Blog

Inawezekana Rage aliwaambia Yanga “Umbumbumbu”?

Sambaza....

Tuanzie hapa, Ismael Aden Rage aliwahi kuwaita mashabiki wa Simba kuwa ni mashabiki mbumbumbu wakati akiwa mwenyekiti wa klabu hiyo ya Simba. Sitaki kuiongelea hii kauli , sitaki kuifikiria sana hii kauli kwanini aliitoa kwa mashabiki wa Simba na sijawahi hata siku moja kuitilia maanani kwenye akili yangu.

Lakini juzi jumamosi hii kauli ilikuwa inapita sana kwenye akili yangu. Nilijitahidi sana kuizuia na kutoipa nafasi kubwa kwenye akili yangu. Lakini mwisho wa siku niliamua kukaa chini na kutafakari hii kauli mzee wangu Ismael Aden Rage aliitoa kwa mashabiki wa Simba au wa Yanga?

Aden Rage

Kumbukumbu zangu za awali zilikuwa zinaonesha kuwa aliitoa hii kauli kwa mashabiki wa Simba na siyo Yanga. Niliwatazama sana mashabiki wa Simba. Simba ipi ?, Simba hii ambayo mashabiki wake huwa wanajali aina ya uchezaji wa timu (style of play ) kutunzwa kuliko kitu kingine ?

 

Unamkumbuka Moses Basena?, Mganda ambaye aliwahi kupita katika klabu ya Simba?. Mganda ambaye alikuwa anaiwezesha Simba kupata matokeo chini ya aina ya uchezaji ambao hauvutii kwenye macho ?

Yani timu itapata ushindi wa goli 3-0, au ushindi wa goli 2-0 lakini chini ya aina ya mpira ambao hauvutii kuangaliwa. Lakini pamoja na kwamba Simba ilikuwa inapata matokeo, mashabiki wa Simba hawakuridhika na matokeo hayo chanya.

Walipata matokeo Chanya ndiyo, lakini chini ya aina gani ya mchezo? Hili swali lilikuwa kubwa sana kwao na ndilo swali ambalo liliwasababisha wao kupanua vinywa vyao na kuongea kauli moja tu, tunataka ushindi chini ya aina ya mpira wa kuvutia.

Haya ndiyo mahitaji Simba kila mwaka, Simba inahitaji hiki. Timu kushinda huku mpira ukiwa unaonekana umepigwa haswaaa. Hiki ndicho ambacho huwa kinafukuzisha makocha wengi, hata Pierre Lenchantre alifukuzwa kwa sababu ya hiki.

Hakuwa kocha mbaya, La hasha. Alikuwa kocha mzuri ambaye hakuendana na mahitaji ya klabu ya Simba. Alikuwa anashinda chini ya aina ya mchezo ambao hauvutii. Mashabiki wa Simba walipaza sauti zao. Pierre Lenchantre akaondoka na leo hii yuko Patrick Aussems ambaye anafanya kile ambacho Simba inataka miaka yote.

Kucheza soka la kuvutia na matokeo yakiwa yameonekana. Hiki ndicho ambacho kinaonesha mahitaji sahihi ya Simba. Na hiki ndicho ambacho mashabiki wa Simba huwa wanakipigania sana. Nilichofikiria hiki nilisita kidogo.

Nikafikiria Ismael Aden Rage alikuwa anawaambia mashabiki wa Yanga au Simba kuwa ni mbumbumbu ?

Mbona kama alikuwa anawaambia mashabiki wa Simba , mbona hawafananii kabisa na umbumbumbu ?

Mbona wanajua wanachokifanya hata kama kwa asilimia ndogo lakini inatosha kuonesha kuwa wanajua mahitaji yao ?

Mashabiki wa Yanga kwenye mechi ya Simba vs JS Saoura

Vipi mashabiki wa Yanga hili jina la umbumbu haliwafai wao kwa kiasi kikubwa? Na inawezekana Ismael Aden Rage alikuwa anawaambia mashabiki wa Yanga tu kupitia mgongo wa mashabiki wa Simba ?

Kwanini najiuliza haya maswali yote ndugu zangu ?. Jibu ni moja tu. Ni aina ambavyo kocha Mwinyi Zahera anavyowafanya mashabiki wa Yanga kuonekana ma Mbumbumbu.

Na Yanga wameridhika kabisa kuwa hivo kuanzia kwa viongozi wa Yanga, mashabiki wa Yanga, sijui sana kuhusiana na wachezaji.

Kwanini nasema hivo ?, kocha Mwinyi Zahera kuna vitu vingi huvifanya ambavyo haviko katika mipaka yake. Ni rahisi sana kwa Mwinyi Zahera kuvuka mipaka yake na mashabiki mpaka viongozi wa Yanga kuishia kutabasamu tu.

Zahera

Nakupa mfano mdogo tu, unakumbuka Mwinyi Zahera alianzisha zoezi la mashabiki wa Yanga kuichangia timu yao ? Hivi unafikiri mipaka ya Mwinyi Zahera ni ipi? , mipaka ya Mwinyi Zahera si inaishia kwenye mambo ya kiufundi na siyo mambo ya kiutawala ?

Kama mipaka yake inaishia kwenye mambo ya kiufundi na siyo kiutawala kwanini anafanya shughuli zote za kiufundi na zi kiutawala?

Kwanini anaingilia mipaka majukumu ambayo viongozi wa Yanga walitakiwa kuyafanya ila yeye ameamua kuyafanya yeye kwa mikono yake ?

Kwanini kama anawazo jema na bora asilifikishe kwenye uongozi wa klabu na uongozi wa klabu ukae kupitia kamati tendaji na kupitisha uamuzi wa utekelezaji kuliko yeye kuamua moja kwa moja kulibeba na kulitekeleza yeye.

Yani yeye ndiye mwenyekiti, katibu , kamati kuu tendaji ya Yanga na ndiye kocha wa Yanga. Yote haya anayafanya mbele ya mashabiki wa Yanga na viongozi wa Yanga bila hata uoga na wahusika wanamshangilia Mwinyi Zahera.

Kitu ambacho kinamfanya ajiamulie kufanya baadhi ya mambo kwa kutaka yeye. Hana uchungu na timu kama ambavyo wengi wanavyomsema.

Huwezi kuwa na uchungu na timu kwa kuitelekeza timu yako na wewe kubakia Dar es Salaam kwa kisingizio kuwa unaenda kwenye majukumu ya mechi za timu ya Taifa wakati hata kambi ya timu ya Taifa haijaanza.

Mashabiki wa Yanga wameridhika na hili kwao wao hawana shida, hawataki hata kuhoji kwenye masuala ya msingi ya timu yao. Hawa ndiyo walitakiwa kuitwa Mbumbumbu na siyo mashabiki wa Simba.


Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x