Blog

Immobile: Chuma chakavu kilichogeuka dhahabu jioni!

Sambaza....

Chukua dakika moja ya heshima kwa akademi ya Sorrento mwaka 2002 mpaka 2008, pia waombee heri viongozi wa akademi ya Juventus mwaka 2008 mpaka 2009 kisha vuta pumzi rudi kitini keti huku ukisoma makala hii ya mfumania nyavu Ciro Immobile.

Usiwasahau Siena, Grosseto wala Pescara walioishi nae kwa mkopo kabla ya kumuuza kwa Genoa alipodumu kwa msimu mmoja. Wakumbuke pia Torino wale walioishi nae kabla ya mwaka 2014/15 alipojiunga na Borussia Dotmund.

Huo ulikua muda wa mpito kwake kwani msimu uliofuata alipelekwa kwa mkopo Sevilla kisha Torino tena, ambapo Lazio walimuona wakasema kijana huyu anatufaa na kumsajili mnamo mwaka 2016.

Cirlo Immobile

Akiwa ameshacheza mechi kadhaa za timu ya Taifa la Italia kuanzia kwa vijana hadi wakubwa, lakini kwa klabu mambo yalikua bado apeche alolo kwa mzaliwa huyo wa Torre Annunziata pale Italy.

Hakuna dhahabu bora ambayo haijapitia moto, basi huyo ndiye Immobile, chuma chakavu kinachong’aa kwa sasa Duniani wakati jua kwake linaelekea kuzama.

Akiwa na miaka 30 kwa msimu huu ameweza kufumania nyavu mara 35, zaidi ya mchezaji yeyote yule unaemfahamu wewe katika ligi kubwa tano Barani Ulaya. Si Ronaldo wa Juventus wala Lewandowski wa Munich, wote wapo chini yake huyu mzee kijana wa Lazio.

Kuna muda unajiuliza kwanini ubora huu kauonesha wakati ambao Dunia inataka damu changa kuliko yeye mwenye miaka 30 unakosa majibu.  Hii inatufundisha kuwa Riziki Mafungu Saba na Mungu hugawa kwa wakati, pia unapewa unachostahili sio unachotaka.

Na Yeye aliyejuu kaona huu ndio muda mwafaka wa Ciro kupata mabao na ukubwa huu sisi ni nani tupinge?

Sambaza....