee kimyaa, hadi goli lifungwe.
Hiki kinaweza kikawa kikwazo cha kwanza kwa Simba inayotegemea mashabiki kama nyenzo muhimu ya ushindi katika uwanja wa nyumbani.
Pili, Eneo la kiungo. Eneo hili ni muhimu sana kwa ushindi wa Simba. Hili ndilo eneo nyeti kwa timu ya Simba kwa sasa. Ushindi wa Simba katika michuano ya ndani na hata ya kimataifa ni kutokana na kucheza vizuri kwa eneo hili.
Eneo la kiungo ni daraja la kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji.

Kushindwa kucheza vizuri kutafanya maeneo yote kulegea. James Kotei ndiye anayeonekana kuwa na muendelezo mzuri na kutimiza majukumu yake kama inavyotakiwa.

Kotei anakaba vizuri, kwa kasi, nguvu, haruhusu mpira upite mbele yake, ni mzuri akiwa hana mpira. Mkude ni mzuri akiwa na mpira, anahakikisha haupotezi, hutumia nguvu zake za miguu kuulinda. Tatizo lake moja, yuko taratibu mno.

Clatus Chama ni mzuri akiwa na mpira pia hata akiwa hana mpira. Anakaba, anapiga pasi za mwisho, anapiga pasi muhimu (key passes), anajua kuingia kwenye eneo la hatari, anajua kufunga pia. Naye tatizo lake yuko taratibu sana. Na muda mwingine huchezea chini sana kiasi cha timu nzima kucheza kama inajilinda.

Kutokana na aina ya uchezaji wa AS Club Vita, viungo ndio watakao kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanapandisha timu haraka haraka. Aina ya mashambulizi yawe ya haraka kuliko kawaida, yaani sekunde chache zitumike kutoa mpira kutoka kwa mabeki hadi kwa washambuliaji.Sehemu hii ikitawaliwa vizuri, Simba watapata matokeo.

Wawa

Tatu, ni safu ya ulinzi. Safu ya ulinzi inaonekana kuwa na mapengo mengi. Hasa beki ya kati, Paschal Wawa amekuwa ni injini sasa. Hubadilishiwa watu wa kucheza nae tu lakini pacha inayoeleweka bado haipo. Wawa vs Paul Bukaba wanaonekana kwenda sawa isipokuwa makosa ya utulivu wakati wa ukabaji bado yanawagharimu.

Tumemuona Bukaba akisababisha penati dhidi ya JS Saoura, tumemuona pia Wawa akisababisha penati dhidi ya A Club Vita. Utulivu wakati wa kumkaba mshambuliaji mwenye kasi unakuwa mdogo, na hii huwatofautisha wao na Erasto Nyoni, ambaye hutumia akili nyingi ku-win mpira kuliko nguvu.

Mabeki wa pembeni, Zana Coulibaly na Mohammed Hussein wameonekana kufanya kazi nzuri. Zimbwe ameonekana kucheza vizuri zaidi katika nafasi yake, na kwa sasa kuna kitu ameimarika zaidi, kilichokuwa kinamuweka benchi kipindi cha nyuma.
Zimbwe anaokoa mipira mingi katika eneo la kati. Yaani anatoka kushoto anakuja kuokoa mipira inayopaswa kuokolewa na beki wa kati. Maana yake ameimarika vyema katika somo la “Recovery system”, analitimiza vyema. Zana mzuri akiwa anashambulia, lakini tatizo la uzito bado ni kubwa. Ni mzito sana wa kurudi haraka baada ya kushambulia.

Zana

Nne, ni “game plan”. Hapa sasa ni kazi ya Patrick Aussems kufanya kazi yake, kujipambanua kwa wadau wa soka duniani kuwa yeye ni kocha anayezijua mbinu za mpira( master of tactics)., Mechi za nyumbani kanuni ni moja tu, nayo ni kushambulia kwa kasi, na kukaba kwa kasi. Vyote vimaanishe KASI.
AS Club Vita, ina wachezaji wazuri sana, ni watulivu wakiwa na mpira, wana kasi kubwa wakivuka nusu ya eneo lao, hutumia mipira mirefu, hushambulia kupitia pembeni. Kwa kuwa watakuwa ugenini na wanatafuta sare lazima hawatowekeza kushambulia badala yake watajilinda na kushambulia kwa kushtukiza na kujaribu kutumia nafasi chache watakazozipata.

Aussems yeye lazima ashambulie kwa kasi, asiwaruhusu wamiliki mpira kwa dakika tano, kila mchezaji awe mwepesi wa kutoa pasi na kukaba. Endapo Okwi atakuwa vizuri huenda mipango ya Aussems itakaa poa zaidi.
Ujio wa Okwi utamfanya Chama kucheza eneo lake kama kiungo mshambuliaji. Okwi atacheza eneo moja kati ya winga ya kulia au kushoto, kasi yake itarahisisha kazi.

Okwi

Umakini unahitajika sana kwa kila mchezaji hasa katika kufanya “marking”. Magoli waliyofungwa Simba ugenini kule Kinshasa ni uzembe katika Marking. Simba hawana “ man to man marking” wakati wa upigaji kona, hii hurahisisha timu pinzani kufanya “ zig-zag movement” na kuwafunga magoli ya vichwa.

Ushindi ni lazima! Lakini kila mtu katika nafasi yake lazima atimize majukumu yake. Mashabiki waende wakashangilie kwa nguvu katika dakika zote tisini, wachezaji lazima wacheze kwa jihad, wawe mfano wa Mbwa Mwitu wanapokuwa hawana umiliki wa mpira.
Kocha Aussems lazima ahakikishe, timu yake inaingia ikiwa na morali ya hali ya juu, lazima ahakikishe kila mchezaji anatimiza majukumu anayompa kwa asilimia kubwa. Bila shaka atakuwa ameisoma Vita kwa muda mrefu na atakuja na dawa yao. Kila la heri, klabu ya Simba., Mungu ibariki Tanzania.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.