Wachezaji wa Simba wakishangilia bao pekee la Henock Inonga dhidi ya Vipers
Tahariri

Jinsi Simba Anavyorudi Katika Ufalme Wake.

Sambaza....

Apandaye ngazi hushuka, wahenga walisema. Wahenga wametuachia semi nyingi sana juu ya mafanikio, walishawahi kusema kuwa umasikini haudumu wakaenda mbali zaidi na kusema kwamba mafanikio hayadumu endapo kama hakuna juhudi za makusudi za kuyalinda mafanikio.

Lakini ukweli ni kwamba kufanikiwa/kufikia kilele cha ubora ni ngumu sana  inahitajika mipango thabiti na mikakati kufika huko, lakini ugumu zaidi ni pale mafanikio yanapopatikana na hayaitajiki kupotea au kuanguka na kuanza upya hapo ndipo maumivu na gharama kubwa hutumika kuyalinda.

Ndani ya misimu sita ya hivi karibuni simba walifanikiwa kunyakua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara kwa miaka minne mfululizo toka mwaka 2018 mpaka 2021, kombe la Shirikisho la Azam mara mbili na walifanikiwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa hususani yale yanayosimamia na Shirikisho la mpira wa miguu Afrika CAF kwa kufika robo fainali la ligi ya mabingwa mara tatu na kombe la shirikisho mara moja.

Kikosi cha Simba kilichotolewa katika robo fainali ya kombe la shirikisho Afrika na Orlando Pirates.

Simba ilikuwa katika ubora wa hali ya juu walisifika kwa kucheze soka safi na la kuvutia kiasi cha kupewa majina ya utani kama vile Wanalunyasi ikimaanisha kwamba wanacheza soka la chini(pasi nyingi), Wanalupaso na mengine kibao, mradi wao ulikua katika ubora wake kila walichogusa au kufanya kilifanyika kwa ubora wa hali ya juu hadi baadhi ya mashabiki na wapenzi wa soka wakaafiki na kukubali kwamba Simba ni moja ya timu bora, kubwa na hatari barani Afrika.

Upo usemi usemao vizuri havidumu bali huja na kuondoka, kama wahenga wasemavyo kuwa nyakati huja na kuondoka basi ule wakati bora wa mafanikio kwa Simba ulipita na kwenda zake, ndani ya misimu miwili ya hivi karibuni Simba ilipoteza kila kitu kiasi cha kushindwa kutetea ubingwa wa ligi na kombe la Shirikisho la Azam na kuwaruhusu mahasimu wao Yanga kujinyakulia mataji hayo mawili kwa miaka miwili sasa mtawalia.

Thadeo Lwanga akifunga bao mbele ya walinzi wa Yanga katika fainali ya Kombe la FA Kigoma katika uwanja wa Lake Tanganyika na kuipa Simba kombe kubwa la mwisho.

Mradi wa Simba ulitetemeka baada kufeli katika mambo kadhaa kama vile

▪Sajili mbovu na za viwango vidogo; Hivi karibuni Simba imekua na sajili nyingi zilizofeli kiasi cha kushindwa kufikia matarajio na kuifanya timu iingie hasara. Wimbi kubwa la wachezaji wanaosajiliwa na kuachwa kila mwaka kunawafanya waanze upya kila uchwao, pili ni kubadilishwa kwa makocha mara kwa mara, kila kocha na falsafa yake hiki kinawafanya wawe wanajenga timu kila msimu kwa msimu wa pili sasa.

Mradi wa sasa wa Simba unajengwa chini wa kocha Robertinho akishirikiana na benchi lake la ufundi pamoja na uongozi wanaijenga Simba imara na wameanza na mambo kadhaa muhimu mfano;

Augustine Okrah tayari amepewa mkono wa kwaheri na Simba akidumu kwa msimu mmoja pekee.

▪Kuanzishwa kwa kitengo cha skauti; Baada ya kufeli katika sajili kadhaa katika misimu miwili ya hivi karibuni simba wameajiri skauti ambaye atafanya kazi kwa kushirikiana na benchi la ufundi ili kutafuta wachezaji sahihi kulingana na mahitaji ya kocha na kuachana na ule mfumo wa zamani ambao ulijulikana kama kamati ya usajili na kuifanya timu ifanye usajili kisasa kama zilivyo timu nyingine kubwa duniani.

▪Kufanywa kwa marekebisho katika benchi la ufundi; hivi karibuni Simba ilitangaza kuachana na baadhi ya wataalamu katika benchi lao la ufundi pengine baada ya kuona kuna utendaji hafifu katika vitengo vyao ambao ni kocha wa viungo, kocha wa magolikipa na daktari wa timu.

Hii ni ishara kuwa wanatarajia kufanya marekebisho yenye tija ambayo yatakidhi haja na mahitaji ya timu.

Ismail Sawadogo anatajwa kuachana na Simba, kiungo huyo alisajiwa katika dirisha dogo.

▪Kuachwa kwa baadhi ya wachezaji; kuachwa kwa baadhi ya wachezaji ni ishara ya ujio wa wachezaji wapya ambao watakua bora kuliko wale walioachwa. Simba imetangaza kuachana na Augustine Okrah, Nelson Okwa, Momo Outara pamoja na Victor Akpan, pengine kuna wengine watapewa mkono wa kwaheli, hii ni ishara kwamba simba wanatengeneza mradi mpya baada ya ule wa kwanza kufa na kukosa makali katika miaka miwili hii iliyopita.

Matarajio ya kila shabiki na mpenzi wa Simba ni kuona timu yao inarudi katika anga za ushindani na kufanya vizuri, pengine ni wakati wao sasa kurudi katika ubora wao tuliouzoea. Wakati ndo utaamua tusubiri tuone.

NB: Maji ukiyavulia nguo sharti uoyaoge!

Sambaza....