Sambaza....

Unaikumbuka ile Yanga ya Mwinyi Zahera?, ile ambayo ilikuwa na nje ya uwanja na njaa ndani ya uwanja?, ile Yanga ambayo ilikuwa inatafuta chakula kwa nguvu zote ?.

Ile Yanga ambayo ilikuwa inaoenakana goigoi lakini ikiingia uwanjani ilikuwa inaonekana imara , tena imara sana?

Ile Yanga ambayo wachezaji wake walikuwa wanaonekana na moyo wa kupigana kwa muda mrefu ndani ya uwanja?.

Ndiyo, naizungumzia Yanga ile ambayo ilienda michezo 18 bila kufungwa, Yanga ambayo ilikuwa mbali na joto la kufungwa.

Walikuwa wanaishi kwenye nchi ya ushindi tu. Nchi ambayo wengi huitamani kuishi lakini siyo jambo jepesi kuifikia.

Lakini Mwinyi Zahera alifanikisha kwenye hili. Aliipeleka Yanga kwenye nchi hii, Yanga ikawa inapata sana ushindi. Ikawa inawapa mashabiki wake ushindi kila uchwao.

Neno “kipigo” lilikuwa mbali sana na masikio yao, unajua kwanini Mwinyi Zahera alifanikisha kwenye hili?

Jibu ni moja tu, aliwekeza hali ya kupigana kwenye timu. Timu ilikuwa na mpaka sasa hivi ipo kwenye kipindi kigumu kiuchumi.

Kipindi ambacho ni ngumu sana kwa timu kuweza kupata matokeo kwa sababu tu wachezaji kukosa “motisha” ndani ya uwanja.

Unaweza ukawa na kikosi kipana chenye wachezaji wenye vipaji vikubwa lakini wakakosa kitu kimoja tu, nacho ni “motisha”.

Hiki kitu ni kikubwa sana, ni kitu ambacho huongeza nguvu ya ajabu kwenye timu. Nguvu ambayo humfanya yule mdogo kuonekana wa hatari.

Unaweza ukawa na timu yenye wachezaji wa kawaida sana!, lakini ukawaunganisha hawa wachezaji na ukawaida wao kwa kuweka tu ” motisha”.

Matokeo ambayo unaweza ukayapata yatawashangaza wengi sana. Turudi kwa Yanga sasa. Yanga ilikuwa inakosa “Motisha” kwa sababu tu ya hali mbaya ya uchumi.

Ni ngumu kwa mchezaji kucheza katika kiwango cha juu kabisa wakati ambao timu ina njaa ya pesa. Ni ngumu sana , tena sana kwa mchezaji ambaye ana familia.

Kwa mchezaji ambaye anawaona wapinzani wake wakibadili magari kila Siku, wakiishi kwenye nyumba bora na nzuri na wakati mwingine wakiwa na wanawake wazuri kuzidi wa kwao.

Hiki huwa ni kipindi kigumu sana kwa mchezaji kucheza na kufanikisha kuiwezesha timu husika kupata matokeo ambayo ni chanya.

Ndicho kipindi ambacho Mwinyi Zahera alikutana nacho akiwa Yanga. Hakutaka kukimbia hali halisi ya timu, alikubaliana na hali halisi ya klabu.

Hakuikimbia kabisa Yanga alichokifanya ni kukimbia nayo na magumu yote. Alikaa na wachezaji akawaambia umuhimu wa kujitoa katika hali ngumu yoyote ndani ya klabu.

Aliwaambia umuhimu wa kupigana kwa ajili ya vipaji vyao. Aliwaaaminisha kuwa bila kupigana vipaji vyao havitafika mbali .

Ndipo hapo ukawa mwanzo wa wachezaji wa Yanga kupigana kwa nguvu sana , walikuwa na hamasa kubwa ndani ya timu.

Hamasa hii ilitokana na kocha wao Mwinyi Zahera kuwaaminisha umuhimu mkubwa wa kupigania vipaji vyao.

Yanga ikawa inafanya vizuri. Lakini kwa sasa tangu wafungwe na Stand United walikuwa wanaonekana ile hamasa yao imepungua sana.

Sambaza....