Blog

Kaseja kakataa kuwa Kaseke, akakataa kuwa Singano, akabaki kuwa Kaseja

Sambaza....

YANGA, Azam Fc zimetoa orodha ya wachezaji waliowaacha. Katika orodha hizo wachezaji vijana ni wengi. Ni wengi mno. Kiufupi tu. Yanga imemuacha Deus David Kaseke, Azam Fc imemuacha Ramadhan Singano. Nasikia mashabiki zake wamembatiza jina la Messi. Sijali sana.

Wengi wameachwa wakiwa hawajafikisha miaka 26 kwa mujibu wa taarifa zao zilizoko Google. Kuna tatizo sehemu. Haiwezekani.

Wakati haya yakiwatokea kina Kaseke, mikataba ya kina Juma Kaseja ( KMC), Mrisho Ngassa, Kelvin Yondani (Yanga), Agrey Morris (Azam Fc), Shaban Nditi (Mtibwa Sugar FC) iko salama. Kuna kitu cha kujifunza. Kuna darasa la bure hapa.

Ina maana vijana wameshindwa kuwastahafisha wakongwe badala yake wakongwe wamegoma kuzeeka na wanalinda nafasi zao, mpaka vijana wanaachwa? Ni swali letu vijana tujiulize kwa pamoja. Wapi tunapokwama mpaka yanatukuta?

Kuna muda huwa najisemea ni wakati wa Yondani na Morris kupisha damu mpya katika ukuta wa Stars, lakini kila nikigeuka kulia na kushoto kutazama vijana wa kuwafanya Yondani na Morris wasicheze siwaoni. Nimetazama hili mara nyingi. Mwisho wa siku macho yangu yanarudi pale pale kwa kina Yondani na Morris.

Aggrey Morris na Bocco

Lakini ukweli mchungu ni kwamba vijana wa lika langu ni wavivu wa mazoezi magumu. Hawapendi kuambiwa haya tunayoyaandika. Wanapenda kusifiwa tu na mazoezi yao ni mepesi ambayo mwanangu hayamshindi. Wamezoea kula kiwepesi.

Jioni moja katika korido za Uwanja Taifa nilimsikia Yondani akisema anatamani kuacha kucheza Stars lakini hakuna mchezaji wa kumfanya astahafu. Niliibeza kauli ile, nikahisi Yondani anajisifu, lakini baadae nilivyoifikiria nje ya 18, nikajiona mjinga.

Yondani alizungumza ukweli. Huu ni ukweli ambao vijana wengi hawapendi kuusikia ukipenya kwenye ngoma za masikio yao. Tumebaki kusema fulani mchawi. Tunaamini uchawi katika jambo la Kisayansi. Mpira ni Sayansi, uchawi unaingiaje?

Kama mpira ni uchawi, basi wachawi wa kwanza ni vijana wenyewe. Uchawi wenyewe unaanzia hapa. Vijana hawapati muda maalum wa kupumzika, hawali vyakula vya kujenga miili, hawapendi mazoezi magumu. Huu ni uchawi mbaya tusioujua.

Ni kocha gani akupange wewe kijana uliyechelewa kulala kwa sababu ya disko amuache nje mkongwe aliyelala mapema. Akala vizuri na anapenda mazoezi magumu? Hakuna kocha huyo.

Kama vijana wanataka kuwatoa wakongwe katika nafasi zao ni lazima mienendo yao ibadilike ili mwisho wa msimu tuone idadi kubwa ya majina ya wakongwe yakikatwa, lakini kama wataendelea kuwa hivi nawaona wakongwe wakizidi kuwa wachezaji muhimu katika timu.

Bahanuzi

Pale unapomuona Kaseja na kujiridhisha kuwa amefikia mwisho, mwenzako anajiona yuko fiti na yuko fiti kweli. Mazoezi yamemfanya Kaseja kila siku aonekane mpya mbele ya mboni za watu.

Mungu akinipa pumzi msimu ujao nitaenda kumuona George Kavila akicheza ligi kwa mwaka wa 22 mfululizo. Vijana wengi wamemkuta katika soka la ushindani, cha ajabu wamemuacha. Kavila wa miaka 10 iliyopita ndiyo Kavila wa leo. Hana makuu yuko vile vile. Anajitambua. Anajitunza.

Sitaki kutaka maji mengi ya watu. Jikumbushe kuhusu Said Bahanuzi. Nani anajua aliko? Binafsi sijui kama kaacha soka au anafanya kazi gani.

Singano

Huyu Mbwana Samatta tunayemtazama kama kioo chetu hajafika Genk kwa bahati mbaya kama tunavyodhani. Aliamua kuacha kazi akafanya kazi, leo hii Wazungu wanaliimba jina lake na kumtukuza. Ni kama ‘Mungu’ wao wa mabao.

Muda huu ambao Singano anapishana na Morris katika chumba cha kusaini mikataba cha Azam, mkononi akiwa na barua yake ya kuachwa, huku Kaseke akipishana na Boban katika chumba hiko naye akiwa na barua hiyo, kuna kiujumbe fulani cha kuondoka nacho kwa hawa vijana wenzetu. Uncle Jerson Tegete nakusalimu uncle. Swalamaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x