Blog

Kama ikishindikana Kampamba, mara 100 arudishwe Kaheza si kumsaini Kapera

Sambaza kwa marafiki....

MAJINA ya wachezaji kadhaa yanahusishwa kujiunga na Simba SC msimu huu wa usajili. Ramadhani Kapera ni miongoni mwa wachezaji hao wanaohusishwa kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania bara. Kapera amemaliza msimu akiwa na magoli kumi ( ligi kuu pekee) na timu yake ya Kagera Sugar FC ipo imeangukia katika ‘play off’ ya kuwania kubaki ligi kuu ama kushuka daraja la kwanza.

Nilitazama mchezo kati ya Pamba FC na Kagera Jumatatu hii katika uwanja wa Nyamagana, Mwanza. Kapera alikuwa akiongoza safu ya mashambulizi ya Kagera na kwa muda wote aliokuwepo uwanjani mshambulizi huyo alinifanya nijiulize maswali mengi mno, mojawapo ni , Simba imeona nini kutoka kwa mchezaji huyo ambacho atakiongeza kikosini mwao?

FUNZO…..

Msimu uliopita Simba ilikimbilia kuwasaini Adam Salamba kutoka Lipuli FC, Marcel Kaheza kutoka Majimaji FC na Mohamed Rashid kutoka Tanzania Prisons. Washambuliaji hao watatu walikuwa na msimu mzuri binafsi katika klabu zao za awali kabla ya kutua Simba lakini mara baada ya kumaliza michuano ya SportPesa Super Cup 2018-Kenya bila kufunga goli lolote uongozi ukaamua kurejea tena sokoni ni ni hapo ndipo walipomsaini Mnyarwanda, Meddie Kagere.

Kelvin Kampamba

Simba kama kweli wanahitaji kufika mbali katika michuano ijayo ya Caf ni lazima wakubali ‘kufungua pochi’ na kuwasaini wachezaji wa viwango vya juu kama kina Kagere, nahodha John Bocco na Emmanuel Okwi. Kwa namna, Kapera alivyokuwa akikimbia uwanjani, alivyokuwa akipiga pasi, akipokea mpira na kugeuka kuelekea mbele sioni kitu chochote ambacho anaweza kukiongeza katika safu ya mashambulizi ya Simba.

Simba inatakiwa kutazama mbali Zaidi hasa jinsi ya kuziba nafasi ya Emmanuel Okwi na mtu ambaye angeweza kuongeza kitu katika eneo hilo ni Kelvin Kampamba-kiungo wa mashambulizi anayetokea pembeni pale Nkana FC.

Kapera ameachwa mbali mno na kina Kaheza, Salamba na Rashid na ni heri Simba ingewarudisha kundini Rashid na Kaheza kuliko kumsaini Kapera mchezaji ambaye katika game ya kwanza ya play off alikuwa akisahau mpira nyuma! Simba wanatakiwa kwenda na muda, kwa maana usajili wa Caf unatarajiwa kufungwa mwisho wa mwezi huu.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.